Mtakatifu SIMON KITURURU - MAWAZONI

FALSAFA na WAZO ndani ya neno - DUH!

Salamu Kutoka Tallin!

>> Wednesday, February 28, 2007


Kuna washikaji wamestukia kuwa nimepotea na hawanipati katika baadhi ya namba za simu.
Tatizo ni hii mitaa ya Tallin, Estonia, isababishayo hilo.Tutakuwa pamoja hivi karibuni.

Kama mitaa hii ya huku Tallin huifahamu, naweza kusema huu ni miongoni mwa miji ambayo inabadilika haraka sana ,kutoka katika hali ya umashariki ya Ulaya kuwa magharibi ya Ulaya. Na uhakika baada ya miaka si mingi, bei za vitu hapa zitakuwa sawa tu na miji mingine ya Ulaya magharibi.

Ila hapa bado hakuna watu weusi wengi. Ni kawaida tu mara nyingine kupitisha siku bila kumuona mtu mweusi. Ila kuna kitu kingine kinifanyacho ni waheshimu hawa watu. Hawa wa Estonia na Wafini , wanahistoria yakutawaliwa kwa miaka mamia na wenzao.Nawapa heshima kwa kutosahau wao ni akina nani. Mpaka leo Waestonia wanaongea kiestonia. Kwa Wafini mpaka leo wanaongea Kifini ingawa Waswedi walishawahi kuwabadilisha wote mpaka majina yao .
Sasa hapa Tallin , kinachotokea ni kwamba kuna mvutano kati ya Waestonia wenye asili ya Kirusi na Waestonia kamili. Ukiniuliza nitakwambia Waestonia halisi hawawapendi Waestonia wenye asili ya Urusi. Sasa inapotokea mtu kama mimi ambaye sina uhusiano na wote , huwa unaweza ukajikuta unavutwa pandezote mbili. Warusi wanataka uwaonepoa na Waestonia kamili wanataka uone kuwa wao ndio poa. Halafu hapo wakati bado uko katikati yao akijitokeza Mfini, mara nyingi anapenda uone yeye ni bora kuliko Warusi na Waestonia.


Lakini kabla sijaendelea nimemkumbuka Peter Tosh asemavyo...

Hii mivutano ya binadamu huwa inanifikirisha sana !
Lakini kwa bahati nzuri hapa kuna Hoteli ya Kiafrika. Ugali utapatikana karibuni kwa jina la Fufu.
Ngojea nikuache na baadhi ya picha kutoka Tallin...
Photobucket - Video and Image Hosting
Hapa nafikiri unaweza kuona huu mji uko katika ukarabati.

Photobucket - Video and Image Hosting
Usistuke, wanahudumia watu weusi vizuri tu.

Photobucket - Video and Image Hosting
Samahani, hapa hawana bado makande!

Photobucket - Video and Image Hosting

Kwa wazoefu, huyu ni Mrashia au Muestoni?


Photobucket - Video and Image Hosting

Huyu jamaa anapendwa hapa , kwasababu wasichana wanamfananisha na David Beckham.

Photobucket - Video and Image Hosting

Photobucket - Video and Image Hosting

Sasa tuendeleze basi libeneke!


Watu mliokuwa FEST Afrika, kwa mfano KIBUNANGO, tuwekeeni picha la FeST.Unajuatena nimelimisi.
Haya tuendeleze, lakini du...Ali Farka Toure, unamkumbuka?

Read more...

Ashki Ya Michango!Lakini Ushachangia Nanihii?

Swali:
Hivi Tanzania tunaweza kurudia michango tuihitajio au waihitajio kikweli?Sisi binadamu tunamapungufu yetu! Ni vigumu kila siku kuweza kufanya yote tutakayokufanya kwa nguvu zetu wenyewe. Tunahitaji misaada mara kwa mara. Tuna matatizo mengi.Na kwa bahati mbaya matatizo haya hayawezi kuisha.

Lakini.....
Naamini mara nyingine sisi wenyewe hutengeneza baadhi ya matatizo. Kwa bahati mbaya au nzuri, kitu kingine kitufanyacho sisi kuwa binadamu ni jinsi tunavyoweza kujijengea mazoea ya vitabia vyetu. Moja ya tabia ambayo ni rahisi kuzoeleka ni ile ya michango.

SISEMI KUWA MICHANGO NI KITU KIBAYA!

NAKUBALI KUNAMICHANGO NI MUHIMU KWETU KUCHANGIA.

Lakini.......

Je, hii michango tuipayo kipaumbele na yenyewe inatupakipaumbele ?

Je, hii michango inasaidia kuendeleza au inabomoa?

Je, hii michango inasaidia tuchangiapo?

Katika baadhi ya vitu binadamu afanyavyo , vimejijenga ndani ya binadamu kwa muda mrefu. Kama unamkumbuka Maslow na kile kielelezo chake cha ngazi za matakwa ya jamii na binadamu.......

......utaona kuwa, tunanasa katika ngazi nyingi tu.


Ukiniuliza kwanini tunachanga sana hata pale ambapo hatuna ujanja tunajihisi ni lazima tutoe michango, kwa kutumia Jicho la mitazamo ya Maslow,
.....nitasema kwasababu
:

 • Kupata amani(ngazi ya pili, kwenye jeduali):tunafarijika kuwa iposiku tutasaidiwa pia na watu tuwachangiao.Iwe ni familia, wafanyakazi wenzetu, nk
 • Kukubalika/kupendwa(ngazi ya tatu):kwa kawaida usipokuwa mchangiaji hukawii kuitwa bahiri na sio mtu safi
 • Staha(ngazi ya nne hapo juu kwenye jeduali): kuheshimika, inatusaidia kuwa na uhakika, na tunajisikia hali ya kufanikiwa.
 • Tunajisikia tunafanikisha maswala, tunajisikia kunakitu ambacho tunafanya .
Kwa hiyo utakuta kuwa katika kila ngazi inaweza ikawa ni mimi au wewe umenasa.Katika kila ngazi kuna kamsukumo kamsutako mtu asipo changa.

Tukiachana na Maslow na mitazamo yake , mimi naweza kusema kuwa hii hali ya michango haiko katika binadamu tu bali hata katika wanyama karibu wote wa kinyaninyani.

Kama wewe ni mfuatiliaji wa tabia za wanyama kama Chimpanzee, na hata bonobo utakuta wanakamtindokao kakushughulikia maswala ya michango. Chimps katika mengi wafanyayo , hukumbuka nani alimfadhili mwingine.Chimps aliyekuwa anamkuna mwenzie na kumtoa vidudu , huwa ni rahisi kwake kupewa chakula na aliyemkuna iwapo atakosa chakula. Bonobo wao imefikia mpaka mwanamke ndio ananguvu katika kundi kutokana na kutengeneza uhusiano kwa kupeana michango. Ndio nakubali hawatoi pesa, lakini unafikiri michango ya pesa inanunulia nini?

Ngoja niwakumbushe tofauti za hawa wanyama wawili niwazungumziao.

Huyu ndio Chimp


Huyu ndio Bonobo.

Yeye huwa mwembamba kuliko Chimp wa juu. Halafu anamidomo ya denda.

Kwanini nimewakukumbusha hawa wanyama?

Duh!
Tuache tu!

Lakini usijisikie mpweke! Si wewe wala mimi pekee katika kamchezo haka ka-maisha tunajikuta tumebanwa kona fulani, hata manyani pia.

SASA lakini.....

Kumbuka michango mingine ukweli wake ni kwamba haukusaidii wala kumsaidia yeyote yule!
Halafu kwa kuzidi kuiendekeza unajiumiza tu!

Naamini msemakweli na afanyaye kutoka moyoni ,hustukiwa tu na jamii!Sasa kama kale kamchango ka-filigisi za sikukuu ya...... hukawezi , achananako.
Ukikaendekeza kanakuumiza tu !

Halafu kumbuka haka kamchezo ka-maisha kana mambo yake mengine.Ukijiumiza kwa kufanya mambo usiyoyaweza ipo siku utaonekana mbaya na umeumia zaidi. Halafu ukionekana mbaya au umeumia zaidi , watu wanakamchezo kakukukwepa. Wataobaki ni wale tu rafiki zako wa kweli ambao,wangekuelewa hata usingechangia.

Tuchange tu tuwezapo, lakini tuangalie tusiibe tu jamani kwa kujaribu kutunza sura!

Hivi michango na minyoo vinauhusiano?

Halafu kwanini ghafla tu, michango imekuwa ndio lifestyle Tanzania?

Mimi sielewi kama nisivyoelewa hapa chini ,Franco akiwa na TP Ok anasemanini.....


Read more...

Ukiniuliza kuhusu Tanzania vitani!

>> Tuesday, February 27, 2007

Ukimsoma H.G Wells katika kitabu chake cha The war of the worlds, unaweza kufikiria kuwa ni mpaka vibwengo kutoka sayari nyingine waingiapo duniani ndio vita kabambe inaweza kutokea. Ukifuatilia jinsi vita mbalimbali, sehemu mbalimbali duniani vilivyoweza kutokea hata zile sehemu watu walipoonekana kuwa wanaishi kwa amani,Tanzania chini ya uongozi mzuri tunaweza kuanza kupigana vita wenyewe kwa wenyewe. Ukifuatilia Bosnia miaka ya tisini, Ujerumani miaka ya thelathini, bila kuwasahau Watusi na Wahutu , hapo jirani, lolote laweza kutokea Tanzania.

Kinachohitajika ilikufanikisha vita Tanzania ni uongozi bora.
Au ulitaka niseme uongozi mbaya?
..lakini tuendelee na sababu zinazoweza kuondoa amani....
Kusahau ladha ya utamu wa amani .Uchumi kuendelea kudidimia wakati viongozi kuendelea kunawili.
Duh!
Dini nazo zikiendelea kutuaminisha maswala na kutusahaulisha kutumia akili.Akili nazo zikiendelea kukosa chakula kiiakikishiayo makali yasaidiayo kutatua matatizo yatukabiliayo, na hata pia kushindwa kututuliza katika dakika ambazo maamuzi lazima yatolewe.

Tanzania pamoja na yote ni jamii iliyogawanyika ingawa mara nyingi tunapenda kubisha. Ni rahisi sana kugundua kuwa:

 • Ukabila tunao
 • Udini tunao
 • Umasikini tunao
 • Uongozi bora ambao unaendelea kutufanya masikini tunao
 • Mfumo wa kisiasa ambao haujatengemaa tunao
 • Ujinga tunao
 • na nakadhalika tunayo.
Vita nyingi duniani zilisababishwa na zinasababishwa na maswala niliyoyataja hapo juu.

Lakini vilevile naamini tunamatumaini. Hakuna haja ya kukata tamaa.

AU UNASEMAJE?

Read more...

Internet


Je, internet imeshakuwa ugonjwa kwako?
Jipime hapa

Read more...

Hivi Ushawahi kufanya matusi?

>> Sunday, February 25, 2007


Kuhusu swala hili la kuhonga, mimi nakiri nishaonga sana.Si unajua yale maswala yakutaka kuwa mstari wa mbele!Au yale yakutaka mambo yawe rahisi zaidi kidogo!
Nilimsoma Ndesanjoaliposema tuanzie nyumbani katika kusawazisha mambo. Mimi naacha hii mambo.Mimi nimeaanza muda mrefu lakini hii kitu napenda nitangaze ,ni kona yingine naanza. Lakini kabla ya yote, nakiri katika hii rushwa na mimi nilishiriki kuisaidia kinamna. Wewe Je?
Tuache haya matusi basi!

AU?
Au ulifikiri matusi ni nini?

Tuendeleze wikiendi. Namuacha Barrington Levy akikupa Murderer

Read more...

UKOKO!

>> Friday, February 23, 2007


Ushawahi kuwa shabiki wa ukoko? Utandu je? Bwana eeh!Kuna wakati nilishajenga tabia ya asubuhi kukwepa mikate na vitu vingine na kuhakikisha napata kiporo cha wali na maharage ya nazi ya jana. Hasa yale yasio na rojo sana. Basi hapo nikipata na chai basi siku imeanza.

Lakini ngojea turudi kwenye Pizza. Nisisahau na hambaga. Unajua hivi vyote ni vyakula vya walalahoi vilivyowafanya baadhi ya watu kuwa mamilionea.Sasa bongo tuna vyakula vingapi vya walalahoi hatujavifanyia kazi?.Au tunasubiri tuone mpaka Malkia akivitafuna, kama Pizza ilivyopata umaarufu ndio tuvishabikie?
Usitishike najiuliza tu!
Tuendeleze libeneke.

Namuachia stereoman..

Read more...

Kitchen Party na....

Hivi hii party imepataje umaarufu namna hii?
Siipingi!Usinielewe vibaya.

Kabla sijasema sana:
Swali:
Hivi wanawake wa kibongo wanaridhishwa kimapenzi?

Duh!
Samahani akina dada , badala ya kimapenzi kwenye swali hapo juu, nilikuwa namaanisha ngono.
Wakati ukifikiria msikilize Sade akisema smooth operator....
Naamini binadamu anaruhusiwa kujitafutia sababu za kufurahi. Na nakiri sijui ni nini kinatokea huko.Lakini nasikia kunamafunzo kibao akinadada hupata. Au ndio aina mpya ya kumfunza Mwali kama ilivyokuwa katika unyago?

Huwa sipendi kuandika mambo katika kuegemea katika jambo nisilolijua sana. Ila nachojua kuwa jamii yetu inahitaji sana mafundisho yawezayo kuokoa mahusiano ya watu. Iwe katika ndoa au hata katika urafiki wa kimapenzi.Tatizo kubwa linatokana na misingi iliyobobea hata kwenye mila zetu. Mila zetu mara nyingi zimewafunza wanawake kuridhisha wanaume na pia kuwafunza kukaa kimya pale wasipo ridhishwa.Kuna makabila machache Tanzania ambayo yalikuwa na historia ya kuwafunza wanaume kuwaridhisha wanawake katika ngono.Ni mara chache utasikia staili kama katerero nk. ambazo hubobea kumridhisha mwanamke zikizungumziwa katika mila nyingi.

Kuna hoja zinajengeka kuwa moja ya sababu kubwa ya mwanamume na mwanamke kuwa na nguvu ya kuonja nje ni hii hali yakutoridhika na kitowewo cha nyumbani.Inasemekana kuwa ingawa mahindi ya kuchoma ya mtaani yananukia zaidi na ni matamu watu wengi wangeweza kuvumilia mpaka wafikapo nyumbani kama wanauhakika mahindi ya kuchoma yale ya nyumbani yapo na yanaridhisha kubwa kuliko.

Sasa eeh! Turidhishane basi!

Ila tatizo mbinu za kuridhishana mara nyingi hakuna pakujifunzia. Sasa kama huko kitchen party kunamasomo haya basi akina dada mnawini, ngawa na mashaka kuwa somo la siku moja na la mazingira niyasikiayo ya Kitchen party latosha

SASA eeh!

Nafikiri tunaongelea sana matatizo mengi yatutatizayo Watanzania. Lakini mara nyingi tunaruka hili la mahusiano.
Kumbuka mahusiano mazuri huzaa wazazi wazuri.Husaidia kupunguza magonjwa.Husaidia kupunguza watoto wa mitaani.Husaidia ukuaji wa watoto walio lelewa vizuri. Huzaa watoto wafanyao vizuri katika shughuli zao. Hupunguza matatizo chungumzima.

Sasa kwanini hatufundishani hizi mbinu za kuridhishana?

Mimi nafikiri tunahitaji kukuza uwazi wa maswala haya. Tumeua mila za unyago na jando. Sisemi tuzirudie. Nachotaka kusema nikwamba si yote yaliyokuwemo katika mila hizo yalikuwa yanaumiza jamii. Tuchukue mazuri tuunganishe na yanayohusiana na maisha tuishio sasa hivi. Tuyafundishe yawezayo kusaidia hata ikibidi somo hili liwe kwenye silabasi za shule.

Duh!
Katika kuzungumzia kuridhishana, nimekumbuka swala la matako.
Rafiki yangu mmoja Mzungu kaniambia anapenda matako makubwa kuyaangalia tu. Kasema kinachomshinda ni pale ajaribupo chuma mboga ambayo ndio madoido apendayo akiwa katika shughuli, hawa sangara wanasababisha ajisikie hafiki ufukweni. Sasa mimi nikamsamehe kwa kuwa alikuwa mkweli.Kwa hiyo msiwalaumu sana wapendao dagaa, huwezi kujua siri ni nini.

Duh!
Na hili jina Kitchen Party, mie lanizingua. Au ndoa inauhusiano zaidi na Kitchen kuliko mambo mengine? Kwanini haikuitwa sherehe ya jikoni lakini?

Sasa kwa wale ambao wanaume wao ndio wazima zaidi katika maswala ya Kitchen, wawe na Chumbani Party nini?

Najiuliza tu!
Lakini unajuatena leo ijumaa. Nakuacha na Lagbaja


Wikiendi njema!

Read more...

Ulisherehekea sikukuu ya kuzaliwa Mugabe?

>> Thursday, February 22, 2007


Mugabe alifikisha miaka 83 jana.Halafu inasemekana bado anampango wa kuendelea katika uongozi baada ya mwaka 2008. Hivi ni kweli anaamini hakuna mwingine awezaye kuongoza nchi?

Huyu kiongozi mpiganaji ukifuatilia maswala yake utakuja gundua kwa muda mrefu ilikuwa vigumu kumbana na kumlaumu. Ukichanganya siasa za kikabila za Washona kama yeye na Wandebele, na pia siasa za Afrika Kusini kwa ujumla, utakuta kuwa mambo hayakuwa rahisi sana kisiasa. Ukija kuwaingiza na wazungu wa Zimbabwe na Waingereza basi unaweza kuona jinsi gani hali ilivyokuwa ngumu kutatua baadhi ya mambo.Lakini sasa hivi naona alishapitiza na sidhani ni msaada tena kwa watu wake.

Mimi nafikiri wakati umefika wa hawa viongozi kuwa na mikakati ya kuondokea ofisini tokea mwanzo waingiapo katika ofisi. Naamini wengi wakishaingia wanakuwa hawajui jinsi ya kutoka. Wengine wanakuwa washaiba wanajua wakitoka wanaweza kufungwa. Wengine ndio hivyo tena , wanastukia kugongana na akina Tony Blair ndio inakuwa imetoka tena, hivyo wanang'ang'ania. Hii ni sawa tu na Wamarekani walivyoingia Iraq bila kuwa na mikakati ya jinsi ya kutoka.

Lakini wajifunze kutoka kwa akina Boris Yeltsin wa russia. Yeye alihakikisha anamweka kijana wake Vladimir Vladimirovich Putin ambaye hatamgusa akimaliza ulaji. Wajifunze kutoka katika uongozi wa CCM. Wao huhakikisha anayefuata hamgusi aliyepita hata kama madhambi yake yanajulikana.

Duh! Lakini inasikitisha.Huyu ni miongoni mwa viongozi ambao kama kwenda shule tu nakuipenda shule inasaidia, yeye katika viongozi wa Afrika si mvivu.Inasemekana hivi sasa bado kuna degree anaisomea.Hizi hapa chini ndio alizonazo kwakuziendea shule na kwa masafa, ukiachana na alizopewa tu na baadhi ya vyuo...
* BA (Educ) Fort Hare;
* BSc(Econ) Fort Hare;
* BSc (Econ) University of London, by distance learning;
* BEd University of London, by distance learning;
* LLB University of London, by distance learning;
* BAdm University of South Africa, by distance learning;
* LL.M University of London, by distance learning; and
* MSc (Econ) University of London, by distance learning.
Kinasikitisha pia kuwa mke wake wakwanza Sally Hayfron, aliyekuwa Mghana, anasahaulika siku hizi kama mwanamama aliyekuwa mpigania haki hata kufungwa jela kwa hilo.

Read more...

Hivi Huyu Demu Mapepe?

>> Wednesday, February 21, 2007

Nilipata bahati ya kusoma katika sekondari ya Mazengo , Dodoma, kabla haijafutwa.Ilikuwa shule ya wavulana pekee. Wanaume tulikuwa wengi kwa mamia na mamia, halafu tukobodingi. Hapo basi kasheshe inayotokea ni hile ya kukosa wasichana.Halafu kumbuka asilimia kubwa yetu ndio tuko katika ile miaka ambayo sekunde chache sana zinapita bila kufikiria wanawake.Unajua tena baolojia ya miili. Wasichana ambao ilikuwa tunawaonaona kabla kupata ruhusa kwenda mjini ni watumishi wa walimu na pia wasichana kutoka vijiji vya karibu.Lakini ilikuwa ukishikwa na wanakijiji umeenda kudoea ,jasho litakutoka. Halafu tena wale wafanyakazi wa walimu nao ilikuwa ni vigumu kuwafuata nyumbani kwa walimu.Ingawa baadhi ya watu walifanikiwa kupona kinamna hii. Shuleni kwetu tulikuwa tunategemea zaidi wasichana watokao sekondari ya wasichana tupu wa Msalato. Hawa ndio tulikuwa tunawaalika tukiwa na sherehe na yale mambo ya disco la mchana. Basi siku wanayokuja ilikuwa inakuwa kasheshe. Utakuta siku hiyo watu wanaazimana nguo, utasikia watu wananukia perfume na hata wengine ndio siku za kupiga mswaki. Siku nzima wajao hawa wasichana utakuta mabwenini hakutulii. Cha ajabu ilikuwa baada ya hawa wasichana kuja halafu disco kuanza inakuwa taabu tena kutafuta patina wa kucheza naye au hata wa kuongea naye. Kwa sababu kunakuwa na watu wengi waogopao kutolewa nje wakiomba kucheza au kuongea na msichana. Na sababu kubwa ilikuwa, ukitolewa nje na msichana utataniwa sana mabwenini. Hivyo basi siku hizi zilikuwa na mambo yake. Nataka-sitaki nyingi ile mbaya!

Basi bwana, bahati ikatuangukia shuleni kwetu.Wakaanzisha kuleta wasichana wachache wa O-level kuja kusoma kama wanafunzi wa mchana.Wakaletwa wasichana 35 hapo.Walipofika tu, tukawapa jina vikuyu. Wengi wa hawa wasichana , walikuwa wametafsiriwa mabwenini kuwa si wazuri.Hivyo ilikuwa ni kitendo cha aibu ukionekana unafukuzia yeyote katika hawa. Ila sasa kumbuka tuko mamia na mamia ya wavulana wasiopata kusikia sauti ya mwanamke mara kwa mara, halafu unaleta wasichana 35 katikati yao!Nahisi unajua litakalotokea! Naamini hawa ni baadhi ya wasichana waliofukuziwa na kupewa kauli za kila aina kuliko wengi duniani. Wakulilia alilia, wakujifanya mcheshi alifanya hivyo, bila kuwasahau wakutishia, ili mradi tu kila mtu alikuwa analenga kujipatia kidude. Kutokana na redio za mianzi hawa wasichana hata aliyekuwa mgumu kiasi gani, alijikuta tu siku ananasa kwa watu fulani.Kwa maana mbinu zote za vita zilitumika.

Nimeikumbuka hii hali leo baada ya kugongana na jamaa anamlilia kabisa mwanadada ndani ya treni. Lakini ukweli ni kwamba anaigiza kwa sababu nishamuona akifanya hivyo kwa mwanadada mwingine siku chache zilizopita. Ila nachomvulia kofia ni sehemu anazofanyia kitendo. Kwenye stendi ya Treni, ndani ya basi, sehemu ambazo kuna watu wengi. Lakini labda kagundua anahurumiwa zaidi kutokana na wasichana kuonanoma watu tunavyojifanya hatustukii kinachoendelea lakini tunapiga kijicho kishkaji na kucheka mbele. Au labda akina dada ndio wanaamini ni mkweli kwasababu analilia hadharani!Sijui!

Duh !Lakini , kuna watu wanajua kuomba!Nafikiri wangefanya hivi katika kuomba kazi , basi kazi yoyote ile duniani wangepata.Halafu mwanadada akikubalia jamaa kadhaa walioonyesha juhudi anaitwa mapepe.Duh!


Ngoja nikuache na Kingwendu family wakuache na huu wimbo Mapepe....


Tusisahau kuna UKIMWI lakini!

Baadaye!

Read more...

Taifa la kesho ! Mielekeo miwili tofauti kimziki.


Tuanze.....Halafu.....Labda future ya miziki ya mtu mweusi haijatetereka.
Labda!

Lakini unahisi Taifa la kesho Afrika linakwenda wapi kiutamaduni, afya, nk.

Read more...

Kloning Sokoine!

>> Tuesday, February 20, 2007

Sijasikia habari za kloning ziigusavyo Tanzania.
Hivi kama kuna-Watanzania ambao tungeweza kutengeneza kopi zao. Yupi ungependa kloni wake arudishwe?

Kuna wadau kibao waliniambia hiki kitu kingekuwa kimekubalika na jamii ,basi wangewarudisha kloni wa ndugu zao wengi tu. Katika wanasiasa wa Tanzania, kuna watu kibao walimtaja Sokoine.

Leo imebidi nijiulize kuwa hivi ni kitu gani cha zaidi kinachomfanya Sokoine aonekane alikuwa tofauti?

Katika majibu machache niliyopata nikashangaa kuwa kwanini yalionekana ni tofauti(special).

Sifa za Sokoine kuu zilizomfanya awe maarufu ni:

 • Mfanyakazi kwa bidii.
 • Hapendi rushwa na anaipiga vita rushwa.
 • Kiongozi asiye na makuu.
 • Anajivunia mila yake.

Labda unaweza ukaongezea sifa zake. Lakini hizo nilizozitaja ndio zilijulikanazo sana. Sasa huhisi hizi ni sifa ambazo kila kiongozi wa Tanzania anatakiwa awenazo?

Sasa jiulize kwanini kila mtu akamstukia Sokoine kuwa bomba?

Read more...

JUMA-PILI!

>> Sunday, February 18, 2007


Hivi huyu JUMA ni nani?
Hivi kwanini baada ya jumatano anatengwa?
Hivi ana undugu na Alhamisi?
Hivi huyu Alhamisi ni nani?
Anaundugu na Ijumaa?

Lakini kabla sijaendelea kusema ngojea nimuachie Lionel Richie aseme....


Halafu ......

Lakini napenda siku moja nipende na niwenimenasa kama hawa Third World wasemavyo....

Read more...

Unaweza kujivunia Uafrika?

>> Friday, February 16, 2007


Kuna watu wananiambia kuwa mara nyingi inakuwa vigumu kwao kujivunia Uafrika. Mimi siwakatalii, kwani ni ukweli Afrika inamatatizo kibao. Kuna watu wanamatatizo kibao mpaka ingawa ninamatatizo milioni na uchafu huonaaibu kulalamika.

Lakini hebu niseme....


Napenda kurudia kusema kuwa, kwa viongozi wetu wa Afrika nirahisi kujivunia Uafrika kwa sababu wanaufaidi kuliko sisi wengine.
AU?

Lakini ngojea Thabo Mbeki aseme....


Kwa sababu nimemgusia Raisi wa Afrika Kusini, halafu ni ijumaaa, sitaki kukuacha bila muziki. Kwa muda mrefu miziki ya Afrika Kusini imenisaidi kupitisha siku za shida na raha.Wikiendi nyingi nimehuzunika na miziki hii na kufurahi na miziki hii.

Ngoja tujikumbushe historia fupi ya miziki ya Afrika kusini.....


Haya basi!Ijumaa na wikiendi njema!
Doh!Jinsi siku zinavyokimbia mtu utajistukia mwaka umeisha halafu chakuonyesha hakuna!

Swali:
Hivi historia ya miziki ya Tanzania imeshafanyiwa kazi?

Ngoja nikuache na ........


Afrika ndio iko mawazoni leo hii.Je, wewe unajivunia Uafrika?.

Read more...

UGUA POLE!

Sijui kwanini sentensi hii ifarijio watu kibao hunizingua!

Huwa maranyingi nasikia :Haya kwaheri!
Ugua Pole!
Hivi kitu hiki kinawezekana?

Read more...

Ushawahi kufikiria kuanzisha dini?

>> Thursday, February 15, 2007

Katika watu wanizinguao kwa jinsi wanavyoweza kushawishi na kujiamini hata katika yale mambo ambayo watu kibao huogopa, ni huyu mtu ajulikanaye kama Jose Luis de Jesus Miranda.

Huyu kapitiliza pale wahubiri wengine walipofikia. Yeye hujiita Yesu. Lakini anasema yeye ni zaidi ya Yesu. Yeye ni Mungu.

Kwa wale wanaoogopa kwenda Jehanamu, huyu dini yake bomba. Anasema hakuna dhambi.

Swali:
Unaogopa kukufuru eeh?

hebu msikilize....

Read more...

Ksii Ksii, Halloo dada eeh!Nisubiri basi !

>> Wednesday, February 14, 2007


Inasemekana wanawake hutokea sayari ya zuhura(Venus) na wanaume hutokea mars(sijui kiswahili chake). Basi kutokana na kutokea katika sayari mbili tofauti basi kasheshe haziishi.
Chakutisha hata urafiki kati ya mwanamke na mwanaume unachokochoko zake.


Inasemekana kuna watu wengi duniani hupenda kuhalalisha kuwa urafiki kati ya mwanaume na mwanamke hauwezekani bila ngono kuhusishwa. Wengine wanasema mwanamke ananguvu ya kutomtamani mwanamme. Hivyo mwanamke asiyevutia wanaume ndio pekee akaribishwaye kama rafiki wa kawaida na mwanaume. Huwa najiuliza, hivi kuna mwanamke asiyevutia mwanaume lakini?Si tushaambiwa kuwa kizuri kijichoni mwa mtazamaji lakini?

Halafu kunaimani kuwa ni wanaume tu huwa wanafukuzia wanawake. Nisikufiche baada ya kutembea hapa duniani mara nyingi tu nimekuta mwanaume kabanwa kwenye kona na mwanamke anapewa kauli halafu yeye ndio anajikanyaga. Kwa bahati nzuri mimi kwa mara yakwanza ilinitokea nikiwa darasa la sita, nilipopigwa kauli na mwanadada mpaka nikawa naona noma kwa sababu watu walishuhudia halafu wakaanza kunitania kwa jinsi nilivyoishiwa kauli.

Swali:
Hivi hizi choko choko za mahusiano kati ya mwanamke na mwanaume, hutokana na tamaduni za jamii au hata baolojia ya binadamu hucheza kipengele?


Haya siku hii ya leo watu wengi husherekea VALENTINE' Day. Husherehekewa sehemu nyingi na wapendanao, nikiwa na maana wapenzi, lakini sehemu nyingine imekubalika katika marafiki wote. Chokoleti na kadi kibao huhusishwa katika kujaribu kuhakikishiana kuwa penzi bado limewaka moto!

Haya mahusiano ya wapendanao ni sanaa kali sana hasa ukikumbuka tofauti za wanawake na wanaume hata katika kuonyeshana mahaba.
Lakini siku hizi ni kawaida kusikia maswala ya usawa wa jinsia.
Wanaume =wanawake.
Ila kinachonitisha ni kwamba bado katika jamiii utasikia lugha hizi:

Utamsikia mwanamume akimuona mwanadada:Duh !Umeona mtoto yule?
Naamini hamaanishi mtoto mdogo aliyezaliwa, lakini huhisi kwamba kunakauhusiano ndani zaidi ya asemaye hivyo kuwa;
mwanamke = mtoto.

Nasikia vilevile wanawake wanamajinayao kwa wanaume:Buzi, Nguruwe nk
Lakini mimi pamoja ya yote ningependa heshima ikuwe zaidi katika jinsia hizi mbili.Na ningependa wanawake wadhidi kuheshimika. Kumbuka hawa ndio mama zetu. Halafu ni ukweli bado hawapati heshima wastahilio.

Tuachane na mifano hiyo yangu ya juu niliyoitaja. Haina nguvu katika kutafsiri mahusiano ya mwanamume na mwanamke. Labda msome Lisa Melton katika atiko yake ajaribu kuelezea naye jinsi gani wanaume huanza kubadilika tokea SRY gene inapoanza kufanya mambo.

Ila kuna huyu Karen Salmansohn ambaye kunabaadhi ya marafiki zangu wa kike wanampenda sana kwenye kitabu chake aongeacho jinsi ya mwanamke awezavyo kuiga siri za wafundisha mbwa jinsi ya kum-control mwanamume.Anadai kama wanaume watokeavyo Mars, mbwa pia. Kama wanawake watokeavyo Venus, paka pia.
Baadhi ya asemavyo kongoli hapa.

Swali:
Hivi wewe unarafiki wa jinsia tofauti asiyekutamanisha kunanihiii?


Mimi nao.
Je, na wewe unaamini katika jamii huru ni mwanamke awekaye mazingira ya mwanamume kumtupia kauli?

Duh!Nakiri sijui mbinu za utongozaji wa wanawake!

Haya kwa wale washeherekeao Valentine's day.Mmeshanunua machopochopo?

Heri ya Valentine!
Lakini ngojea mimi niendelee na Manu Chao hapa.....

Read more...

Kuchamba kwa aina yeyote ni staili tu mojawapo yakushika mavi.

>> Tuesday, February 13, 2007


Kwetu wengi ni ujanja kukimbia baadhi ya kazi ziletazo masilahi katika maisha.
Tunachagua kazi kutokana na sifa au tafsiri ambayo kwa vigezo fulani inaleta aina fulani ya heshima ikubalikayo katika jamii ilengwayo.
Wakati nafuatilia maswala ya ni nini taaluma au kazi yenye heshima nikastukia kuwa jambo hili si rahisi kama nilivyokuwa nafikiria.
Nikakuta kuna jamii marubani ndio wenye heshima zaidi.Jamii nyingine ni madaktari.Nyingine wanasiasa , wafanyabiashara nakadhalika.
Halafu nikastukia pia jinsia huchangia pia katika kuchagua hadhi ya taaluma fulani fulanni. Nasikia siku hizi mitaa ya Brazil ,ukiwa daktari uliyebobea katika operesheni plastiki zenye kulenga urembo, basi wewe ndio kiboko.Wakati wasichana wengi Russia inasemekana wanakuheshimu sana ukiwa mfanyabiashara.

Sasa ukisikia jinsi maswala ya kubeba maboksi na ufagizi yanavyozungumziwa na baadhi yetu utaweza kufikiri hiyo ni kazi ya ajabu sana.Unaweza kufikiri kuwa wafanyao kazi hiyo si muhimu. Lakini ukweli ni kwamba kazi ni kazi.Na kazi yoyote inayo kupatia maslahi mimi naamini ni kazi bomba. Na mara nyingi hizi hughuli ambazo hata hatuzitaji kwenye umuhimu , ndizo zitusaidiazo sana kila siku.

Swali:
Umuhimu wa kazi ni nini basi kama si kukupatia maslahi?


Halafu je, unafikiria ni kitu bomba kama watu wote watabobea kwenye shughuli zile ambazo jamii fulani imechagua tafsiri ya kwamba zina hadhi ndogo?

Hivi hadhi yako si kitu cha kufikirika tu kwako na hata katika jamii?
Au unafikiri kuna ukweli wa zaidi ya kifikira?


Ndio, madaktari ni muhimu, lakini unafikiri waosha maiti wakikosekana nini kitatokea?

Unakumbuka moja ya kitu kitufanyacho kuwa binadamu baada ya kula ni ile haja ya kwenda haja kubwa. Baada ya kumaliza haja ,kuchamba kunafuatia.

Hapo kila mtu sasa huonyesha maringo yake dingiri dingiri mpaka chini!

Wengine hutumia maji ,
Wengine makaratasi,
Mawe,
Majani,
Mchanga,nk.

Kila mtu hutetea staili yake ya kushika mavi inamafanikio zaidi.Au wengine husema ni ya usafi zaidi.


Lakini lengo la wote ni moja. Kuweka moja ya sehemu nyeti katika mwili wa binadamu iwe safi.

Lakini mimi naamini hiki kitendo wote tunakifanya na hatukionei kinyaa.
Hivyo kama wote tunaweza kufanya kitendo hiki mara kwa mara, sioni sababu ya sisi walewale kuanza kufikiria eti kuna baadhi ya shughuli haitufai au ina hadhi ya chini.

Kwamaana naamini kitendo cha kuchamba ni shughuli ya hadhi ya chini ambayo wote huishughulikia kwa makini na mafanikio bila kulalamika.
Duh! Hivi kitendo hiki cha kuchamba ni cha hadhi ya chini kweli?

Halafu ushastukia kuwa vyote tuvitumiavyo kufanikisha shughuli hii ukiviangalia katika kona nyingine vyote ni uchafu?

Hapa nazungumzia maji,makaratasi, mawe majani na vingine vyote vitumikavyo kama makokoneo.

Maji yaweke yasipotakiwa, makaratasi ,nk. yote yanafanikisha tafsiri ya uchafu.
Pia yanaweza kuitwa uchafu kama hayalengi ufumbuzi wa jambo lilengwalo.

Sasa sikatai kuwa taaluma yako ni muhimu kwako.Sikatai kuwa jamii inatafsiri na kuzipa hadhi taaluma fulani fulani kutokana na mahitaji yake katika jamiii. Sikatai kuwa taaluma yako inaweza ikawa ndio inaumuhimu katika jisi utafsirivyo hadhi yako.

Lakini kama unaenda haja kubwa na unachamba , mimi nahisi tuko katika hadhi moja.

Unaweza kunibishia na kunikatalia lakini!

Swali:
Hivi kwanini kinyesi cha mtu mwingine kinatutia kinyaa kuliko cha kwetu wenyewe?
Au ndio kinanuka zaidi?


Duh!Sijui kwanini kitendo hiki kinaitwa kujisaidia.Lakini tusisahau kushukuru kama tunapata choo.Kwa maana inamaanisha tumekula chakula.Na tusisahau kuwa kunawatu wanakufa njaa sasa hivi.

Haya tufanyeni tu hizo kazi zitupatiazo maslahi.

Siku njema!

Read more...

Mwezi wa Historia ya mtu mweusi

>> Monday, February 12, 2007

Marekani na Canada mwezi huu wa pili huenzi historia ya watu weusi. Kutoka mwaka 1926 wakati ilikuwa ni wiki moja, mwaka 1976 kuanza kuenziwa kwa mwezi mzima , na mpaka leo, twaweza kusema mambo mengi yamebadilika.

Swali:
Hivi mambo yamebadilika kweli?

Bado ni kawaida kuitana majina ya ajabu ajabu , kuuana na mambo mengine kibao.
halafu ishaanza kuwa kawaida kusikia vita kati ya Walatino na weusi Marekani. Sasa ikiwa mwanzo tatizo lililokuwa likizungumziwa kuwa ni la weusi na weupe tu, inakuaje sasa hivi weusi na walatino wanapigana vikumbo mtaani?Je , ule ugomvi wa wazungu na weusi hautoshi?

Halafu kale kamchezo kakuitana majina kati ya watu weusi na weupe masharti yake huwa yananizingua sana.
Hebu mcheki huyu mwalimu akijitetea..


Ni sawa kuwa watu weusi sio wenye matatizo peke yao. Ukisikia ya Wapalestina wanavyo bwengana sasa hivi kwa sababu wengine ni Hamas na wengine fatah unaweza ukaingia dhambi ya kupata uahueni kwa kuona matatizo si ya watu weusi tu. Lakini kunakitu nadhani utakuwa unakisahau au hutakiwi kukisahau hivi sasa. Ukweli ni kwamba asilimia kubwa ya watu weusi wanakosa kujiamini. Watu weusi bado tunaaminishwa kuwa hatuna thamani kutokana na rangi. Karibu kila kona ya dunia tunajaribu kuaminishwa kuwa hatuwezi maswala.

Ukweli ni kwamba ni mimi na wewe ndio tutakiwao kubadili hii mitazamo ya watu. Katika mwezi kama huu ambao huenziwa Marekani na Canada, sioni ni vibaya kujikumbusha na kukumbuka kuwa mapambano yanaendelea.Watu wote weusi duniani ni muhimu kukumbuka kutosahau hili.Na kivyetu vyetu kujitahidi kuwa mchango chanya.Bado tunahitaji watu wamifano wengi. Akina Mandela hawatoshi.

Swali:
Lakini ni kwanini tuenzi historia ya watu weusi kwa mwezi tu? Je, sio siku zote tuishizo ni za kuenzi historia yetu?
Je, unasemaje kuhusu mwanamume mweusi huyu anavyoenzi mwezi huu wa kukumbuka historia ya mtu mweusi?Hebu msikilize......

Ingawa tukiliangalia swala hili katika kona tofauti , unaweza kuona kuwa labda kunatofauti ya unyonge kati ya mwanamke mweusi na mwanaume mweusi. Lakini naamini tukizidi kuimarisha timu zote mbili - wanawake weusi na wanaume weusi- ikawa timu moja isiompendelea mwanamme, timu yetu itakuwa babu kubwa.Kwani bado naamini kuwa kunatabia ya kutowashirikisha wanawake katika maswala kwa kuamini kuwa wao wanapendeza nyumbani tu. Naamini tunapoteza baadhi ya vichwa muhimu kwa kufanya hivyo.

Dondoo:
Unakumbuka hii filamu aliyoitengeneza Kiri Davis, ionyeshavyo mpaka sasa jinsi gani watoto weusi hujisikia wamepitwa uzuri na weupe?

Au icheki hapa basi tena....


Ukiangalia hiyo filamu hapo juu utaweza kusema kuwa hilitatizo ni la watoto wazaliwao na kukulia nje ya Afrika. Lakini nauhakika lawezakuwepo popote kama watoto watakua wakiwa hawana mifano ya kujivunia ifananayo nao.
AU?

Haya ndugu zanguni!
Baadaye!

Read more...

Hivi unatafuta maisha eeh?

>> Sunday, February 11, 2007


Hivi ukishazaliwa si maana yake unaishi?
Au?
Unatafuta maisha eeh?
Duh !Hapa nilipo kuna baridi!


Lakini maisha magumu!

Halafu pesa hii inayosemekana ni sabuni ya roho nishai kweli!
Lakini ngojea Pink Floyd waongee.....

Read more...

Aliko alizaliwa Jana!

Duh! Nilisahau kuwa jana ilikuwa siku yako Aliko!Heri ya kuzaliwa!Aliko eeh !Mara nyingi watu hatusemi tufikiriavyo kuhusu watu wengine. Lakini ukiniuliza mimi nitasema ,.....
Wewe Bomba!

Nakutakia kila la heri Aliko!

Kama humjui mtafute kwenye picha hii niliyoichukua mwezi jana.

Hapa je?

Naamini umemstukia.

Ngoja nimuache Stevie Wonder na Gilberto Gil wanisaidie kuku.......

Read more...

Tufurahi ingawa tunamatatizo!

>> Friday, February 09, 2007

Wikiendi hii Uko na umpendao?
Mimi nahisi sijawahi kupenda bado.Nikisema hivyo, usichanganye na kuhisi kwamba mimi mpweke!

Duh !Ushastukia matatizo hayaishi?

Read more...

Wauaji!

>> Wednesday, February 07, 2007

Nyerere aliua.
Mkapa akaua.
Bush Anaua.
Blair anaua.
Papa John Paul aliua.
Ayatollah Khomeini alikuwa muuaji.
Mandela aliua.

Hivi hawa viongozi wakitoa amri watu waende vitani wanasahau kuwa amri hiyo niyakuruhusu kuua? Wakitoa amri watu wauawe inamaanisha sio wao walioua kwa sababu si wao walioshika bunduki au kitanzi kuua?


Hivi muuaji ni nani?
Hivi muuaji ni yule tu ambaye amejistukia kaua au jamii imetafsiri kitendo chake ni uuaji?

Kwa nini wapiga wezi Tanzania hawajisikii kuwa ni wauaji hata kama wamempiga mwizi mpaka akafa?

Hivi kwanini binadamu wanachagua nani wakumuita muuaji?

Je mimi na wewe si wauaji?

Usitishike najiuliza tu!

Read more...

Ayaan Hirsi Ali


Maswala ya kidini ni magumu sana. Lakini kunabaadhi ya watu wanavyoyakabili huniacha mimi mdomo wazi. Huyu mwanadada Ayaan Hirsi Ali aliyezaliwa Somalia na kukulia Kenya kabla ya kujilipua Uholanzi ni miongoni mwa watu hawa ambao huniacha mdomo wazi.
Niliangalia akihojiwa siku moja nikaamini kuwa kama Salman Rushdie aliwekewa fatwa sitashangaa kuona huyu akiwekewa hivi karibuni.Baadhi ya ayasemayo ni haya....
Pamoja na kutengeneza sinema itwayo submission iliyofanya director wake auawe na kumfanya yeye awe kwenye listi ya kuuawa, haachi wala kupunguza kusimamia ayaaminiyo.
Sehemu ya sinema hii ni hii hapa...


Nachojiukiza ni kwamba hivi mpaka wa kusimamia uaminicho ni upi?


Je, msimamo kama wa Martin Luther King Jr aliyekuwa anaamini mtu asiyeweza kufia kitu hafai kuishi ni sahihi?
Unaikumbuka misemo ya Martin Luther King Jr?

Read more...

Marafiki asanteni!

>> Tuesday, February 06, 2007

Tokea nianze kublogu nimebahatika kujifunza mengi lakini pia nimefanikiwa kujenga uhusiano na wanablogu kibao. Wengi wao sijawahi kukutana nao lakini huwa nasahau kuwa sijawahi kuwaona uso kwa uso. Naamini hii ni moja ya nguvu ya blogu. Wanablogu kama NDESANJO, EGDIO, DAMIJA, Luihamu...nk huwa nasahau kabisa kuwa sijawahi hata kukutana nao, kwa jinsi nilivyowazoea kifikira.Ila Rasta Luihamu wewe mdini ile mbaya! Nakutania:-). Wanablogu kama MWANDANI, JEFF , MJENGWA, nk blogu imerudisha mawasiliano ya karibu kwani ni siku nyingi hatujakutana. Na kizuri ni kwamba kila siku nakutana na kujifunza kutoka kwa watu wapya .

ASANTENI WANABLOGU WOTE!

Siwezi kusahau kuwa marafiki zangu wote hunipa tafu sana. Napenda kuchukua nafasi hii nyingine kuwashukuru wote, kwa yote. Sina picha za wote lakini nimeona niweke baadhi ya marafiki zangu ambao tumebahatika kukutana siku za karibuni na nikabahatika kuwa piga picha.

Basi baadhi ni hawa.....
Bonanza na Rummy


Halafu unajua watu wengi hawajui Rummy ni Mtanzania....hebu mcheki hapa akiwa na bendi yake ya MIGHTY 44
Haya tuendelee..
Erick
Ronaldo
Deo


Aliko
Edo,-na Raymond

Gonzaga a.k.a Mr Dj

Erick the Godfather

Chriss a.k.a T.I


Byamungu a.k.a Smooth
Chacha

Ben a.k.a TerminatorAllen


Mernad a.k.a Promotor
Mtimkubwa, -, na DJ Ezza

Haya jamani tuendeleze libeneke!

Read more...

Hivi kama Afrika sisi ni masikini haturuhusiwi kucheka?

>> Saturday, February 03, 2007


Mapambano yanaendelea!
Kabla sija sema......
Kassav


Nashangaa kwamba nimekutana na watu wanashangaa, itakuwaje Afrika ina matatizo bwelele lakini Waafrika bado wanatabasamu.Mwingine akaniambia kuwa Afrika iko nyuma kwasababu Waafrika tunatabasamu wakati tuna shida. Mimi naamini hii ni kurahisisha mambo. Furaha na kilio si siri ya kwenda mbele kimaendeleo.Ni siri iishiyo ndani ya binadamu. Naamini kuwa Waafrika, hata kwenye kucheka hatusahau kilio. Au?

Swali:
Hivi maendeleo ni nini?

Halafu.....
Mory Kante

WIKIENDI NJEMA!

Read more...

Tanzania kama ni msichana!

Duh! Hivi kwanini sina mpenzi? Hivi hakuna bloga mwanamke mzuri ambaye ataruhusu tutamaniane?
Natania!:-)
Lakini Tanzania kama ni mwanamke wangu huuu ndio wimbo ningempa....................

Read more...

Is U experienced?


Katika njia za maisha lazima utapigwa chini mara kadhaa .Lakini kitu kizuri ni kwamba unajenga uzoefu na inafikia siku huwezi kuzinguliwa kirahisi.

Je, we mzoefu?
Nimemkumbuka Barrington Levy leo

Read more...

Tanzania

>> Friday, February 02, 2007

Iko siku jina hili litakuwa likihusianishwa na mafanikio!
Lakini mpaka siku hiyo ni mimi na wewe tunaohitajika kubadili watu wafikiriavyo kuhusu Tanzania.Inabidi tujaribu kubadili mambo .La sivyo ni hawa hapa chini watakaoendeleza mitazamo ya watu kuhusu Tanzania.
Hebu angalia kazi aliyopelekewa Mr Loewestern
Afadhali na hii.....


Itakuwafuraha ikifikia siku ambayo ilikuitangaza Tanzania haitahitaji tuzungumzie wanyama na Mlima Kilimanjaro kama vigezo muhimu kuliko vyote.

Read more...

Mkopo na ladha ya ukwaju!

>> Thursday, February 01, 2007

Katika kipindi nasoma Mazengo Secondary, siwezi kusahau jinsi ilivyokuwa kasheshe pale mkopo wa chapati kwa Mama Kabota ulipokuwa umepitiliza. Halafu unajua huna sababu nyingi zakuombea pesa nyumbani. Kisingizio cha kuugua ulishakitumia ukatumiwa pesa. Iliyobaki unaanza kubadilisha njia ya kukwepa maeneo yote ambayo unahisi utagongana na Mama kabota. Ukigongana naye bila kutarajia unanywea mpaka unajionea huruma mwenyewe.

Kwa ujumla kudaiwa ni jambo ambalo linazingua sana. Unaweza ukastukia umebunia njia za uchochoroni ambazo haujawai kuziwazia ili tu kukwepa kugongana na anaye kudai. Safari ya dakika tano inaweza kukuchukua saa nzima kutokana tu na kumkwepa anayekudai.

Sasa mimi inanishangaza jinsi Viongozi wetu wanavyokuwa huru kwenda kuomba mkopo mwingine. Wananishangaza waonekanavyo wenye furaha na uhuru wawapo pamoja na wanaodai. Halafu hukawi kukuta hata wakiwa likizoni wanaenda kupumzikia kule wanakodaiwa. Hivi hii ni hali ya mkopajia au hili jina mkopo linamaana tofauti kwa viongozi wetu?

Unakumbuka unavyonyong'onyea wakati unaenda kuomba mkopo?Je, huwa unapata kigugumizi eeh!

Read more...

Davos!-Hivi hii sio shoo ya pembeni tu?

Kila ninapozidi kusikia maswala yanayosemekana kufanyika Davos katika WEF(World Economic Forum) , nashindwa kujizuia kufananisha mkutano huu na sideshows zilizokuwa maarufu katika circus. Nashindwa kuacha kufikiria kuwa hawa viongozi wetu wa nchi maskini hualikwa hapo kuwa kama vituko kwa matajiri kuangalia.

Huu mkutano uwekao kiwanja kwa wafanyabiashara maarufu na wanasiasa kutoka nchi tajiri kujadili maswala kwa kigezo cha kupata muelekeo tofauti katika dunia ,mimi naona ni kigezo tu kitumikacho kuwaunganisha wenyenavyo . Kwa maskini aalikwaye ni kama kituko cha kukodolewa macho tu.

Unakumbuka lakini sideshows za zamani? Zile ambazo zilibobea kwa kuwaweka binadamu kwenye show kwa ajili ya wengine kuwa kodolea macho ilikuwa na furaha? Zile zilizomfanya Sara Baartma , the Hottentot Venus maarufu.
Au zile zilizo wafanya hawa mapacha wa Kisiamizi ,Chang na Eng kuwa maarufu dunianiBila kumsahau Prince Radian na wengine wengi.Si sisikii kitu chochote wafanyacho wawakilishi wa watu maskini katika mikutano kama hii. Lakini ni kawaida kuwaona viongozi wetu wakiwepo huko na wakikodolewa macho. Nasikia na baadhi yao huwa maarufu sana kwenye mikutano hii kwa kujua kuwachekesha wenye navyo na pia kwa sababu tu ya kuwepo katika vijiwe hivyo.

Kama kwenye sideshow muda ukapita na watu wakastukia kuwa hakuna mpango kuwa kituko tu katika onyesho ili mradi kunapesa inaingia. Sasa ningependa tuone viongozi hawa watuwakilishao wanaendesha shoo na sio kuwa vituko vya kukodolewa macho tu.

Read more...

Idumu Jumuiya Ya Wanablogu Tanzania


Photo Sharing and Video Hosting at Photobucket

Partner

save mt. Kenya campaign
In partnership with africapoint.com

Taswira BANANGENGE

  © Blogger templates Romantico by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP