Kuchekelea Wazungu !
>> Wednesday, May 17, 2006
Kwa muda mrefu sasa nimekutana na maswala yanayo nifanya nijiulize mambo mengi kuhusu ukarimu wa kibongo.Kuna wakati napigwa na butwaa hata pia kukerwa na ukarimu huu. Nazungumzia ukarimu uliojengeka sasa , ukarimu wenye masharti.Kunawakati ukarimu huu unanisababisha niamini kuwa, sisi wabongo tulitawaliwa na hawa wageni kutoka nchi za nje kutokana na ukarimu huu.Wabongo kwa kirahisi kabisa wanaweza kukuruka katika huduma ili wamuhudumie Mzungu. Nakubali kwamba ukarimu ni kitu kizuri, lakini naona huu ukarimu mara nyingine umekuwa unavuka mipaka, hasa ukiwa unapendelea baadhi ya watu katika matukio maishani. Kama sisi wabongo ni wakarimu kwa nini tusiwe wakarimu kwa kila mtu sawasawa, bila ya kujali anatokea wapi? Nakumbuka ukarimu wapewao watoto wamjini waingiapo kijijini unavyowaponza wanavijiji.Unakuta watokao mjini wanajaliwa zaidi mpaka katika maswala ya kujamiiana kitu ambacho kimesaidia kueneza ukimwi kutoka mijini kwenda vijijini bongo.Huu ndio ukarimu ninaouita wakuchekelea wazungu. Mara nyingi sana nimeshuhudia ukarimu huu ukiwezesha watu kujali watu wa mataifa mengine zaidi ya wabongo wenzao.Chakusikitisha ni kwamba tabia hii imejipenyeza mpaka katika serikali yetu. Angalia katika ubinafsishaji, wawekezaji wa nje hupewa ukarimu wa hali ya juu, hata pasipo sababu maalumu. Ukienda mahotelini ikatokea kuna wageni wa mataifa mengine wako hapo,mara nyingi, watapewa huduma kwanza kabla ya wabongo hata kama wabongo wamewahi na wanalipa vilevile.Huku magharibi ukiienda katika balozi za Tanzania, utakuta vilevile unaweza ukarukwa kwasababu kuna watu wa mataifa mengine walioko humo.Katika nchi kadhaa nilizo wahikutembelea za hawa Wazungu, kwa mfano, Finland, kuna kitu kimoja ninawasifu. Hata iweje huangalia matakwa na faida ya Wafini kwanza.Nchi ndogo kama Estonia, katika balozi zao , Muistonia kwanza ndio jina la mchezo. Lakini sisi wabongo jasho litakutoka.Rafiki yangu aliibiwa kila kitu Johanesburg ,Afrika Kusini, akaenda Ubalozini iliapate kibali cha muda ,ushauri au pasipoti ya muda, jasho lilimtoka.Ndio kwanza utafikiri kajipeleka motoni. Rafiki yangu mwingine ikamtokea Sweden ndio kwanza ubalozini walimshambulia kauza pasipoti.Cha ajabu wageni hawa tunao wajali Tanzania labda hawana kumbukumbu maana ukija kwao utashangaa mwenyewe jinsi wasivyokukukarimu . Mara nyingi ni mpaka wajue kunakitu watapata kutoka kwako ndio utakapo ona ukarimu wao.Lakini ,muda wote utajikuta unaonekana kuwa ni tatizo tu.Na mifumo yao yakuendesha nchi hujengwa kuzingatia zaidi wazawa nasio wageni.Wananchi wa nchi nyingi za Ulaya wanapenda kukukarimu kwa kukuuliza maswali haya: Umetokea wapi? Unafanya nini?Lini utaongoka?Ila wenzetu wanapenda nchi zao na wanajua jinsi ya kuzipanguvu nchi zao. Wananchi wa Finland kwa namna yoyote ile hujaribu kuisaidia nchi yao,kwa mfano, hata nyanya na vitunguu ,kama vimezalishwa Finland vinapigwa bendera ya Finland. Hata kama ni ghali kuliko vyakutoka nchi nyingine ambavyo ndio halihalisi, watu hununua vya kutoka Finland kwanza.Wanafanya hivi wakijua kuwa wanawasaidia wakulima wa Kifini.Katika miziki, nenda urudi utakuta watu hujali kwanza wanamuziki wao kabla ya kuanza kununua miziki ya wengine. Sisi wabongo ni wakarimu sana kwa mambo ya wenzetu mpaka utaona tunapenda kuvaa bendera za mataifa mengine, na vitu vyetu vya bongo hasa kukiwa na uhakika vimezalishwa bongo, ndio kwanza tunavikimbia. Angalia mpaka kanga wavaazo akina dada zetu zikafikia kuzalishwa India na kusaidia kuua viwanda vyetu vya nguo bongo.Ukarimu huu wakutoangalia madhara tunayayotendea Taifa letu ufe.Lakini naona hatujifunzi! Sasa hivi tunawakarimu wawekezaji madini yetu ,uzalendo wetu.... nk. Je hii sio sababu ileile tuliwakarimu wakoloni nchi yetu?Sisemi kuwa ukarimu ni mbaya, lakini ukarimu mwingine ni ujinga.
2 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:
Du niko muda Mrefu tu hapa Scandinavia area, Sasa miaka kumi hivi .Nilikuwa naishi Finland ,sasa niko Sweden.Bongo nitarudi kijumlajumla lakini sina tarehe maalumu.
Zemarcopola inasikitisha sana:-(
Post a Comment