MTU bila WATU, akiamua JAMII iamini NYAMA ya PAKA ni TAMU kuliko ya MBWA !
>> Wednesday, November 07, 2007
Mtu mmoja na mawazo yake, ana nguvu katika jamii.
Mtu mmoja pale tu awezapo kufanya idadi ya watu wakutosha wafuate mawazo yake, anaweza akashangaza umati kwa jinsi awezavyo kusababisha umati upendao Bongo Fleva ,upende SINDIMBA.
Swali:
- Unakumbuka Ghandi hapo mitaa ya india, alishawahi kusababisha umati wa Wahindi uache kuvaa nguo alizohisi zinafaidisha Waingereza wakati yeye mwenyewe kavaa nepi?(ilikuwa haiitwi nepi lakini:-))
- Unaweza kufikiria nini ukienda kwenye mkutano wa kiongozi wako sasa hivi ukamkuta anahutubia huku kavaa nepi?
Idadi ya watu wanaotakiwa kukufuata ili wazo lako lichukuliwe maanani , inategemea na wewe mwenyewe na aina ya wafuasi wako.
- Yesu na baadhi ya Masupastaa wa baadhi ya dini tuzishabikiazo, walianza na wafuasi wachache.
- Akina Fidel Castro , Museveni na .... waliingia msituni na wafuasi wachache.
Yesu , alianza na walalahoi ambao silaha yao ilikuwa imani yao kwake.
Fidel Castro na Museveni , inasemekana ilipobidi walitumia mabavu katika kuhakikisha kuwa wafuasi wao wanabakia wafuasi. Nafikiri unakumbuka stori za jinsi isemekavyo CHE GUEVARA alivyokuwa rahisi kukupiga risasi mtu, akihisi kuwa huaminiki katika jeshi la FIDEL CASTRO.
Swali:
- Nyama ya mbwa haina sumu , unahisi kwanini huili au unajivunga kuionja?
- Ushastukia watu wanakula nyoka mwenye sumu kwa kujua jinsi ya kuondoa sumu wakati wanaacha nyama ya ng'ombe kwa sababu za maisha ya baada ya kufa?
Sasaaa.....
Asili ya mitazamo mingi , ilianzia kwa mtu mmoja.
Unaweza kufuatilia mpaka kwa mtu mmoja aliye tamka kwa mara ya kwanza kuwa anahisi dunia ni mduara na sio kama meza.
Mtu atoaye wazo na wafuasi wake katika hilo, wanaweza wakawa na nguvu au wasiwe na nguvu kutokana na wachukuliwavyo katika jamii.
Mtu aaminiwaye katika jamii , ni rahisi ushauri wake kuwa; watu wale nyama za mbwa koko mtaani ili kupunguza mbwa wazururao , ukachukuliwa uzito kuliko mdau jamii impuuzayo akisema kuwa sababu kubwa ya siasa mbovu Africa ni pamoja na uwepo wa tabaka litawalao ambalo limejaa watu waheshimiwao katika jamii lakini hawana dira ya wapi waelekeze nchi zao, kwa hiyo mpaka tabaka hili litakapo pata kuwa na wengi wanye uchungu wa kweli , ndio itakuwa mwisho wa kupiga makitaimu kimaendeleo.
DUH!
Mtu bila watu , mchango wa mtu unakuwa mdogo sana katika jamii.
Hata katika kuijanza jamii, mtu huhitaji angalau mtu mwingine wamimbishane ili azaliwe mwingine kuongezea kaidadi ka watu duniani.
Lakini......
Tusisahau mchango wa mtu mmoja, kwani ndio kiini halisi cha swala.
Naamini inawezekana ikawa ni wewe mwenye wazo ambalo ndio utatuzi wa matatizo fulani yatuzungukayo.
Naamini hakuna mtu au wazo moja litakalo kuwa jawabu ya yote.
Hata Yesu na watu wengine fulani, bado mpaka leo mawazo yao hayakukubalika na wote.
Kumbuka kuwa hawa ni ambao wanahusianishwa na Mungu katika hoja zao na bado watu wanawastukia maeneo maeneo.
Hivyo...
..... Uwezo wa mtu wakawaida na hoja zake binafsi kukubalika unatakiwa kulenga maeneo yaguasayo udhaifu uliopo katika jamiii.
Swali:
- Hivi unafikiri ni kwanini masikini wengi hawacharuki kirahisi katika nchi masikini wakati wanashuhudia wachache wakifaidi matunda ya jasho au udhaifu wao?
Lakini...
... pamoja na kwamba wazo lako nitalikataa, bado ni wazo zuri likiwa lina jenga jamii na kupunguza machungu yaigusayo jamii. Wazo lako linaweza likaoneka na la ajabu kutokana tu na kuwalenga watu walioko na kujengwa kifikra na mifumo ambayo inasababisha mawazo ya ajabu ya wengine yashamiri na kuifanya dunia kuwa ya ajabu kama uionavyo hivi leo.
Mfumo ambao unaruhusu baadhi ya mawazo yasikike na kufuatwa zaidi kuliko mengine ndio unao sababisha mtu kama George Bush , Marekani na hata Kikwete Tanzania, waweze kuwa ni watu tuwasikilizao na watuongozao kuliko wale ambao kwa mtazamo flani wangeweza kuwa ndio viongozi ambao wangekuwa wanatuongoza sasa hivi kama mfumo huu haungekuwepo.
Swali:
- Kama mfumo huu uendeshao dunia leo hii ni mbaya sana, unahisi ni kwanini umeshamiri namna hii?
- Kama CCM ni mbaya kwa Tanzania, unafikiri ni kwanini bado wajanja hawajitengi nacho?
Lakini....
.......naamini kuwa mawazo mengi watu tufikiriayo kuwa ni mapya, ni mawazo ambayo mtu mwingine alishawahi kuyawaza na kutoyafanyia kazi.Tatizo ni kwamba mara nyingine wazo lako wewe ni zuri lakini kunamtu mwingine ndio yuko katika nafasi ya kuweza kulifanyia kazi.
Tatizo ni kwamba , ni vigumu kwetu wengi kukubali utoe wao kwa ajili ya wengine kufaidika kama tunahisi sisi hatutafaidika na wazo hilo tuchangialo. Ni vigumu kushauri watu wale mbwa mtaani kwao kama mimi huku minofu haitanifikia.
Cha ajabu ...
...karibu sisi wote naamini tunachangia sana kibinafsi kukwamisha jamii kwa kutochangia kwetu angalau kimawazo katika matatuzi ya magumu yaigusayo jamii.Naamini hata mawazo yetu tukiyaweka wazi, kuna mwingine anaweza kufaidikanayo hapo baadaye kwa kuyafanyia kazi au hata kuyakarabati kama akina Nyerere walivyofanya.
Swali:
- Unahisi unawafuasi?
- Watoto wako au hata ndugu, wale wadogo uwanunuliao peremende bado hawakufuati na mawazo yako?
Naacha!
Mawazo mengine hayafai kuandika haraka haraka, nisije nikajipoteza bure na wafuasi wangu!
DUH!
Tulia na Mtu mmoja aitwaye Savion Glover atuonyeshe mchango wake katika sanaa ya TAP DANCE
Nahisi ni muachie tu na SAMMY DAVIES JR ,andeleze kutuonyesha TAP DANCE
3 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:
Kaka kuna kitu nafikiria. Hivi kwa nini tunavaa?
Jibu rahisi, kujisetiri. Lakini kwa nini tujisetiri?
Je, uvaaji wa chupi unafanana na uvaaji wa nguo nyinginezo?
@Bwaya: DUH!
Kuhusu uheshimiwa, nadhani ukiwafahamu watu vizuri hutabaki na unayemheshimu. Ukitaka kuwaheshimu watu, usiwajue. Hiyo ni mipaka ya tafsiri yangu.
Halafu suala la mawazo: Kuwa na mawazo na kutokuyafanyia kazi, ni kutokuwajibika. Tusisubiri wafuasi, tuwaze. Kwanza wazo mpaka liwe wazo lazima lipingwe. Tutakuwa tumefanikiwa ikiwa tutawaza pasipo kujali wengine wanasemaje na/au watatufuata.
Samahani kwa michango kadhaa kwa maramoja.
Tuko pamoja.
Post a Comment