Tufurahi tufurahi Wikiendi eh!
>> Saturday, November 25, 2006
Duh ingekuwa poa kuwa binadamu wangekuwa wanfuraha siku zote. Unamkumbuka The Cool Ruler?
Gregory Isaacs katika baadhi za nyimbo zake zinazonikumbusha mbali sana.
Duh ingekuwa poa kuwa binadamu wangekuwa wanfuraha siku zote. Unamkumbuka The Cool Ruler?
Gregory Isaacs katika baadhi za nyimbo zake zinazonikumbusha mbali sana.
Nikiwa na Spika , Balozi wa Tanzania mwenye makazi Sweden na mbunge
Jana tulikuwa tukimsikiliza Spika wa bunge. Nikipata nafasi nitaleta dondoo zilizotoka kinywani mwake.
Jacob Zuma alidai alioga kuzuia virusi baada ya kufanya mapenzi na mwanadada mwenye ukimwi.
Kwa nini binadamu anauwezo wakufanya mapenzi na mtu mwenye ukimwi kwa hiari yake mwenyewe hata kama anajua kuna kufa?Je unamkumbuka Jacob Zuma?
Niliwahi kuulizwa maisha ni nini? Swali hili nikashindwa kulijibu kwani lili nisababishia maswali mengine mengi sana. Naamini binadamu mara nyingi anaishi akitafuta maana ya au uthamani wa maisha! Kwa wengine maisha yanaanza kuwa na maana pale anapo kuwa na watoto. Hivyo watoto wake wana kamilisha au kutoa jibu la kwanini aamke asubuhi kwenda kazini au hata ajitunze. Wengine maisha kwake yanakamilika kupitia mitazamo ya kidini. Anaamini yuko hapa kwa mpango wa Mungu na hivyo basi moja ya mambo yaletayo maana kwake ni pamoja na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Anautunza mwili wake kwa sababu mwili ni hekalu la Mwenyezi Mungu. Kuna mwingine maisha hayana jibu sahihi. Hivyo ni lazima awe katika hali ambayo inamsahaulisha machungu ya maisha ambayo yanaonekana ndio pekee yana tawala maisha.Wengine wanaishi maisha yakutokujali lakini wakijua kuwa hawajali. Wengine wanaishi maisha ya kutojali lakini kwa sababu hawajui wamejiingiza kwenye nini.
Hivi ushawahi kujiuliza kwanini unataka kuishi muda mrefu?Hivi ushawahi kutamani maisha waishio Wazee wa miaka mingi? Hivi ukikumba ukimwi na maisha yako yakafupika na labda ukafa kwa kuteseka sana inakutisha? Je, ukikumba mdudu utawatesa watu wa karibu yako?
Lakini hayo yote ni maswala ambayo wewe mtu mzima unaweza kuyatafakari. Kwa watoto ambao wanakumbwa katika janga hawana chaguo kubwa. Hawana uwezo wa kuelewa hata wamekumbwa na nini!Hawajui ngono wala nini! Je unawakumbuka hawa watoto wanao kumbwa katika janga kama hili?Mimi sijui mengi lakini nafikiri angalau viumbe wasio na hatia wasiingizwe katika kasheshe litokanalo na chaguo mtu mzima mwenye akili timamu achagualo kufanya.Tujaribu kuwafikiria watoto. Tujaribu kuwafikiria watu tunao wajali. Hivi wewe unamjali nani?Je, uko tayari kivyako au ukishakufa ndio imetoka hiyo ndugu na jamaa watafanya mambo?
Angalia nyumba hii ya Rehema hapo Kenya:
Baadhi ya Mafuvu ya waliokufa baada ya Khmer Rouge kuamua watu wote wawe wakulima.
Nimejikuta katika siku za karibuni nikiingia katika mijadala ya kilimo. Baadhi ya watu wamekuwa wakifikiri kuwa nabisha kuwa kilimo si muhimu hasa baada ya kusema kwamba siamini kuwa matatizo ya Tanzania yana jibu moja kama baadhi ya watu wapendavyo kutaja kilimo kama ndio jawabu pekee. Mwanablogu Luihamu alifikia mpaka kutunga shairi akitaja jina langu na la Ndesanjo kuhusiana na maswala haya ya kusisitizia umuhimu wa kujali umuhimu wa nyenzo nyingine katika kutatua matatizo ya Tanzania. Bado hapa napenda kukazia kuwa tunahitaji kila ujuzi ilikuweza kufanikiwa Tanzania. Mkulima alivyo muhimu ndio hata mwana tekinolojia, mwana sayansi ya jamii, mfanyabiashara, nesi , dakitari na taaluma zote zilivyo muhimu katika kujenga nchi yetu.
Nimeona labda nikumbushe watu historia kidogo igusayo maswala yawezayo kutokea kama mkazo wa mambo ukiwa katika eneo moja liaminikalo kuwa hilo pekee ndio njia. Naamini kuwa binadamu kama angeweza kujifunza kutoka katika makosa basi kunauwezekano wakutopoteza muda katika kutafuta matatuzi mengi tu. Siamini kuwa ni lazima kila mtu apitie katika makosa hayohayo wakati unaweza kujifunza kwa makosa wengine waliofanya. Sidhani ni mpaka ushike moto iliujue unaunguza.Naamini mambo mengi tunaweza kujifunza kutokana na kutafakari mafanikio na makosa yetu na yale ya wenzetu hapa duniani. Naamini kwa kufahamu vikwazo na virahisisha mambo ambavyo twaweza kujifunza kutoka kwa wengine tunapata muda wa kuweza kukwepa kurudia makosa na kukazia miundo mbinu ituwezeshayo kuyakabili mazingira yetu na matatizo yetu. Naamini kama Watanzania tunamengi tumefanikiwa na mengi tumekosea na tunazidi kukosea. Ni kweli kama Watanzania si kweli majawabu yote au njia zote walizopita watu wengine basi nasi zitatufikisha paradiso.Ila naamini kuwa kuna mengi twaweza kujifunza kupitia machambuzi ya ni nini wenzetu walifanya na wanafanya katika kutatua matatizo yao. Mara nyingi tunakazanina kujifuza kutoka katika nchi zisemekanazo kuwa zimeendele. Mara nyingi tunasahau kuangalia nchi nyingine ,hasa hatutaki kujifunza kupitia makosa ya wengine. Ili Tanzania iendelee tunahitaji busara zitokazo kila pande na sio tu zile tu ambazo twafikiri ni za nchi zisemekanazo ziko dunia ya kwanza. Leo hii nimechagua Cambodya na China katika historia .
Tukiachilia mbali siasa na mambo mengi yaliyo izunguka Cambodia, utakutakuwa kitu ambacho uongozi wa Khmer Rouge ulitakakufanya ilikuwa ni kuikomboa Cambodia. Walifikia hatua ya kulazimisha watu kwenda vijijini, na kuwa lazimisha wawe wakulima. Ili kuhakikisha kuwa wanapata tabaka la wakulima walitengeza sera zitakazo wapa watu wapya wenye misingi ya kazi ya ukulima au kwa Kiingereza "New People" through agricultural labor. Wakafanikiwa kufuta pesa na mabenki. Wakafuta maswala ya shule na kulazimisha watoto wa mjini wawe wakulima kijijini. Wale wenye elimu walionekana wameambukizwa fikira potofu hivyo wakauawa na wengine kwenda jela. Lakini kwa ujumla walichokuwa wanajaribu kufanya ilikuwa ni kuikomboa nchi wakiamini kuwa kilimo tu ndio njia pekee. Sishangai kuona jinsi gani walishindwa. Lakini kitu nachokistukia ni kwamba mpaka kwenye blogu zetu nakutana mara nyingine na hoja ambazo zinaonyesha kuwa kuna watu bado wanaamini kabisa katika hoja ambazo zina fanana fanana na Khmer Rouge. Nadhani tunakumbuka hata maswala ya vijiji vya ujamaa. Sasa wakati tunajadili kuwa kilimo ndio jibu pekee kama Mzee Luihamu asemavyo tukumbuke basi na baadhi ya mambo yaliyotushindwisha kufanikisha vijiji vya ujamaa . Tukumbuke basi na mambo yaliyoishindwisha Khmer Rouge kuwabakiza watu vijijini . Kwa maana mara nyingi tunawanyoshea watu vidole wakiwa vijiweni mijini bila kukumbuka kuwa kuwapo kwao vijiweni ni matokeo ya tatizo na sio kiini cha tatizo.
Tukienda China, ni vizuri kumkumbuka Mao Tse Tung na kitu chake alichokiita Hatua Kubwa Mbele(The great leap Forward).Yeye aliamini kuwa ilikwenda mbele basi lazima kuingilia maswala ya viwanda kwa nguvu zote. Watu wakalazimishwa kutengeneza chuma majikoni mwao.Chuma ilikuwa ndio ufunguo wa maendeleo.
Posta la propaganda za Mao likikwa mbia ujanja katika kutatua uchumi ni chuma. "Take steel as the key link, leap forward in all fields".
Hatua nzima aliifanyia kazi bila kuwa na ukweli wa mambo ya jinsi gani mambo yafanyike. Hivyo asilimia kubwa ya mambo watu waliolazimishwa kufanya hayakuzaa matunda. Mashamba hayakutosheleza chakula kwa watu. Viwanda havikuweza kuzalisha bidhaa bora. Watu wakafa njaa. Inasemekana katika kipindi hiki hata ndege karibu waishe China kutokana na amri ya kuwaua kwa sababu ya kuamini wanakula mazao. Kutokana na kuua ndege wadudu kibao walizidi kutokana na kukosa maadui wakuwazuia kuzaliwa kwa wingi kupita kiasi. Haya yote huonyesha jinsi gani jambo moja laweza kuzua tatizo jingine kama mipango na utekelezaji wake ni holela.
Sasa kwa nini naongelea mambo yaliyopita? Si ni ukweli kuwa Tanzania sio Cambodia wala China? Jibu ni ndio. Lakini katika kipindi hiki ambacho ni lazima tuende mbele bado kuna mambo mengi yanayoamuliwa na viongozi wetu kienyejienyeji tu.Sasa matokeo yake ni kwamba tuna weza tukajikuta tunaendelea kufanya majaribio(experiments) na maisha ya watu na nchi ilimradi tu kesho inafika.Tukumbuke kuwa bado Tanzania tunahitaji kiongozi mwenye nguvu awezaye kufanya maamuzi kwa faida ya nchi . Lakini naombea kiongozi huyo asiwe kama wa Khmer Rouge au kama Mao ambaye pamoja na mengi kuna mambo mengi alikuwa anayaamua bila kujua athari zake zitakuwa ni nini. Je , unafikiri viongozi wetu wamejifunza kutoka kwa mapungufu ya Viongozi wa Tanzania waliopita? Au ndio mambo ya kutunza statasi quo? Je viongozi wetu wanajifunza jinsi gani nchi kama China ilistukia tatizo na kugeuza mwelekeo?Je tumejifunza kwanini hawakurukia ubeperi kama wa nchi za magharibi kama USA na Uingereza? Je, Kikwete ndio kiongozi wetu atakaye tatua tatizo?
Kutokana na kuchelewa mkutanoni kutokana na matatizo ya kiufundi nimeona niandike tena kile ni lichokuwa nimechelewa kukipa sauti yangu kuhusu mkutano wa wanablogu.
1. Mikakati ya Kufikisha Ujumbe wa Wanablogu kwa Watu Wengi Zaidi:
Nakubaliana na yaliyo jadiliwa kikaoni. Lakini ningeshauri kuwa kuwepo ndani ya jumuia kamati yenye kufuatilia yenye 2/3 ya watu walioko Tanzania wenye kazi ya kufuatilia nukuu zizungumzwazo katika magazeti redio na Televisheni ili wote wanablogu ambao hatutakuwa tuna jua wamenukuu nini nadani ya Tanzania tuweze kujua kuwa tumenukuliwa kisahihi. Pia kama tumenukuliwa vibaya au kutokueleweka tuweze kupata nafasi ya kujitetea au hata kusawazisha vyombo vya habari kwakutu nukuu vibaya.Member waliobaki watashughulikia maswala ya Wanablogu kama wanukuliwavyo nje ya Tanzania.
2. Maadili:
Nakubalia na na mawazo yaliyotolewa kikaoni.Lakini lazima uhuru wa mwanablogu kusema apendacho lazima ubakizwe. Lugha safi ni muhimu lakini itambulike watu tofauti huchukulia kuwa wametukanwa katika vigezo tofauti. Mimi nashauri lugha ambayo ikataliwe ni ile tu ijumuishayo matusi ya nguoni. Pia mtu yeyote ndani ya jumuiya atakaye fikia kumdhalilisha mtu au nchi kwa kutumia blogu yake bila sababu maalum ambayo anaweza kuzitetea atolewe kwenye aggregator na pia hoja zake zikanwe na kamati maalum ya maadili. Nashauri atolewe ndani ya aggregator kwa muda wa mwaka na ikiwezekana wanajumuiya kumtoa katika viunganishi vyao. Kurudi kwake katika jamii kutokane na kuomba kwake msamaha kwa aliye dhalilishwa kwa kuandika hivyo kwenye blogu yake.Pia lawama za adhalilishawe ziwekwe kwenye tovuti ya jumuiya.
Picha ziwezazo kumdhalilisha mtu pia ziangaliwe.Lakini kama zina ukweli wa hoja zinazoweza kutetewa kwa mtazamo wangu zinaruhusiwa.Ila maswala ya picha za ngono na wasiwasi yanaweza kuteteleza madhumuni ya jumuiya nzima kwa kusababisha kuhusisha na kupotosha mwelekeo wa jumuiya nzima.Sipingi kuwepo kwa blogu za ngono Tanzania kwa sababu ngono ni jambo linalotakiwa kuongelewa, lakini mpaka sasa sijaona blogu ya ngono ambayo inaelimisha Mtanzania maswala ya ngono. Nashauri blogu ya ngono itakayo kubalika ni ile tu ambayo hailengi udhalilishaji wa mtu yeyote na yenye ujumbe uhitajikao katika jamii. Kwa mfano mimi naweza kuikubali blogu ya ngono iwafundishao vijana uroda na madhara yake na jisi ya kuuvinjari kiusalama na kiafya. Blogu za ngono ziwekayo picha za watu ambao hawakutoa idhini ya kutolewa picha zao na kwa madhumuni ya kuwaletea washawasha na ashki wasoma blogu na isiyofundisha mimi nadhani zisikubalike kwenye jumuiya.
Kusiruhusiwe kutukania watu dini zao.Lakini isije tu ikafikia kuwa maswala ya dini ni mwiko kuyaongelea.
Kamati ya ushauri wa maadili iwe inatoa mawazo ambayo wanajumuia watayapigia kura . Kwa mfano ili mtu kutolewa kwenye jumuia ingekuwa vyema kuwe na wiki nzima ya wanablogu kupigia kura uamuzi.Hii ingefanyika kama tulivyo pigia kura tarehe ya siku ya blogu.
3. Jumuiya:
Naunga mkono swala lakuwa na jumuiya iliyo sajiliwa. Naamini itatoa nguvu zaidi kwa wanajumuiya hasa katika maswala ya haki za wanablogu na kazi zao na pia maswala ya kuaminika.(credibility).
Katika tovuti ya jumuiya kuwepo na muhtahsari wa yaliyosemwa katika vyombo vya habari kutoka blogini.Pia kuwe na nyumba ya kuchat na forum ambayo itawezesha wanablogu kukutana mara kwa mara ikiwezekana wakitumia majina watumiayo kwenye blogu zao.Kuwepo na ukurasa wa maoni ya wanablogu na chumba cha ushauri kwa jumuiya ya wanablogu. katika chumba hiki mambo mbali mbali ambayo yanapendekezwa kufanyiwa kazi na kamati ya jumuia yatawekwa wazi.
4. Uongozi:
Nakubaliana na Uongozi wa muda ulioteuliwa .Ningependa jina uongozi lisitumike bali tutumia jina la wawakilishi.Tuwe na kamati ya wawakilishi katika kamati mbalimbali.Kwa mfano tuwe na kamati ya maadili. hii itafuatilia kuwa tunafuata miongozo tunayopanga yakutuongoza kuendelea kuwa huru lakini sio kuwa vyomo vya chuki na kashfa kwa watu. Tuwe na msemaji mkuu ambaye ndio atakuwa anahakikisha kuwa hata katika mikutano yetu hatupitilizi kupita wakati. Tuwe na kamati ya ustawi wa blogu za kitanzania. Hii itahakikisha maswala ya muonekano wetu na ni kwa jinsi gani tunawakilishwa katika vyombo vingine vya habari. Kamati zote ziwe na watu watano. Kwa sababu ni kawaida kwa wanablogu kuzidiwa na shughuli wakati mwingine hivyo kukosa muda wa kufuatilia mambo au kuandika mambo . Tuwe na kamati ishughulikiayo maswala ya elimu ya teknolojia hii ya kublogu na jinsi gani wanablogu na wananchi wataweza kujiboresha zaidi katika matumizi yake. Hapa na maana maswala ya uboreshaji wa blogu zetu na pia maswala ya ufundishaji au uelimishaji wa maswala ya blogu.Kuwena msemaji mkuu wa jumuiya ambaye yeye kwa kupitia ushauri wa jumuia nzima anaweza kuisemea jumuiya ibidipo.
Kuwe na kamati maalumu inayofuatilia jumuiya kama NGO. Hii itakuwa inafuatilia pia jinsi gani tunaweza kujenga akauti ya Jumuiya itakayo wezesha maswala yatakayo hitaji pesa . Mfano, ikiwa mwanablogu yuko matatizoni kutokana na mambo aliyo wakilisha bloguni.Mfano ikiwa tutahitaji kuwa na fund yetu kama wanablogu ya kusaidia maendeleo ya kitu tukubalianacho.Iwe ni watoto yatima au uhuru wa habari nk.
Kuhusu Jina ningependa katika kila kitu tutumie majina ya Kiswahili. Jina la jumuiya mimi na shauri liwe:
Jumuiya Ya Wanablogu Tanzania(JYWT).
jina la Aggregator, mimi ningepenga jina liwe la Kiswahili au Kifupi cha jina la Kiswahili
Mfano wa majina niyafikiriayo ni:
Bloguni Wasemaje(BW)
Sauti za Watanzania Bloguni(SWB)
Kipya Katika Blogu za Watanzania(KKBW)
Kuhusu muda wa wawakilishi kuwepo katika kamati ningeshauri muda wa miaka miwili . Kila baada ya miaka miwili tungepiga kura kuchagua wanakamati wapiya au kuwabakiza wale ambao tunaona mchango wao una umuhimu wakuendelea kwa muda mwingine.Kuwepo na uwezekano wa kuitisha kikao cha dharura cha kutengua uwakilishi wa mtu katika kamati. Kwa ujumla jumuiya ibakie kuwa ya wanablogu wote hakuna kiongozi wala afuataye bali wote kwa pamoja tukienda mbele. Wawakilishi wanapewadhamana kuwakilisha wanablogu kurahisisha ufanisi wa jumuiya tu. Ila ni wajibu wa jumuiya nzima kuhakikisha kuwa tunakuwa nguvu ya kuelimisha , kuhabarisha, na ya kujikomboa.
Naamini mila na desturi zetu wabongo bado zina nguvu sana ingawa watu wanadai hizi ni zama ya bongo fleva. Naamini kuwa katika shule zetu za jadi mbinu mbalimbali zilitumika kuwezesha mambo fulani katika jamii kwenda shwari na kulindwa kwa nguvu zote na jamii. Mimi ni mchanganyiko wa Kipare na Kijita na katika makabila yote haya mawili njia za kuelimisha zilitumia mbinu nyingi ikiwa pia na vitisho. Mfano kwa Wapare maswala ya kufundishwa kuwa mwanamume wa shoka yaliendana na vitisho na maumivu. Kama wewe ni mwanamume basi lazima uweze kuvumilia maumivu .Nadhani kwa walioenda jando watakumbuka! Kulikuwa mpaka kuna simba wamsituni akumezaye ukishindwa kufanikisha mambo fulani ya kidume. Hii maana yake ulikuwa unauawa ingawa ilidaiwa umeliwa na Simba. Sasa njia hizi za kutufundisha heshima , maisha na hekima nyingine nyingi zikajakuuawa na wakoloni na wengine walioleta tamaduni mpya. Basi unaweza kudhani kwa sababu Wakoloni waliua shule za jadi basi na baadhi ya mambo tuliyokuwa tunatishiana yamekwisha!Utadhani mpaka sasa tumeweza kuelewa au hata kujiuliza ni kwanini mambo mengine yalitishalo kabila moja, hayalitishi jingine hata hivi sasa baada ya makabila ya Tanzania kuchanganyika na kutawanyika katika mikoa mbalimbali . Jibu bado tukopalepale. Tunaamini wachawi wanapaa na ungo ingawa hata kushuhudia hatuja shuhudia. Tunaamini kibibi fulani kichawi kwasababu macho yake mekundu bila kushuhudia aliyelogwa. Tuna chanja na kuvaa hirizi kibao bila ya uhakika hata wa ni nini hasa tunakiogopa.
Sitaki kukataa kuwa hakuna uchawi kwa sababu hili ni jambo lililorekodiwa miaka mingi tu na vitabu vingi vimelizungumzia. Lakini mimi ninachoamini ni kwamba uchawi mkubwa ni hofu ya kibinadamu itokanayo naupungufu wa kibinadamu wakutokujua. Na upungufu huu kwa bahati mbaya hauna dawa. Upungufu huu umefanya wengine waabudu miti ili kuujazia, wengine Yesu, na Wengine Mtume Mohamedi. Tatizo jingine la upungufu huu uko kama njaa, kila siku unahitaji kupewa chakula ilikujazilizia pengo la upungufu wa kibinadamu ilikupata uhaueni. Mimi naamini pamoja na kuwepo wachawi, moto wa ahera na mambo yote hayo, lakini upungufu wa kibinadamu wenyewe hulenga binadamu kitofauti kutokana na binadamu mwenyewe alivyo na mazingira yake katika kumuelekeza binadamu huyu kuamini nini kinampa ujazo na uhaueni. Basi utakuta huku wanaogopa makaburi, kule wanaogopa mbuyu na hata wengine kukimbia vifuu vya nazi kutokana na mazingira yao. Basi unaweza ukakuta kutokana na mlengwa hirizi ikajazia na kuziba hofu hiyo, dini au hata kujinyonga. Naamini ubongo wa binadamu unanguvu kiasi kwamba hufanyia kazi hofu za binadamu na kuzipa uhai na uhalisi.Na naamini asilimia kubwa ya wajulikanao kama wachawi, waganga wa kienyeji au hata uchawi wenyewe haukuthibitika ingawa una uhalisi. Halafu si kweli zote ni zakufundisha maana nyingine ni zakutishana kwa madhumuni yakutishana tu.Na nyingi za mila na desturi hizi hatakama zilikuwa zinafundisha zamani hazina mchango mkubwa sasa hivi katika kuifundisha jamii ya leo.Na kama kuna sababu zakuzikubali hizi dini za kuletwa moja ni kwamba kwa sasa ndio zimeshikilia ukanda katika kuipa jamii muelekeo, ingawa hata kwa hili sina uhakika zitaweza jukumu hili mpaka lini kama jamii haifumbui macho nakuelewa mchango wake bila ya kukariri na kufuata kiulimbukeni.
Lakini hizi mila za kutishana kwa dhumuni la kufundisha kitu haziko afrika pekee. Na rafiki yangu Myahudi alikuwa anatishwa na wazazi wake asiweke Tattoo kwa sababu hata weza kuzikwa kiyahudi akiwa na tattoo, kitu ambacho baadaye akagundua hakina ukweli. Nakumbuka pia nilipotembelea Russia mitaa ya Viborg nishawahi kuwatisha wenyeji wangu kwa kuwa nilipiga mluzi ndani ya nyumba na wao waliamini kabisa kwa kupiga mluzi ndani ya nyumba unaleta bomba la balaa. Kitu ambacho mimi siamini, kwani mimi nilifundishwa usipige miluzi porini. Hivyo hizi mila na desturi ambazo zina mambo haya ya kutishana haziko Afrika tu. Duh !Unakumbuka kitabu kiuzacho kuliko vyote siku hizi cha Harry Potter kinastori gani za kichawi?
Sasa ngojea nikupe stori fupi kuhusu uoga wangu wa makaburi.
Nakumbuka tokea utotoni nilizoea kusikia habari za kutisha kuhusu maeneo ya makaburini. Nakumbuka kunakipindi nilikuwa nang'ang'ania kutokwenda kulala mapema ilikuendelea kusikiliza stori za wakubwa, basi ilikutaka kunifanya niondoke wanaanza kusimulia stori za kutishatisha. Sehemu kubwa za stori hizi zilikuwa zinalenga maswala ya majini mashetanishetani na maeneo ya stori yanakuwa makaburini. Basi nisitake kukuongopea mara nyingi ilivyokuwa inaingia giza nilikuwa natishika kukatizia njia yoyote inayokatizia makaburini.Kilichokuja kunishinda ni pale nilipokuwa natembelea Upareni kwani kule ni kawaida kabisa marehemu kuzikwa katika eneo la nyumba. Sasa kutokana na kukulia mikoani ambako kunatamaduni za kuogopa maeneo ya makaruri ilinichukua muda kidogo kuzoe mpaka kuona ni kawaida.Kama nakumbuka vizuri Wachaga nao hawana uoga sana na makaburi hivyo nadhani kwa waogopa makaburi wanaweza kupata taabu sana uchagani na Upareni pia. Lakini akipata tabu Uchagani atatokwa na jasho akikatiza katika anga kama za Ufini ambako kuna mpaka siku katika mitaa ya krismasi ambapo makaburini ndio pakwenda sio kikilio bali kimatembezi.
Mila na desturi zetu nyingi ni nzuri lakini hatuzisomi na kuzielewa sasa hivi tunapo ingia katika tamaduni za bongo fleva. Tatizo linalojitokeza ni kwamba mila nyingi nzuri zitapotea, halafu na zipo mila na desturi nyingi zisizo na manufaa sana kwetu tutaendelea kuzitunza. Bahati mbaya mila ambazo zitatunzika ni zile tuziogopazo! Je ukimchungulia mtu mzima utapofuka macho?Je , utakwenda pikiniki makaburini?
Katika vyombo vya muziki nivizimiavyo ni Bezi gitaa. Halafu si siri miziki ya jazz ni moja ya miziki niitumiayo kusafiri katika ndoto za mchana(day dreams) na pia nikiwemo ndani ya treni ya mawazo.Nisikufiche Majazz yanapanda hata wakati nafanya kimbunga cha ubongo(brain Storming). Sasa huyu Mkameruni ni miongoni mwa wanamuziki wa kiafrika ambao wanatambaa katika miziki niipendayo kisawasawa.Anatambaa kuanzia Afro mpaka kwenya klasiko Jazz bila shaka.Hebu msikilize kwenye solo hii hapa chini:
Kama nilivyosema huyu katika wapiga Bezi gitaa waafrika huyu Richard Bona ni miongoni mwa naowahusudu. Tarehe saba mwezi huu nilifanikiwa kuona shoo yake na kuongea naye. Alichonizingua alipojua tu natokea Tanzania akaniauliza unatokea Bagamoyo? Swali hilo ingawafupi lilinidhihirishia kuendelea kutambulika kwa wasanii watokao Bagamoyo. Kwa maana sasa ni mara nyingi nikikutana na wasanii waaminikao katika fani kutoka nchi kibao tu wanakuwa wanajua kuhusu Bagamoyo. Bahati nzuri safari hii nikikutana na Richard Bona, nilikuwa na Msanii mahiri wakibongo, ambaye najua ipo siku Tanzania itamjua aitwaye Menard Mponda , hivyo halikuaribika jambo.
Richard Bona akikupa kile kibao kiitwacho 'Engingilaye'
Dr James Naismith akipozi na gozi la mpira wa kikapu enzi hizo
Kwa wapenda michezo naamini mnamkumbuka huyu daktari aliyebuni mchezo wa Basketi Boli. Ninachojiuliza ni kwamba katika mazingira ya kwetu tumetosheka na michezo iliyopo ambayo mingine hata kutokana na umasikini hatuwezi kushiriki? Nakubali tunamichezo mingi Tanzania. Nakubali tuna michezo kuanzia bao mpaka mieleka ya asili. Je, katika shule zetu bado kunaruhusiwa ubunifu wa michezo ili kukidhi matakwa ya mazoezi ya viungo ya Wanafunzi? Nakubali kuwa tuendelee kuipa kipaumbele michezo hii ambayo inashindaniwa kimataifa duniani. Nakubali kuwa huyu Dr J Naismith alibuni mchezo huu kuwaondoa wanafunzi kuboreka wakati wa kipindi cha baridi(winter) ambapo wanafunzi walifanya mazoezi ndani ya maholi. Lakini kwa Tanzania naamini kuboreka kwa wanafunzi katika maswala ya mazoezi kupo sana.Je hii sio changamoto ya kuchochea haja ya mchezo mpya? Na sasa hivi vijana wengi wanaacha kabisa kufanya mazoezi na kubobea mbele ya Luninga kujadili mechi za Uingereza. Sawa, inawezekana hawa ni wachache wafanyao hivyo. Lakini unaonaje muelekeo wa vijana kwa ujumla ukiweka mazoezi ya viungo kama kigezo?Labda hatuhitaji mchezo mpya!Labda ni kibano cha maisha kisababishacho kushuka kwa ushiriki kikamilifu katika michezo kwa vijana! Lakini nchi nyingi ni hasa wenye kibano ndio wanaibuka kuwa kiboko katika michezo. Ukienda Brazili akina Pele ni ushahidi.Inabidi kuangalia tena uhamasishaji wa michezo, mfumo mzima na streteji za kufanikisha michezo bongo. Naona Raisi Kikwete anapenda michezo sio kama Mwalimu Nyerere ambaye pamoja yake mazuri mengi aliyofanya, alishindwa kuona umuhimu wa michezo kama silaha moja wapo ya kujenga Utaifa. Labda hatuhitaji Dr Naismith wa kibongo!Nawaza tu usiogope!
Kila siku ukitazama au kusoma habari utasikia kasheshe za mikwaruzano duniani. Mambo mengi ya vita na majanga utayaona yakiwa kurasa za mbele za magazeti. Cha kushangaza ni kwamba baadhi ya mikwaruzo hii utaiona inaendeshwa na watu wanaosema ni wanadini zipendazo amani. Kinachoshangaza ni jinsi gani hizi dini zisemekanazo ni za amani zilivyokuwa na misingi ya utenganishi. Au hivi ni hawa wanadini tu ambao uzigeuza hizi dini kuwa chanzo cha utenganishi?
Hebu tuangalie baadhi ya chokochoko hizi:
Israeli na Wapalestina ni kawaida kabisa kuwakuta msitari wa mbele katika kupigana. Hawa pamoja na mambo mengine tofauti za dini zao ni moja ya jambo kubwa lifanyalo wabwengane. Hivyo hapa tunawakuta wale wenye dini ya kiyahudi wanabwengana na waislamu. Na wameanza zamani! Je, unawakumbuka Falashas au Beta Israel?Hawa ni wale Wahahudi Wakiethiopia. Kuna theori zinaeleza uondokaji wao baada ya ufalme wa Judah kugawanyika mara mbili na baada ya Jeroboam kumrithi Mfalme Solomon.Na baadhi ya mambo anukuliwayo ni pamoja na dini yao. Nilipenda kuwagusia kidogo Waisraeli hawa weusi hapa kwasababu mpaka leo wana mikwaruzo ya kidini Ethiopia.Na pia mzungukowao wakukimbia Israel mpaka sasa hivi warudishwapo Israel umejaa mikwaruzo ya kidini. Wako bado mafalasha kwa maelfu ndani ya Ethiopia ambao wanasubiri kuchukuliwa kwenda Uisraeli.
Waisraeli weusi ndani ya Ethiopia walikuwa na mikwaruzo na wakristo na waislamu pia. Wako ambao walilazimika kubadili dini na sasa wanarudia uyahudi ambao wanaitwa Falash Mura. Lakini wapo wanaoamini kuwa baadhi ya Falash Mura wanarudia Uyahudi ilikuweza kurudi Irael. Chaajabu ndani ya Israel wanabaguliwa kwa rangi na hata kidini na Wayahudi wa kiothodoksi.Wayahudi wakiothodoksi wanaamini Mafalashas kuwa sio wayahudi kamili.
Tukiondoka mashariki ya kati ambapo kasheshe liko wazi tunaweza kukatua mitaa ya Marekani kusini. Ukienda nchi kama Brazili , mikwaruzo ipo kati ya Wakatoliki na Maprotestanti. Hili utalikuta kwa Waairishi pia ndani ya Ulaya.
Ukienda India utakuta kasheshe iko kwenye Wahindu na Waislamu, Wahindu na Wakristo, Waislamu na wakristo bila kuwasahau Wahindu na Masikh. Ukidondoka Pakistani utakuta kasheshe kati ya Waislamu na Wakristo, Waislamu wa Sunni na Shia.
Ukienda Australia utakuta mikwaruzano kati ya Wakristo na dini za Kiaborijini na pia na waislamu pia.
Kwa haraka haraka utakuta kila kona ya dunia kuna mikwaruzo ambayo waiendeshao wanadai wako ndani ya dini zipendazo amani. Sasa ni nini kiko ndani ya dini hizi ambazo zafanya wanadini wakwaruzane bila upendo?
Sijaisahau Tanzania katika hili. Dini inayoonyesha kutulia kuliko zote ni ya kipagani ndani ya Tanzania. Sijawahikusikia wasio kwenye dini za amani zilizoletwa wakichimbiana mikwala na wenye dini. Sijawasikia wakilalamika kutoalikwa kwenye ubwabwa na Raisi Jakaya kikwete. Tanzania kuna chokochoko kati ya Waislamu na Wakristo.Kuna misingi ya chikochoko ndani ya makanisa mbalimbali. Kila thehebu hutakakuhalalisha ukweli wake kwa kujenga hoja za kukosoa jingine.Hivyo timu zipo umekosekana uwanjatu na mashabiki.
Ukirudi Israeli , Mafalasha wanabagulia na wanadini wenzao wayahudi wakiothodoksi. Ukirudi Iraq waislamu kwa waislamu wanabwengana kwa misingi ya nani ni msunni na nani Mshia. Kunakipindi ilinishangaza mitaa ya Kilimanjaro kukazuka mpaka ugomvi kati ya Waluteri na Waluteri wenzao.Kisa wanagombania dayosisi iliwaendelee kumtukuza Mungu wa amani. Sasa sababu zinasemekana kuwa ziko nyingi! Sasa sitashangaa kasheshe likizushwa kutokana na sababu hizi zisemekanazo kuwa nyingi!Chakusikitisha ni kwamba watu tunashindwa kujifunza kutokana na mikwaruzo hii ambayo mingine ni ya maelfu ya miaka. Pale Juu niligusia zaidi swala la Beta Israel kwasababu unaweza kustukia jinsi gani misingi ya amani ikawa inakuletea mikwaruzo anga zote za dunia uamiako.Nazidi kujiuliza, kwanini dini zetu za amani zinaleta utenganishi namna hii? Je Tanzania tutaponyeka kuingia katika kasheshe kubwa zaidi ya tuliyonayo sasa kutokana na dini hizi za amani?Sijui , niko bado ndani ya Treni hii ya mawazo
Wakati najiandaa kwenda kumuona Oliver Mtukudzi leo hii, nimejikuta napitia miziki ya kiafrika kibao ambayo imenisaidia kupitisha siku za shida na raha. Bado napooza kichwa katika behewa hili la mawazo kwa kuwasikiliza zaidi Oliver na pia Manu Dibango. Hivi, unakumbuka ile Soul Makossa?Mimi nilikuwa naiimba kiswahili yote.
Oliver Mtukudzi akikupa Ndakuvara
Manu Dibango akikupa Soul Makossa
Ed Bradley
Huyu mwanahabari Ed Bradley amefariki Alhamisi hii.Leukemia imemuondoa hapa duniani. Huyu ndie aliyekuwa ananipamotisha sana hasa nikiwa namcheki katika kipindi cha 60 minutes. Ni miongoni mwa watu weusi wachache walioweza kuingia katika vipindi vya televisheni vilivyo maini strimu kabla mambo ya cable tele hayajavinjari Marekani. Kuna kauli moja aliyowaikusema iliniingia sana. Alisema kisa cha yeye kuingia sehemu ambazo watu weusi walikuwa wanaamini haiwezekani ilitokana na wazazi wake kuwa wanamwambia tokea utotoni kuwa:mtu unaweza kuwa chochote utakacho. Akamalizia kwa kusema :unajua ukiwa unaambiwa kila siku jambo hilo unaanza kuamini katika hilo. Mimi nakubaliana kabisa na hilo. Sisemi kuwa ni rahisi lakini ni jambo lenye ukweli ndani yake. Sasa mara ngapi unasikia katika bongo yetu mzazi anakazana kumwiita mtoto wake pumbavu , huna akili, nk?Mimi nilichojifunza kutoka kwa Ed ni kwamba mtoto huanza kuamini katika hilo na kuanza kukosa kujiamini. Ni sawasawa tu na jinsi watu wengi weusi wasivyojiamini hasa watu wa rangi nyingine wakiwa katika anga kutokana na kuitwa pumbafu hujuikitu.
Pumnzika ED!
Najiuliza ktu kwanini watu tunapenda kuonyeshana meno tukidai kuwa ni tabasamu? Unafiki mkubwa umejaa na chuki ambazo zinafichwa nyuma ya meno yaliyokenuliwa.Lakini Je kila anayetuchukia angekuwa anatuonyesha dunnia ingekuwaje?
Nasikiliza Uhuru Mweusi wakikwambia Dont show me your Meno Plastic smile can't work
Black Uhuru 1981
Mimi sina jibu hilo. Waulizeni ambao unahisi wangeniunganisha katika blogu zao. Lakini hata katika blogu yangu sijamuunga kila mtu.Lakini si umenipata?Kumbuka hapa ni katika treni ya mawazo. Maana yake hakuna majibu sana.Kama maswali tu!Utayapata.
Moja ya picha imuonyeshayo yesu kama mtu mweusi.
Hivi karibuni sinema mpya ya kimarekani imetoka ikimuonyeshaYesu kama mtu mweusi. Sinema hii inaitwa The Color Of The Cross. Kuhusu swala la kwamba Yesu alifananaje ni swali ambalo limeulizwa na kuchambuliwa kwa miaka kedekede. Nachojiuliza ni kwamba , hivi kwanini watu wanahangaika sana kujua Yesu alifanana vipi? Hivi hii sio hali ileile ya watu kutaka kujifananisha na waliofanikiwa? Hivi hali ya watu kutaka kujulikana wanauhusiano na mtu maarufu, au wanafanana na mtu maarufu sio dalili ya udhaifu katika idara ya kujiamini?
Katika sinema hii kunakipengele kihusishacho rangi ya Yesu kama sababu nyingine yakumthulubu.Sijaiona hii sinema bado.Wewe je?
Cesaria Evora hufanya maonyesho yake bila viatu akiashiria kukumbuka akina mama na watoto masikini waishio kisiwa atokacho cha Cape Verde
Siku chache zilizopita nilifanikiwa kumuonatena Cesaria Evora akifanyaonyesho lake maridadi kama kawaida yake. Huyu mama ajulikanaye kama DIVA MTEMBEA PEKU(The Barefoot Diva), ananiua sana awezavyo kudaka watu kwa sauti na uimbaji wake , nakuwafanya wakae chini kimya kusikiliza wakati hakuna anayejua anasema nini. Zamani wakati wa ndombolo,nyimbo za kihindi na hata za magharibi, nilikuwa bingwa wakuzitungia maneno ya kiswahili. Nakumbuka wengi tu tulikuwa tunaimba nyimbo kama: Maiko Jaksoni njooo, sitakiiii, kama hutaki nenda!Nyimbo ambazo tulikuwa hatuelewi zinaongelea nini , lakini zinachezeka. Kwa sababu zinachezeka basi maswala ya ujumbe yalikuwa si muhimu. Ila huyu mama anachonizingua ni uwezo wake wakukukalisha chini hata kwa masaa mawili akikuimbia na ukatulia na kuingiwa tafakari za kila aina mpaka unastukia anawaaga.Akiaga hapo ndio unastukia kuwa kumbe alikumeza na muziki zaidi ya masaa mawili. Kutokana na hilo husafiri duniani kote na kuimba akipokelewa kwa mikono miwili bila tatizo.
Sasa nani alisema kuwa kwa kuimba kiswahili tutashindwa kuwa na wasanii ambao wanaeleweka duniani? Naamini kama Cesaria anaweza kwa kushikilia nyimbo na midundo ya ki Cape Verde, basi na Watanzania tunaweza kwa kushikilia miziki yenye midundo yetu. Basi hata ambapo wasanii sasa hivi wanapotaka kubobea kwenye midundo ikaribianayo na ya Marekani tukumbuke kuwa bado tunaweza kufanikiwa kwa kuendeleza midundo yetu.
P.W Botha-The great Crocodile
Mamba mkubwa , ndivyo alivyoitwa P.W. Botha. Huyu Mzee mpaka kufa kwake hajawahi kukiri wala kuomba msamaha kwa uhalifu wa serikali yake kwa watu weusi Afrika kusini. Pia alivyo ulizwa ingekuwaje kama watu weusi wangechukua nchi mwaka 1948 wakati chama chake kilichukua hatamu akasema nchi ingeharibika. Mpaka anafariki hakuamini katika kipaji cha uongozi wa mtu mweusi. Lakini je kwa mifano ya viongozi wetu Afrika na rekodi zao za uongozi unaweza kumlaumu huyu Mzee kwa kufikia kuamini watu weusi hawawezi uongozi? Amefariki akiwa na miaka 90. Natumaini kuwa karibu Afrika itaanza kupata viongozi ambao wataturudishia heshima yetu Waafrika na wote wenye rangi nyeusi. Kabla hawajatokea changamoto aliyoacha P.W. Botha ni kwamba: je, si ni kweli mpaka sasa viongozi wetu weusi ndio wanazidi kuchangia kuporomoka kwa nchi zetu za Afrika?Kama viongozi wanabisha Botha hakuwa anasema ukweli kuhusu uongozi mbovu wa viongozi wa kiafrika basi wafanyekazi na kutukwamua katika matatizo yetu Waafrika. Haya naona hata Mo Ibrahim anataka mpaka kuwalipa pensheni ilimfanyekazi.Fanyeni kazi basi, AlaaH!Habari zaidi hapa
© Blogger templates Romantico by Ourblogtemplates.com 2008
Back to TOP