Rasta Luihamu na baadhi ya wadau wamekuwa wananipiga maswali kibao hivi karibuni. Najaribu kujibu hapa baadhi ya maswali ambayo yanazidi kujirudia.
Kuhusu Waafrika kuogopa kurudi Afrika
Mimi sidhani kwamba ni vigumu kuelewa kwa nini Waafrika wengi wanavyowezakuogopa kurudi nyumbani. Pia siwezi kusema kuwa Waafrika wengi ni ukweli kuwa ni woga uwafanyao waishi mabara mengine. Mpaka sasa hivi elimu itawalayo Afrika ipo katika vitabu vya wageni kutoka nchi nyingine. Luninga watazamazo zimetawaliwa na maonyesho yaelezwayo na watu wengine na kwa mtazamo mkubwa usioupa sura nzuri Afrika. Kama uijuavyo tabia ya binadamu, ni rahisi kuelewa kwanini atajaribu kutembelea sehemu zisifiwazo ilikujionea mwenyewe. Kila muafriaka aliyeko nje ana stori yake. Wengine walishakata tamaa na Afrika. Kwa sababu hakuna wanachokiona ambacho kina wapa moyo kuwa wanamchango wowote wakutoa.Hii hasa ni kutokana nakuamini mfumo ambao upo ni vigumumu kuwapa nafasi ya kutoa mchango wao. Wapo ambao wamekwama nje ya bara. Maisha ni magumu, lakini bado wameweza kutunza hali ya utu wao kwa kujificha mbali na Afrika ambako ndugu na jamaa hawatashuhudia kasheshe ya maisha waishiyo. Wako ambao maisha yao na ujuzi wao hawawezi kuutimiza ndani ya Afrika kutokana na kukosekana mfumo uwianayo na elimu ambayo msingi wake wameupata tokea shule zetu za Afrika zinavyotuandaa. Wako wanaodhalilishwa kila siku. Wapo ambao wanaheshimika na kuthaminiwa. Kuhusu kujiandaa kabla ya kuvamia jambokwangu naona ni jambo ambalo kila mtu anatakiwa kufanya kwanza. Hivyo kwa wale walioishi muda mrefu nje ni lazima waliangalie hili swala. Hata kwa wale amabo wanaamini vijana wote wa mijini warudi vijijini, kama aaminivyo Mzee Luihamu,si busara tu ukaamua kwenda tu huko kijijini na jembe lako begani bila kujiandaa na hali halisi ya maisha ya kijijini. Maisha ni mchezo wa ajabu. Ukikua unastukia maamuzi yako kimaisha haya kuhusu wewe peke yako.Maamuzi yako hugusa ndugu na jamaa hadi jamii nzima. Maamuzi yasiyokuwa na mipangilio maalumu mara nyingi hayana nguvu ya majawabu ya kudumu.Kuna maamuzi yenye majina matamu lakini sio ukweli kuwa ni ya matatuzi ya kudumu.
Kuhusu nani atavaa viatu vya Martin Luther King Jr au Malcom X
Mimi binafsi sidhani kuwa kuna mtu atavaa tena kiatu cha Martin Luther King wala Malcom X. Kwa sababu sidhani kuwa kuna mtu yeyote amabaye anaweza kuwa kama mwingine. Nacho amini kila muda katika historia una matatuzi yake yalinganayo na muda huo. Hivyo yeyote mwenye busara atajifunza kutoka kwa akina Martin Luther Jr,Malcom X, Mwalimu Nyerere, babu, bibi, msaidizi wa kazi za nyumbani, na jamii kwa ujumla ilikufikia busara zimwezeshazo kutatua matatizo yamkabiliayo . Kumwezesha kutabiri mwelekeo wa mambo ilikuepuka au kuweza kukabili matatizo yatarajiwayo nk.
Kuhusu imani
Imani ni ya mtu binafsi na naamini kuwa mtu hawezi kulazimishwa kwamba aamini nini. Naulizwa sana mambo ya Urasta na Mzee Luihamu ameniambia kuwa tusiogope Urasta na Marasta , kwa kuwa ni wana wa Yosefu wa Israeli. Namuelewa kwanini anasema hivyo. Lakini chakujiuliza ni kwamba dini nyingi hizi watu wafuatazo sasa hivi zimekuwepo muda mfupi sana ukizingatia historia ya uwepo wa binadamu duniani. Je, kabla ya Yosefu Waafrika si walikuwepo? Je siinakumbukwa mikutano ya kujadili ni vitabu gani viingizwe kwenye biblia? Je ina maana Mwenyezi Mungu kabla ya dini na vitabu hivi vitakatifu viongozavyo imani karne hii alikuwa hana mapenzi na viumbe wake?Kwa mtazamo wangu ni kwamba imani ni kitu cha mtu pekee. Mtu akifa anaanza kivyake mwenyewe hivyo haya maswala ya imani za watu sitaki kuyaingilia. Kwa rasta Luihamu, mimi binafsi siogopi kuwa Rasta. Nilishawahi kuwa Rasta na kujikuta na pingana sana na baadhi ya misigi ya imani hiyo.Kwa kifupi, nilizaliwa katika familia ya kikristo.Nikawa Muislamu kwa muda, nikaokolewa na Mozesi Kulola, Nikarudi kwenye Ulutheri, na nikaendelea kujiuliza maswalali na naendelea kujifunza kuhusu imani.Hivi sasa naamini Mungu bila kufungamana na mfumo au institution yeyote.
Kuhusu vilevi
Mimi simshauri mtu yeyote atumie vilevi. Madhara yake hujulikana vizuri tu. Sidhani kuwa kuna kilevi hata kimoja ambacho hakina madhara. Pia, hili swala kila mtu anakichwa chake. Kwa ujumla sidhani kuna mtu anweza kupinga madhara ambayo yanaweza yakajitokeza na kumharibia mtu maisha. Lakini kumbuka hata chakula kina weza kukudhuru pia kama unakila bila mpango.Hivyo maswala haya ya vitu tuviwekavyo kinywani si yakuharakisha majibu kirahisirahisi. Sasa, mimi sivuti bangi wala kutumia madawa yoyote. Ndio nakunywa pombe za aina kadhaa. Simshauri mtu kuwa akiniona nakunywa basi naye aanze?Hapana hilo sifanyi.
Kuhusu muonekano wa kiafrika
Kwanini huwa najibu sana kuwa mimi ni muafrika lakini wakati mingine navaa suti? Mimi siamini Uafrika ni mavazi. Sidhani ukivaa Kichina basi unahalali yakuitwa Mchina. Napenda mavazi ya kiafrika. Huvaa mavazi ya kiafrika. Napenda kuvaa navyojisikia na siamini kuwa Uafrika wangu unapungua kwa kuvaa hivyo. Sidhani kuwa Mandela kwa kuvaa Kiindonesia amepunguza Uafrika kusini wake.Halafu sioni kwanini muonekano wa nywele zangu uwe ni tatizo . Siamini kuwa muonekano wa nywele ni kipimo cha ubinadamu wa mtu.Muonekano wa nywele zangu mimi kama Muafrika naona ni wa kawaida tu.Na naamini ni wa kiafrika sana ambao isingekuwa wamagharibi kuunganisha na tafsiri mbalimbali ungeweza kuwa wakawaida sana katika maofisi ya Afrika. Nashangaa sana kuona kuwa bado watu huchukua muda sana kufikiria swala hili. Je na wewe ufuge nywele kama zangu?Hilo ni juu yako. Je, wewe unavaa nguo za Kiafrika zipi? Jinsi au lubega?
Sidhani kuwa nimepungukiwa Uafrika kwa kuwa hapa sijavaa nguo zitafsiriwazo kama ni za Kiafrika. Ila sikushauri unywe pombe, unajua mwenyewe :pombe si chai
Read more...