TANZANIA katika KUSAHAU mchango wa MKOJO wa kikojozi AJIKOJOLEAYE kwa sababu kuna AJINYEAYE!
>> Thursday, October 30, 2008
Labda kweli kujinyea ni jambo kubwa kuliko kujikojolea, ila ukweli ni kwamba siku ya siku chumba chenye godoro likojolewalo kwa bidii, chanuka tu kama kilichonyewa.
Madogodogo yajirudiayo kila mara huzoeleka na hata kusahaulika jambo tufikirialo ni kubwa likitokea.
Mambo madogo madogo ni rahisi kuyapuuzia.
Tatizo ni ......
labda hata kipimo kitumikacho kupima makubwa chaweza kuwa ni cha kupimia madogo.
Ukizoea kuwa makubwa ndio yalalamikiwe na kufanyiwa kazi, madogo huachiwa ya shamiri.
Yafikiriwayo ni madogo hata kama mabaya, hayatiliwi maanani kwa kuwa kipimo kitumikacho hakituonyeshi matokeo ya mkusanyiko wa madogo.
Ukweli ni kwamba mengi makubwa mabaya tuyalalamikiayo chimbuko lake ni mkusanyiko wa madogo tuyadharauyo.
Hebu tujikumbushe.....
- Mkusanyiko wa viharage ndio siri ya ujazo wa bakuli la maharage.
- Umati wa punje za mchele, ndio siri ya wingi wa ubwabwa msibani hata kama ni wa jana na umechacha.
- NA KADHALIKA kadhaa wa kadhaaa..
Jambo dogo ni dogo kwa kubwa, lakinilabda jambo dogo ni kubwa kama hakuna kubwa.
Ukizoea kudharau dogo kujifunza kuzoea kudharau kubwa si tatizo.
Nina maana...
Kama waweza kuzoea kudokoa, waweza kuwa gwiji la kuiba.
Sasaaaaa.......
Inasikitisha kuwa karibu kila ninakopita Tanzania, naonajinsi Watanzania tunavyo dharau mchango wa madogo ambayo wengi wetu tunayaweza.
Chochote kidogo hakina heshima kutokana na mchango mdogo mdogo wa kuamini katika makubwa ulivyofanikiwa kukatisha watu tamaa katika kufanya madogo madogo tuyawezayo.
Siku hizi:
- Ukiiba kidogo utafungwa, ukiiba makubwa unaonekana mjanja na ubunge unapewa.
- Kutupa hata karatasi moja moja au chupa ya maji haionekani kwamba nimchango usababishao ukubwa wa jalala tuliitalo miji yetu.
- Tunaamini katika mchango mkubwa wa serikali mpaka kutufyekea majani mbele ya nyumba zetu .
- Ukiwa mfagizi unadharaulika na wathamio usafi wa ulipofagia.
Kusahau mchango uletwao na madogo ni kosa lifanywalo kwa waonao tu kuwa ni mpaka makubwa ya fanyike ndio mchango ufanikishao jambo.
Tatizo ni....
Tulio wengi hayo makubwa hatuna uwezo nayo.
Lakini....
Makubwa yasahaulishayo muonekano wa madogo yaweza kuwa SI msaada mkubwa kama tufikiriavyo.
Tukikumbuka kukumbushana kufanya madogo tuwezayo twaweza kutimiza makubwa.
Sikatai mchango wa makubwa, ila nachoamini ni kwamba tukijenga tena tabia ya kuthamini kufanya tuwezayo bila kusubiri hatutapiga makitaimu namna hii .
Cha kushangaza.....
- Moyo wa kuchanga bado upo ingawa siku hizi unaelekezwa kwenye harusi kuliko hata elimu.
- Ukiomba mchango wa kusomesha mtoto hupati lakini wa Kicheni pati na begi pati utapata.
- Ukiombwa mchango wakuzibua mifereji mtaani kwenu hutatoa wakati ukiombwa pombe utanunua.
- Watu huangaika sana kutunza heshima na status zao kwa kujaribu kufanya wasiyoweza.
Labda kwa sababu tunatoka katika tamaduni za kudharau wadogo basi hata kama wanajua kuliko wakubwa hawatasikilizwa.
Sasaaa....
Naamini siri ya kutomzoea kikojozi tumjuaye hata kama leo kajinyea ni kukumbushana kuwa jamaa ni kikojozi.
Naamini ndio maana mpaka leo KAMPUNI ya COCA COLA pamoja na kujua kuwa unajua COCA kola inautamu gani, hutumia pesa kibao kukuambia kuwa COCA COLA ni tamu.
TUSIKATE tamaa!
Kama umenisoma mpaka hapa labda nimekukumbusha ufanye uwezacho.
Siri ni katika vitendo.
Uwezo wa kutenda ni binafsi ingawa watu hupenda kunyosheana vidole kuwa jamaa hafanyi bila kujua uwezo wake.
Swali:
- Ukubwa au umuhimu wa jambo wa upima kwa kipimo gani?
- Siri ya akili ya kutafsiri ukubwa wa jambo si umuhimu wa uchungu wa madogo?
- Kama huogopi kufa unafikiri huna woga wa kuvunjika kiuno au nanihii?
Tukumbuke tu kuwa mchango wa madogo ni mkubwa!
Mungu ibariki Tanzania! Mungu ibariki Afrika!
TUTAFIKA!
BAADAYE BASI!
Ngojea tubadilishe mawazo kutoka katika matatizo ya Tanzania na kwenda Marekani kumsikiliza John McCain akumbushe ya Marekani
Au ngojea COOL KIDS waje na Black Mags
Samahani kwa matumizi ya maneno na sentensi ziwezazo kumtia mtu fulani kinyaa kama tafsiri za akili zake humkumbusha chooni , mafinyofinyo au sehemu zinukazo kwa sababu tunasubiri halmashauri ya mji ije kusafisha!:-(
8 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:
Aminia mzee wa mawazoni!
Kama nimerejea vile ulingoni.
Mada yako hewani nimeipenda. Nachoweza kusema ni kwamba WATZ tunashindwa kuyapima na kuyakabili makubwa kwa vile hata madogo tunayakabili na kuyatatua kiubabaishaji!
Nimepita tu leo!
@Mtanzania:Mkuu ulipotea sana!Asante kwa kunipitia hapa.Nakubaliana kabisa na mtazamo wako , tunababaisha sana katika madogo halafu tunashanga ubabaishaji ulivyoamia kenye makubwa.
Nilipata ujumbe!Niko mbali kidogo lakini nitapita hapo mtaani hivi karibuni. Nitakustua nikija!
MAWAZONI MAWAZONI MAWAZONI hakika ni falsafa kali kama za yule BOB Marley lakini siyo lile jani lake. kaka Simon natoa hoja kwamba unahitajika sana kuandika vitabu vya falsafa ingawa hofu yangu ni wabongo kupenda kulewa na starehe tu kusoma walimaliza wakiwa shule. MAWAZONI MAWAZONI jamani nina kitabu cgangu cha kumbukumbu naiba sana mambo ya MAWAZONI lakini usinipeleke mahakamani kama nimeiba simu au gunia la mkaa lakini nikiba BOT pale hakuna noma mkubwa u vipi
kazi njema
Markus: :-)Hakuna noma Mkuu!
mkuu,unaweza kunena wengi wasikuelewe.
kumbuka kipindi kile cha yesu,alinena nao kila siku lakini hawakumwelewa,lakini wakati ulipofika akawawafanulia.
mkuu unenapo nami nakuelewa.
@Rasta:Yesu alikuwa mtundu!Hata enzi zake kungekuwa na internet kunena kwake bado kungezingua.Tamu tamu nyingi anakataza:-(
ayaaah jamani tamu tamu zipi tena au yale mambo ya kunoga noga na kunogewa???
Hapa suala si nani ananena nini kwa nani ili kiwe nini. Suala ni kama linenwalo latunzwa na kama ndivyo basi hakuna shaka ukifika wakati muafaka litazinduliwa tuu. Haya ndiyo tuhitajiyo kusoma kuweza kuikomboa jamii toka katika utumwa wa kialiki, lakini jamii si "tumwa" tu, bali "zembe, vivu, dhaifu na yenye mtazamo na fikra fupi". Isiyotaka kuwekeza na kujishughulisha katika chochote kisicholeta matunda ndani ya wiki ama wakirefusha ni mwezi. Jamii yetu yapanga "mshahara to mshahara" na iliyo nje haijitahidi kuvuka kale kamstari katenganishacho "elimu vs Ustaarabu". Wengi wameelimika (kwa mujibu wao) lakini hawajastaarabika. Wamepumbazwa na akili za ki-magharibi na kuanza kutukana na kukandia kwetu. Lakini heshima yako Simon wala usiitegemee toka kwa jamii yetu sasa hivi maana wajua "prophet will never be honoured in him own yard" na hilo watambua. Lucky Dube alisema kwenye wimbo wake TILL YOU LOSE IT ALL kuwa "he is a hero now that he's dead..... when he was alive you didn't know his name, when he was alive he didin't gain respect" Well sikuombei ila najua kuwa tutakufa siku moja na kama hutoweka haya kwenye kumbukumbu mwanana basi utaondoka nayo na "mission" yako kuwepo duniani kwa fikra na MAWAZO haya itakuwa haijakamilika. Tunza Kumbukumbu kwenye kitabu ama namna yoyote kwani mwanangu ajaye LAZIMA atambue haya
Blessings
Post a Comment