Hivi Huyu Demu Mapepe?
>> Wednesday, February 21, 2007
Nilipata bahati ya kusoma katika sekondari ya Mazengo , Dodoma, kabla haijafutwa.Ilikuwa shule ya wavulana pekee. Wanaume tulikuwa wengi kwa mamia na mamia, halafu tukobodingi. Hapo basi kasheshe inayotokea ni hile ya kukosa wasichana.Halafu kumbuka asilimia kubwa yetu ndio tuko katika ile miaka ambayo sekunde chache sana zinapita bila kufikiria wanawake.Unajua tena baolojia ya miili. Wasichana ambao ilikuwa tunawaonaona kabla kupata ruhusa kwenda mjini ni watumishi wa walimu na pia wasichana kutoka vijiji vya karibu.Lakini ilikuwa ukishikwa na wanakijiji umeenda kudoea ,jasho litakutoka. Halafu tena wale wafanyakazi wa walimu nao ilikuwa ni vigumu kuwafuata nyumbani kwa walimu.Ingawa baadhi ya watu walifanikiwa kupona kinamna hii. Shuleni kwetu tulikuwa tunategemea zaidi wasichana watokao sekondari ya wasichana tupu wa Msalato. Hawa ndio tulikuwa tunawaalika tukiwa na sherehe na yale mambo ya disco la mchana. Basi siku wanayokuja ilikuwa inakuwa kasheshe. Utakuta siku hiyo watu wanaazimana nguo, utasikia watu wananukia perfume na hata wengine ndio siku za kupiga mswaki. Siku nzima wajao hawa wasichana utakuta mabwenini hakutulii. Cha ajabu ilikuwa baada ya hawa wasichana kuja halafu disco kuanza inakuwa taabu tena kutafuta patina wa kucheza naye au hata wa kuongea naye. Kwa sababu kunakuwa na watu wengi waogopao kutolewa nje wakiomba kucheza au kuongea na msichana. Na sababu kubwa ilikuwa, ukitolewa nje na msichana utataniwa sana mabwenini. Hivyo basi siku hizi zilikuwa na mambo yake. Nataka-sitaki nyingi ile mbaya!
Basi bwana, bahati ikatuangukia shuleni kwetu.Wakaanzisha kuleta wasichana wachache wa O-level kuja kusoma kama wanafunzi wa mchana.Wakaletwa wasichana 35 hapo.Walipofika tu, tukawapa jina vikuyu. Wengi wa hawa wasichana , walikuwa wametafsiriwa mabwenini kuwa si wazuri.Hivyo ilikuwa ni kitendo cha aibu ukionekana unafukuzia yeyote katika hawa. Ila sasa kumbuka tuko mamia na mamia ya wavulana wasiopata kusikia sauti ya mwanamke mara kwa mara, halafu unaleta wasichana 35 katikati yao!Nahisi unajua litakalotokea! Naamini hawa ni baadhi ya wasichana waliofukuziwa na kupewa kauli za kila aina kuliko wengi duniani. Wakulilia alilia, wakujifanya mcheshi alifanya hivyo, bila kuwasahau wakutishia, ili mradi tu kila mtu alikuwa analenga kujipatia kidude. Kutokana na redio za mianzi hawa wasichana hata aliyekuwa mgumu kiasi gani, alijikuta tu siku ananasa kwa watu fulani.Kwa maana mbinu zote za vita zilitumika.
Nimeikumbuka hii hali leo baada ya kugongana na jamaa anamlilia kabisa mwanadada ndani ya treni. Lakini ukweli ni kwamba anaigiza kwa sababu nishamuona akifanya hivyo kwa mwanadada mwingine siku chache zilizopita. Ila nachomvulia kofia ni sehemu anazofanyia kitendo. Kwenye stendi ya Treni, ndani ya basi, sehemu ambazo kuna watu wengi. Lakini labda kagundua anahurumiwa zaidi kutokana na wasichana kuonanoma watu tunavyojifanya hatustukii kinachoendelea lakini tunapiga kijicho kishkaji na kucheka mbele. Au labda akina dada ndio wanaamini ni mkweli kwasababu analilia hadharani!Sijui!
Duh !Lakini , kuna watu wanajua kuomba!Nafikiri wangefanya hivi katika kuomba kazi , basi kazi yoyote ile duniani wangepata.Halafu mwanadada akikubalia jamaa kadhaa walioonyesha juhudi anaitwa mapepe.Duh!
Ngoja nikuache na Kingwendu family wakuache na huu wimbo Mapepe....
Tusisahau kuna UKIMWI lakini!
Baadaye!
6 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:
Mapepe ndio yenyewe katika kufunika soni! Kuna wakati huna budi kufanya mapepe ili kunanikiwa! Aidha kuhusu Mazengo na Msalato umenikumbusha mbali kidogo... Sio siri miaka ile ya themanini niliwahi kucheza Disco na akinadada wa Msalato! Lakini walionivutia kwa uchangamfu ni akinadada wa Central! Ilikuwa wakati wa UMISETA!
Hii ya disko la mchana umenikumbusha wana-Nsumba tulipokuwa tukiwaalika shuleni kwetu Nganza au walipokuwa wakitualika.
Basi wanafunzi wengi walikuwa ni wasukuma tena wenye lafudhi kali. Mziki ulipokuwa ukianza utaona mmoja anakufuata kama ifuatavyo:-
Kaka- dada roho yangu imekudondokea naomba tucheze.
Wakati mziki ukiendelea....
Kaka: sijui mwenzangu unaitwa nani?
Dada: Naitwa Juliana
Kaka: Mmh...Bonge ya jina..
Kaka: Sijui uko form gani?
Dada: Form three
Kaka: Mmhh!..Bonge ya fomuu....
kaka: Sijui unachukua combi gani
Dada: PCB..
Kaka: Mmmh...Bonge ya Kombi....
kaka: kwenye baiolojia mmefikia topiki gani?( ukimwambia atakwambia sisi tumefikia reproduction)
Basi ikifika hapo wasichana huanza mbele kiaina..., lakini na yeye humalizia, sawa dada, lakini mimi naitwa Masanzagulilwa anuani yangu ni sanduku la barua 1212 Nsumba sekondari....
Sasa hayo mazungumzo juu yanakuwa yanaenda sambamba na midundo ya muziki na lafudhi ya kisukuma. Ningekuwa nina ujuzi wa kurekodi video kama Kitururu ningewaigilizia mpate picha vizuri. Kitururu umetukumbusha mbali.
**Luihamu vipi na wewe ulisoma shule za jinsia moja?
@DaMija:Duh!
Tehe! Tehe! tehee!! Da Mija umenivunja mbavu leo Duh!"....roho yangu imekudondokea..."
Duh! Hata mimi roho yangu isha kudondokea Damija!Iokote lakini!:-)
Nimeziokota.
Post a Comment