Mtakatifu SIMON KITURURU - MAWAZONI

FALSAFA na WAZO ndani ya neno - DUH!

Baadhi ya Dondoo kuhusu Tanzania Leo Hii Kwenye Kitabu Cha CIA

>> Friday, May 26, 2006

Kitabu hiki cha CIA hua kinanizingua sana wakati mwingine. Kwa sababu kuna watu wengi ndio hukichukulia kama ndio ukweli mtupu usio na dosari hata kiduchu.






#Mzozo wa Kimataifa: Mzozo na Malawi juu ya mpaka kwenye ziwa Nyasa na Mto Songwe

#Namba ya Meli: Tanzania ina meli kumi tu.

#Watumia intaneti: Kuna watu 333,000 tu watumiao intaneti Tanzania

#Stesheni za TV: Kuna stesheni tatu tu za TV.

#Simu za nyumbani: Kuna 149,100


#Wakulima: Wakulima ni asilimia 80%


#Ardhi ilimikayo: Ardhi ilimikayo ni 4,23% tu.



#Watanzania kiumri: Umri wa kati ya miaka 0-14 ni asilimia 43.7% ya Watanzania wote.
wwavulana ni 8,204,593 na wanawake ni 8,176,489. Hii inamaana baada ya muda kutakuwa na upungufu wa wanawake 28104 wa kuoa kama kila mwanaume katika kikundi hiki atahitaji mke.

Read more...

JE UNAWAKUMBUKA WAAFRIKA WASIO NA RANGI?

Tokea mara ya kwanza kumsikia Salif Keita ,nilishindwa kujizuia ila kuwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wake. Wakati nikijiandaa kwenda kuangalia onyesho lake jumanne ijayo hapo mjini Helsinki, nimeshindwa kuepuka kukumbuka kuwa yeye ni miongoni mwa Waafrika ambao pambano lao husahaulika.



SALIF KEITA
(The Golden Voice Of Africa)














Hili ni pambano lakukubalika katika jamii ya Waafrika na hata ya watu wenye rangi nyingine, aambalo limejaa kasumba na mila potofu za kuwatenga mazeruzeru. Kwa wale wasikiliza muziki wa reggae wanaweza kumjua Mzee Yellowman . Huyu Mjamaika namuingiza hapa ilikuonyesha kuwa hili pambano ni dunia nzima. Kwani hata yeye ukifuatilia maisha yake utakuta kuwa mila hizi za ubaguzi zilimdhuru sana huko Jamaika.

KING YELLOWMAN













Tukirudi hapa barani Afrika, huko nchi za kusini, inasemekana kumeingia mpaka imani potofu kuwa mtu akifanya mapenzi na zeruzeru basi atapona UKIMWI.

Ukisikia mambo watu wanayohusisha uzeruzeru nayo,utashangaa mwenyewe! Soma zaidi hapa. Kuanzia kuwa wamelaaniwa, wanaleta bahati mbaya mpaka kuwa wana mapepo wachafu. Mpaka dunia hii ya leo, achilia mabali siku hii ya leo, inashangaza kuwa watu wanashindwa kujua kuwa watu hawa walichopungukiwa ni chembechembe za melanin tu, ambazo ndizo zitufanyazo wengine tuwe weusi,wengine ,weupe , kahawia, nk. Lazima tukumbuke kuwa watu hawa bado wananyanyasika mashuleni , makazini , na katika jamii kwa misingi isiyo kuwa na ukweli. Cha zaidi cha kujua ni kwamba kutokana na kukosa hizi melanin , basi huathirika kirahisi na jua. Hupata cancer ya ngozi kirahisi kuliko watu wenye chembechembe. Pia huwa wana matatizo ya macho(vision). Basi sasa kwanini wanyanyaswe kwa mambo hata ambayo hayahusiani nao?


PRINCE YELLOW











Kabla ya kumaliza, nisingependa kusahau kumtaja Prince Yellow au Al Beeno na pia huyu mtoto wa Malawi Geoffrey Zigoma , wakiwatu ni baadhi ya wanamuziki wanaonikosha roho

GEOFFREY ZIGOMA













TUSISAHAU KUUNGAMKONO MAPAMBANO YA KUONDOA UBAGUZU HUU AMBAO UMEKITHIRI BADO KATIKA JAMII ZETU.

Read more...

LEO NI SIKU YA KUMBUKUMBU ZA UKOMBOZI WA AFRIKA!

>> Thursday, May 25, 2006


NAWATAKI WOTE HERI YA SIKU YA AFRIKA!
Safari bado ndefu ukombozi kukamilika. Naomba tuzidi kujengana na kusaidiana mpaka tutakapo fikia ukombozi kamili.

Read more...

TANGAZO:AFRIKA INATAFUTA VIELELEZO NA NGUZO ZA KUEGEMEA.(Ukiziona Mtaarifu mwenzio)

*Papa Wemba was not just a singer. He was also the prince, the "Pope" of SAPE.
Young men rushed to become clothes conscious dandies and carefully followed the special codes of SAPE, from their shoes to their hair style. A form of anti-poverty and anti-depression rebellion, SAPE was also a way of fighting against the dictatorship of the "abacost", a local version of the three-piece suit and virtually an official uniform of the Mobutu regime.
-RFI MUSIQUE

*Congolese immigrants living in Paris and Brussels, were busy living the Sapeur lifestyle - constantly hustling for money, keeping up with Papa Wemba's fashion ideology, and pursuing a `dedication' by Wemba, who is paid a lot of money by his fans in order to sing their names in his new album. Bragging and boasting, loud and proud, constantly advertising themselves and each other, they are stars on a stage they mentally construct in the absence of real ones. -IMDb



*Joseph Kony considers himself quite a good Christian, and he wants Uganda to be a Christian nation.If the LRA wins, Kony has promised that Uganda will become a theocracy, with laws based on the Biblical Ten Commandments.
-NNDB

*Joseph Kony adds: "Most people do not know me... I am not a terrorist... I am a human being, I want peace also." -BBCNEWS






Inasemekana binadamu alitokea Afrika, kwa hiyo si vigumu kuamini Muafrika ni miongoni mwa binadamu aliyekuepo muda mrefu hapa duniani. Hivyo lazima Waafrika tuna vielelezo(role models) au mifano mingi ambayo ingeweza kutupa kiegemeo wakati wa matatizo na mifano ya kufuata kujijenga kiakili, kiuchumi, kiutamaduni.....-au basi japo angalau kutupatia kujiamini katika mambo yetu. Hili si jambo dogo na kinanifurahisha kuwa bado watu tunaendelea kutafuta vielelezo hivi ingawa kama watapatapa maji hata nyoka unaweza ukafikiria ni mzizi ambao utakuokoa usichukuliwe na maji. Kuna mifano mingi ambayo ni rahisi kuiona ambayo inamwezesha Muafrika au mtu mweusi kutembea kifua mbele. Lakini pia iko mifano mingi zaidi ambayo inamsababisha mtu kuona haya kuonekana mbele za watu. Mifano mingine ni hii ya jinsi Waafrika tunavyotapatapa kutafuta nguzo na vielelezo vya kutusaidia.

Wenzetu Wamarekani weusi bado wananyanyua macho kutazama vielelezo kama vyakina Malcom X, Martin Luther King vikiwa mstari wa mbele.Lakini kwa miaka hii ya karibuni wamemchukua hata Mandela kama kielelezo chao. Sisi Waafrika hatuko nyuma tumewachukua akina Malcom X na Martin Luther, halafu Mandela ndio pekee bado ang'araye katika bara zima. Kwa mtazamo wangu mtu kama Nyerere pamoja na mafanikio yake mengi bado anachukuliwa kuwa ni kielelezo na nguzo iliyoshindwa, kutokana na baadhi ya mawazo yake mengi kushindwa kutimilika.Akina Mkwawa na wakina Kinjekitile hao ndio kabisa hatuwakumbuki, natukiwakumbuka ni kama hadithi isiyotufundisha kitu leo. Kitu ambacho si ukweli. Ila kukatisha hadithi ndefu , ningependa kusema vielelezo na nguzo zetu nyingi tunaziacha zife. Ila hii ni mifano ambayo iko wazi kupita kiasi. Ningerudi katika mifano miwili ambayo naiona inaelezea jinsi watu tunavyotapatapa kutafuta nguzo ya kuegemea katika maisha yetu ya leo kama Waafriaka.Mifano niliyopenda kuitumia ni Papa Wemba nguzo ni Nguo na Joseph Kony amri kumi za Mungu. Ingawa ukifikiria kidogo tu utapata kibunda cha mifano.

Mfano wa kwanza nautoa kwa Papa Wemba. Huyu Mkongo mimi nauhusudu sana muziki wake. Tukiachana na muziki kunakitu kingine yeye hujulikana nacho.Yeye ndio aliyeutia umaarufu Ukongoni mtindo wa kuvaa nguo za ghali na kusababisha kwa baadhi ya wafuasi wake kuamini katika mavazi kama vile watu wengine wanavyoamini katika Ukristo na Uisilamu. Yeye alipata kiegemeo katika nguo za ghali, akaanzisha kitu kinachoitwa SAPE('Société Ambianceurs et Persons Élégants') .Kuna documentary yake moja ukiiangalia utaona jinsi Wakongo kuanzia Afrika mpaka Brussels na Paris wanavyohangaika kutafuta pesa ilitu wasipitwe na toleo jipya la nguo kutoka mwanamitindo ya nguo Mfaransa, Mjapani au Muitali . Watu wako tayari kuiba ilitu wavae Armani, Gucchi,...nk. Soma hapa mahojiano ya watengeneza documentary hiyo. Ukifuatilia hii dini ya nguo ambaye papa wake ni Papa Wemba , utakuta kuna dalili nyingi zionyeshazo utapatapa maji wakujaribu angalau kujisikia kuwa kuna kanguzo kakuegamia. Tatizo lake ni moja tu. Kanguzo haka hakadumu kwa maana mitindo inabadilika kila kukicha. Hivyo Dini hii ya Kiafrika ambayo roho mtakatifu wake ni nguo za kutoka mtoni za bei ghali kama kielelezo na nguzo, naamini watu inabidi wafikiri mara mbili. Ndio utatembea uonyeshe maringo yako lakini sinauhakika na uwezo wake wakuziba uwazi katika maisha ya Muafrika na sifa ya Uafrika. Nguo kama mavazi tu sinatatizonalo lakini nguo zinapozidi kuwa kama mavazi naananza kuingiwa na mashaka.

Katika kutafuta kiegamio, mwafrika mwenzetu Joseph Kony akakipata kwenye biblia. Huyu Mwafrika mwenzetu mkereketwa wa dini na Afrika amekuwa vitani tokea mwaka 1987. Amejitahidi sana kupigania haki ya kutawala Uganda kikristo na kufanikiwa kuua watu katika maelfu, wengi tu kubakwa au hata kukosa kwa kukaa . Yeye anaamini kuwa amrikuu kumi zilizoko katika biblia zingeineemesha Uganda. Chakushangaza amefanikiwa kuzivunja hizo amri kumi mara nyingi tu katika kutafuta amani na maendeleo Uganda. Ila anasema anapenda sana amani.Msome hapa . Anakaririwa akisema anataka amani, wakati akishikishwa kitita cha dola elfu ishirini na makamu wa Raisi Sudani kusini. Mtu anaweza kumuamini, lakini je kielelezo anachokiegamia kinatufaa Afrika? Kama kinafaa sana mbona kinamshinda mwenyewe?

Naamini tunahitaji muelekeo Afrika. Mandela pamoja na upungufu wake amejaribu vyakutosha. Mandela amechoka sasa na ukweli ni kwamba Afrika inahitaji nguzo na vielelezo vingi. Tunazo nguzo na vielelezo vingi ambavyo tumevilaza. Inabidi tujaribu kuvifufua. Ushujaa wa watu kama akina Mkwawa inabidi urudi midomoni mwa watu. Pia tunahitaji mifano , vielelezo na nguzo mpya za kuegemea Waafrika. Kama ni wewe basi jitokeze. Akina Nyerere, Nkurumah na wale wote enzi ile walikuwa ni vijana wadogo tu. Usimsahau hata Gaddafi katika kundi hilo. Naamini nguzo na vielelezo vipya kama akina Kikwete hawatavitoa basi akina Jeff Msangi tunawasubiri.

Read more...

LIKITOKEA NIGERIA ,LIMETOKEA KWA AFRIKA NZIMA.

>> Tuesday, May 23, 2006

"What do you want me to do?" Akin asks in pidgin English, explaining why he turned to a life of Internet crime. "It is my God-given talent. Our politicians, they do their own; me, I'm doing my own. I feed my family - my sister, my mother, my popsie. Man must survive."

- Ndio asemavyo mtoto Akin kama anukuliwavyo na CNN.

Inasemekana katika kundi la Waafrika watano kuna uwezekano kuna Mnigeria mmoja. Hivyo utaweza kunielewa umuhimu wa Nigeria katika picha ya Mwafrika ionekanavyo duniani. Kinachosikitisha mpaka sasa hivi Nigeria pamoja na utajiri wake ,wasomi wake, na idadi ya watu iliyonayo inahangaika kuweka mambo sawa. Siasa ya Nchi hiyo haijatulia bado.Nigeria hata siasa zizungukalo jambo la idadi ya watu ni gumu sana.Wakaskazini kule kwenye jangwa jangwa ndio wanasemekana wengi na ndio wana chukua rudhuku kubwa kutoka serikalini.Ruzuku inasemekana hutolewa kutokana na idadi ya watu.Hivyo unakuta kule kunakotoa mafuta ambako ndio kusini kutokana nakuonekana kuwa kuna watu wachache basi kuna pata ruzuku ndogo. Wengine wanadai kaskazini kutokana na kuwa na viongozi wengi wakijeshi waliopita ndio maana waliweka maswala kupendelea kwao.Kwani kila siku watu kusini wanajiuliza, inawezekanaje kule kaskazini kwenye janga kukawa na watu wengi kuliko sehemu zenye chakula na ardhi nzuri? Kitu kingine cha ajabu ni kwamba wasomi wengi wa Nigeria wametokea kusini, lakini viongozi wengi walioongoza nchi wametokea kaskazini. Babangida na Buhari ni miongoni tu mwa viongozi wazamani wakijeshi wanaotakakurudi.



Hivyo ukimchanganya na Atiku(pichani)aliyekuwa makamu wa Raisi wa Abasanjo basi mwakani tutasikilizia uchaguzi wake. Naombea uende salama. Ingawa habari kama hizi maranyingine huleta utata ,ila inabakia palepale kuwa Nigeria ikitulia kuna sehemu kubwa tu ya Afrika itafaidika.Ingawa imejitahidi siku za karibuni kulipa madeni ,bado kuna mambo kibao yanayo itengenezea nchi hiyo na Afrika jina baya.


Katika kitu kinachonishangaza ni kwamba zile e-mail za kutoka Nigeria zinazozunguka mtandaoni kumbe bado zinawadaka watu. Lakini kama hazikukudaka zile basi je, zile pesa ulizotuma kwenye Western Union ,au ile Moneygram ilifika? Kongoli hapa

Ibrahim Babangida

Mwanajeshi kutoka kaskazinni ya Nigeria anayesemekana anapesa kama vumbi. Usijeukashangaa siku moja kuambiwa tajiri kuliko wote duniani sio Bill Gates ila Mnigeria mmoja ambaye haijulikani alifanyakazi wapi.

Read more...

UKOMBOZI WA MTU MWEUSI DUNIANI KWA MTINDO WA SUN TZU

*All warfare is based on deception

*Hence, when able to attack, we must seem unable; when using our forces, we must seem inactive; when we are near, we must make the enemy believe we are far away; when far away, we must make him believe we are near.

*If your opponent is of choleric temper, seek to irritate him. Pretend to be weak, that he may grow arrogant.

*If he is taking his ease, give him no rest.

*Attack him where he is unprepared, appear where you are not expected.

*Now the general who wins a battle makes many calculations in his temple before the battle is fought.
[Chang Yu tells us that in ancient times it was customary for a temple to be set apart for the use of a general who was about to take the field, in order that he might there elaborate his plan of campaign.]

The general who loses a battle makes but few calculations beforehand.


- Sun Tsu.


Ukiwa unasoma historia inamaana kwa kiwango kikubwa unasoma mambo ambayo hayakuandikwa na mtu mweusi. Huhitaji kuwa mtu mwenye akili nyingi kugundua kuwa hili ni tatizo kubwa. Asilimia kubwa ya historia imeandikwa na watu ambao hawakumjua mtu mweusi. Baadhi yao walikuwa wanamuogopa mtu mweusi,wapo ambao walimuona kama ni chombo cha kufanyisha kazi, wengine walikuwa wanamchukia na bila kusahau waliokuwa wanampenda, lakini si kwa kumlinganisha na wao bali kwa kumuona ni kiumbe kifurahishacho macho na pengine kinogacho katika maswala ya uroda. Hatuwezi kuwasahau pia waandishi ambao waliandika kuhusu watu weusi kwa ajili ya serikali zao ilikuhalalisha mtazamo wa serikali zao na watu wao ilikumdhalilisha mtu mweusi.

Watu weusi ambao asilimia kubwa wanatokea Afrika tulitumia sana masimulizi zaidi ya maandishi kujua historia zetu. Na baada ya mkoloni kuna asilimia kubwa tumeacha kabisa kufuatilia historia zetu kama mababu zetu walivyokuwa wakiijua. Tumechukua historia iliyoandikwa na watu wengine kama ndio ukweli mtupu kuhusu sisi.Pia kuna asilimia kubwa ya historia yetu imepotea kabisa!

Kumbuka sio muda mrefu dunia nzima ilikuwa iko katika usawa kitekinolojia na hata kiuchumi. Ukifuatilia utakuta kuwa Mtu mweusi alikuwa si mtu wa kudharaulika. Ningependa ukumbuke, katika dunia yenye teknolojia moja changa au isiyo na tekinolojia, ni mabavu tu yanayotumika kuishi. Bila kufikiria sana, tabaka la watu ambalo lingeweza na liliweza kuhimili kirahisi mazingira ni la watu weusi. Tuchukulie mifano ya leo hii katika dunia iliyotawaliwa na Televisheni za Marekani. Bado michezo yote ya nguvu inatawaliwa na watu weusi.Kuanzia Futiboli ya kimarekani, Baseball, basketball,riadha nk. Ukirudi nyuma ndio kabisa, watumwa weusi walitumika zaidi kwa sababu ndio waliokuwa wakihimili zaidi shuruba za nguvu.

Sasa kwa nini watu wenye nguvu wakawa watumwa? Kuna sababu nyingi lakini mimi nasisitizia hizi mbili. Nguvu za mtu mweusi ndio zilizomletea unyonge mtu mweusi. Kwa kuwa na maguvu akachelewa kurahisisha vyombo vya kazi na pia silaha. Hii ikamsababishia kushindwa waliporudi watu wengine na silaha zilizo bora zaidi. Pili , hatukumjua adui na pia hatukujijua kuwa nguvu za misuli yetu zimepitwa na wakati.

Matokeo yake ni sasa mtu mweusi anaangaliwa kama mtu wa chini na jamii zote nyingine. Hii namaanisha Wazungu, Waasia wa jamii ya kichina, kihindi,waarabu na wengine wote. Sasa hivi wenye nguvu ni wao, hivyo kumbuka wakati sisi tunanguvu walifanikiwa kutupindua.Je unafikiri sisi tutashindwa kupindua meza? Haina haja ya kufanya kama wao . Lakini naamini kabisa tunauwezo wakulinganisha mambo.Si lazima tuwapindue, haiko katika silika ya mtu mweusi kwa mtazamo wangu.


Hapo ndipo tunapokuja kwa SUN TSU. Kitabu chake nilikipenda ningependelea ukisome kitabu chenyewe.Lakini hapa naweka kongoli upitie baadhi ya tafsiri ya kitabu hiki kwa kiingereza. Huyu mchina aliandika kitabu hiki muda mrefu sana kabla ya Yesu kuhusu vita. Kwa mtazamo wangu watu wote weusi tuko vitani kumkomboa mtu mweusi. Na kama ni vita basi lazima kuwe na mipangilio ya vita(Strategies).
Jambo la kwanza inabidi tuwajue hawa watu wa utaifa (race) mwingine.Ikibidi kila kitu juu yao kama inawezekana. Kongoli hapa The art of War kilicho andikwa na SUN TZU (Ingawa kuna baadhi ya wasomi wanahisi sio yeye aliyeandiaka). Some ukiweka mtu mweusi katika fikra zako.
Katika kitabu hiki jambo ambalo narudia kusema kuwa linanigusa sana ni umuhimu wa kumjua unayepigana naye na pia umuhimu wa kujijua mwenyewe. Ingawa kitabu hiki kimeandikwa miaka zaidi ya efu mbili iliyopita kinauwezo wa kumkomboa mtu mweusi leo hii. Kuna maswali ninayo jiuliza kila siku. Je sisi watu weusi tunajijua? Je tuna wajua hawa watu wenye utaifa (race) nyingine?

Hili si jambo la kivita tu. Usipo wajua hata mahusiano yako ya kimapenzi nao hayawezekani. Usipojijua hukawii kujikuta unatumika kisawasawa bila kujua , kwa maana nyingine unarudi Utumwani.


HEBU TUANGALIE WATU WEUSI TUMEFIKIA WAPI LEO:

1. Asilimia kubwa ya Wasomali(atleast in Scandinavia) hawakubali kuwa ni Waafrika weusi bali wao ni Waarabu.(Sisemi kuwa ni kila mtu katika kundi hili ila asilimia kubwa)

2. Waafrika weupe weupe kidogo kama Waithiopia na WaEritrea wengi niliokutana nao wanaamini wao ni Babu kubwa(Superior) kuliko Waafrika wengine weusi. Hii ni pamoja na Wasomali ambao walikuwa wana waonea Wasomali wenzao Wabantu. (Sisemi ni kila mtu katika kundi hili ila asilimia kubwa)

3. Tiger Woods hujaribu sana kujieleza kukwepa asilimia ya Uafrika aliyonayo.

4. Condoleezza Rice na Colin Powell wako kwenye timu ya George Bush.

5. Barry Bond achukiwa Marekani kwa kufikia rekodi ya Baby Ruth (mzungu) kwenye baseball.
6. Obasanjo alitaka kuendelea kutawala kwa muda wa tatu mfululizo.

7. Raisi Jakaya Kikwete asifiwa kwa jinsi aonyeshavyo maringo yake -dingili dingili mpaka chini.

8.Jacob Zuma ala uroda bila soksi na mtoto mwenye vijidudu vya UKIMWI
9.Tanzania bado hatuna uhakika na uwezo wakujilisha.
10. India, kwa weusi wa tabaka la chini hata kujulikana kisheria hawajulikani kama wapo.
11.Manyota wa hiphop kama akina P.Diddy wanaweza wakarekodi video wakiwa na wanawake weupe walioko nusu Uchi bila kunyongwa(Lynched) na Wazungu.

12.Asilimia kubwa ya watu weusi ndio walioathiriwa na vijidudu vya UKIMWI.(Ingawa hii inaweza ikawa ni porojo kutoka kwenye vyombo vya Uongo)

13.Simon Kitururu bado anaishi ulaya ambako Wazungu wenye msimamo mkali wameanza kuzidi kuongeza makali yao katika kuwashambulia watu weusi.

14.Bado Waafrika kibao tuna zama baharini tukijaribu kuzamia Uspaini kutokea Senegal na sehemu nyingine za Afrika Magharibi.

15.Oprah mwanamama mweusi atajirika kwa kuendesha shoo ipendwayo na akina mama weupe watu wazima Marekani

16..............

JE WATU WEUSI TUNAJIJUA? JE TUNAFANYA NINI?

Read more...

NI NINI SILIKA YA TANZANIA?

>> Monday, May 22, 2006




Nimejaribu kutafsiri kichwa cha habari hapo juu kutoka kwa Kiingereza.'What is Tanzanian National Character?'. Nimependa kuingiza kiingereza chake kuonyesha ni jinsi gani lugha za watu zinavyoathiri hasa ukizitumia kusoma kwa muda murefu. Unaanza kujikuta unababaika kupata maneno ya lugha yako ya asili. Narudi kwenye hoja.

Tanzania tunapenda kuamini kuwa kunakitu kimoja kinachotuuunganisha, nacho ni Utanzania. Lakini kuna mambo mengi tu ambayo yanafanya Watanzania wawe na majibu tofauti waulizwapo kuhusu Tanzania na Utanzania. Kuna maswali mengi Waislamu na Wakristo hutofautiana majibu, Wasomi wa shule za vitabu na wale wa shule za kitamaduni hutofautiana majibu. Wanawake na wanaume hutofautiana majibu, Wazanzibar na Watanganyika hutofautiana majibu, pia watu wa makabila tofauti hutofautiana majibu.

Katika safari zangu Ughaibuni na hata bongo ni mara nyingi nimejikuta na jizuia tu kuingilia hoja kutokana na kusikia mtu akielezea Tanzania na Utanzania tofauti na ninavyouelewa mimi. Mara nyingine nimejikuta na mtambulisha mtu kuwa ni Mtanzania, halafu yeye akakataa nakusema yeye ni Mzanzibari. Pale Zanzibar pia nisha kuwa naongelea kuhusu sisi Waafrika nikakanwa na mtu tuliye fanana naye akiniambia yeye ni Mpersia. Siku nyingine nilikuwa na ongelea usawa Tanzania nikajikuta naambiwa Waislamu bongo hawajapewa usawa kielimu. Nika ongelea jinsi Watanzania walivyozoea kuwa na viongozi wa kike tofauti na nchi nyingine za kiafrika. Nikichukulia data za Wanasiasa wanawake ambao wako katika serikali, nikaambiwa wale nimapambo tu hawana nguvu. Kitu kibaya tu ni kwamba maswali kama haya mara nyingi yanazuka muulizaji akiwa ni wakutoka nchi za kigeni. Halafu kuna kile kitu ambacho sikipendi ambacho hujitokeza. Dalili ya kwamba tunapingana. Ingawaje nawezakusema sisi tuna nafuu katika Afrika Mashariki ,ukilinganisha na Kenya na Uganda, lakini hili swala bado ni la kutupia jicho.

Sasa Je ni nini maana ya Utanzania kama tunauelewa tofauti tofauti namana hii. Mimi nafikiria kuna mambo yafuatayo ambayo yanaweza kufungua macho kwa nini Watanzani pamoja na Utanzania wetu , mara nyingi hatuna majibu sawa. Kwa mtazamo wangu hizi ni baadhi za elementi zinazochangia silika ya Mtanzania, na pia kuwepo kwa majibu tofauti tofauti mengi. Ningependa kupata nyongeza kwa wanamagazeti wa Mtando.

1.Watanzania wako ororo (sensitive) na swala la Utaifa. Hili linatokana na historia ya kutawaliwa na pia Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao mpaka leo unamushkeli. Kazi ya kujenga identiti ya Mtanzania haijafikia upevu.


Picha kwa hisani yaISSA MICHUZI
Usingeweza kujua kua tokea siku hii ya muungano pichani mpaka leo swala la muungano bado linamushkeli.



2.Watanzania ni watu wenye vichwa ngumu kisirisiri.(passively stubborn people). Mpaka leo ni rahisi sana watu kudindisha kufanya jambo ili tu kupruvu jambo. Bado maoni ya wakoloni yana nguvu katika mawazo ya Watanzania.Kuna mawili yanaweza yakatokea, kukubali kirahisi kwasababu Taifa linalosema limeendelea au kudindisha bila ya sababu maalumu. Yote haya huweza kutokea bila ya mtu kukuambia usoni. Bosi Mkaburu anaweza akadindishiwa hata kama anasema ukweli ili tu kumwonyeshea hapa sio Zimbabwe. Maoni kwa wawekezaji- epuka kuweka mazingira ya kazi yako kutoa picha ya Mnyampara na Mtumwa.Kwa Watanzania utashindwa wewe.

3.Watanzania ni watu wanaoathirika na dini sana. Mtu hata kama sio Mkristo au muislamu , kuna kitu tu kina muathiri kiimani. Lazima kuna imani fulani anaifuata na ambayo ina mambo yanayomtisha. Kwa Wakrristo na Waislamu ni jehanamu , lakini kwa wengine wote kuna kakitu tu katakacho kueleza ebwana msitu huu usiingie usiku au du ukifanya hivyo, jasho litakutoka nk. Halafu katika Waislamu na wakristo bado kuna katatizo au kamvutano ambako kako kwa chinichini. Kwa mtazamo wangu bado waislamu wengi bado huamini kuwa Wakristo hufaidika zaidi na Serikali. Na Wakristo wengi huona waislamu kama hawachuki muda kurizoni baadhi ya mambo kabla ya kuchukua hatua.

4.Watanzannia kwa ujumla wanapenda siasa. Siasa tokea kabla ya uhuru imechangia kujenga silika ya Watanzania. Lakini Siasa za Nyerere za chama kimoja bado zihazijaweza kuwatoka watu akilini. Uzuri wa siasa za Nyerere zimekuza umoja wa Watanzania. Lakini kuna uwezekano wakuvunja umoja bado hasa kupitia mambo ya husuyo dini. Siasa ya vyama vingi bado ni changa sana kuonyesha makucha yake bado.

5.Asilimia kubwa ya Watanzania hawajaelimika vya kutosha. Hii husababishwa na mfumo wa elimu ambao bado umeshindwa kumkomboa Mtanzania kutoka katika utumwa wa kifikira na pia kushindwa kumuwezesha Mtanzania kujikomboa kiuchumi hata pia kiafya.

6.Tanzannia ni bado ni nchi yenye ukabila.(Tribal Nation). Bado ukabila umeshikilia mambo mengi. Kuna baadhi ya makabila bado yananufaika zaidi ya mengine, kielimu ,kiuchumi, nk. Kuna sababu nyingi kweneye hili. Kuna maswala ya idadi ya watu kwenye kabila,mahala lilipo kabila,udini, elimu , nk.

7. Kiswahili ni Jambo moja ambalo linaunganisha Watanzania. Katika Jambo moja ambalo Watanzania huwa na jibu moja ni katika umuhimu wa Kiswahili Tanzania. Lakini kiswahili kinakuwa butu kwa wasomi wengi kutokana na kutotumika sana katika elimu ya juu. Hivyo asilimia kubwa ya wasomi hawana maneno ya kiswahili ya kuyatumia kuelezea taaluma zao.

8. Kwa mtazamo wangu watanzania ni watu wachapakazi lakini ni watu wafanyao kazi polepole.



Ongezeeni au kosoeni wana mtandao.........................

Read more...

MAHUSIANO YA UBINADAMU NA NGONO

>> Thursday, May 18, 2006

Niliposoma jinsi Mzee Zuma pale mahakamani Afrika Kusini alivyojitetea nilichoka mwenyewe. Maana mzee mzima akanitolea kuwa baada ya kupata uroda na mwanadada mwenye virusi alioga kupunguza bahati nasibu ya kupata bingo ya ukimwi.nimejiuliza maswala mengi tokea kipindi hicho. Sentensi hiyo iliniwezesha kupata majibu mengi kuhusu Zuma hata bila ya kusoma historia yake. Miongoni mwa mengi ilinifanya nionekuwa hasingenifaa kuwa Raisi wangu. Nilipozidi kuangalia habari za Afrika kusini nikakuta kuwa huyu bwana bado anaendelea kuwa na mashabiki wengi sana wanaomfuata. Kwanza nikaanza kuhisi kuwa labda ni kwasababu ya ukabila. Nikaanza kuamini kuwa Wazulu wengi wanategemea kuwa yeye ndio atakaye wawakilisha katika makorido ya nguvu za kiserikali pale Serikalini. Inawezekana kunaukweli katika hilo, lakini bado kuna kitu kingine kikaanza kunikera. Nikajiuliza, hivi katika maisha yangu ni watu wangapi ambao najuananao ambao wanajua madhara ya ukimwi lakini huwabado siku ya siku wanasema potelea mbali ajali kazini? Je hakuna ka ukweli kuwa kama ni kweli Zuma anavyosema, watu kibao wakipewa majaribu mitaa ya chumbani wanaweza kufikia hatua yakusema potelea mbali liwalo na liwe. Maana Zuma anadai kuwa yule kidosho alikuwa anamwonyeshea maringo yake dingilidingiri katika anga nyeti. Mimi nianaamini kuna kaudhaifu katika binadamu na maswala haya ya ngono. Bill Clinton alipogundulika kamchezo kake anakofanya ofisini, mshauri wake wakidini Bill Graham akasema , ebwanaee viumbe viwili , cha kike na kiume ambavyo havina hitilafu kama inawezekana visiwe ndani ya chumba wakiwa pekee. Inasemekana kila binadamu ana siku yake ya udhaifu na mtu wake anayeweza kumdhaifisha akibonyeza vifumgo muhimu basi baadhi ya topiki za baolojia zinaweza kufanyiwa eksiperimenti. Kinachotisha ni kama Raisi Mwinyi alivyosema, haka kaugonjwa kamekalia mahala pabaya au alisema mahali patamu hata sikumbuki vizuri.

Hili jambo limenifikirisha sana. Nikaanza kuangania nijinsi gani ngono inavyopendwa na binaadamu. Na je bianaadamu nimjinga kiasi gani kuweza kuchezea moto kila siku hata akijua kuwa moto unaunguza. Kusema ukweli kutokana na mashuhudio yangu, Zuma anachekesha na kusikitisha kutokana na wadhifa wake ,lakini hayuko peke yake. Kunakaudhaifu sana katika swala hili la ngono. Nirahisi kusikia du , nisingempata leo ndio ingetoka hiyo, hivyo ilibidi tu nifanye. Halafu bado utasikia lakini umemchemki mtoto mwenyewe , yule haiwezekani akawanao.......Hizi si kauli anazoongea mtu asiyejua madhara, bali mtu mwenye elimu ya madhara yaletwayo na ngono kabisa.Haya yanaweza kuwani mawazo yanayozunguka katika vichwa vya wengi tu. Mimi siwezi kujitoa katika haka kakona kaubinadamu. Lakini ningependa tujiulize sana wakati mwingine je kwa sababu sisi ni binadamu ni haki yetu kuanguka katika huu mvutano wa taamaa za mwili na chaguo la busara?

Kuhusu swala la Zuma tunaweza tukaliacha likawa ni siasa za Afrika kusini. Tunawezakulichukulia kuwa ni udhaifu wa mwanamume mweusi. Maana kuna baadhi ya watu weupe wenye siasa kali wanaodai kuwa katika baadhi ya mambo ambayo mwanaume mweusi hana breki nayo hili la ngono ni mojawapo. Au tunaweza kujiuliza katika maisha yetu wenyewe tunajifunza nini kutokana na tukio. Kila mtu atakuwa najibulake . Wenye kutaka kuishi muda mrefu, lao na wale wanaoishi kila siku kama ndio mwisho wa dunia, lao. Jawabu ulipatalo jaribu kuangalia litawaathiri vipi watu wa karibu yako. Ikibidi jiandae kwa hilo pia. Maana huwezikujua, baadhi ya watu washamaliza mambo yote yanayoleta maana katika maisha yao hapa duniani.

Ndio matamanio ya ngono ni jambo ambalo halikwepeki kwa kiumbe asiye na kasoro .Hii ndio njia inayotufanya binaadamu tuwepo duniani mpaka leo hii. Labda ni kweli kuwa katika kila janga wapo wale watakao shinda majanga na kuendelea kuishi. Lakini je katika hao watao kuwemo katika kikundi cha survivor of the fittest na sisi tutakuwepo?Du ngoja nikaoge! Sijafanya Zuma staili lakini, nimetoka mazoezini:-)

Read more...

KWENDA SHULE SI KUELIMIKA

>> Wednesday, May 17, 2006

Mpaka itakapofikia kuwa mfumo wa elimu wa Tanzania unaomwezesha Mtanzania kuweza kusoma na kuandika utakapomwezesha kuelimika ndio maendeleo ya Mtanzania yatakapo kamilika. Mtanzania akielimika Tanzania tulivyozungukwa ma Maziwa na mito hatutakufa njaa.Misri inakatizwa na mto mmoja tu na hawafi njaa. Watanzania tukielimika usindikaji wa mazao utaboreshwa, kwani tokea mababu walifanyahivyo. Lakini Watanzania si tunaenda shule?
Okei, nawezakukubali si wote wanaenda shule, lakini je wanaoenda shule wanaelimika?

Ninaamini kuwa mfumo wetu wa elimu Tanzania ambao mpaka sasa hivi haujafanikiwa kumwezesha kila Mtanzania kusoma na kuandika bado unachangia kuwafanya watu walioenda shule wasiweze kuelimika. Mfumo wetu waelimu unamfanya mwanafunzi kusomea mitihani. Nakumbuka Kutokea shule ya msingi mpaka kidato cha sita Bongo nilikuwa miongoni mwa kundi la wanafunzi ambao cha msingi ilikuwa ni kuhakikisha unafaulu bila hata kuwa na uhakika na mambo unayosoma. Na nina mifano mingi inayonizihirishia kuwa sisi hatuwa peke yetu. Tulikuwatunasomea mitihani. Unakuta mtu ana maswali na majibu ya mitihani ya miaka mpaka ishiri iliyopita. Halafu si ajabu ukifungua kitabu ukisoma, mshikaji akatokea akuulize, je unajua sehemu hiyo haitoi maswali kwenye mtihani? Basi hapo ndio inakuwa mwisho wa kuendeleza kuusoma ukurasa ua hata topiki hiyo. Unajikuta kila siku unasoma lakini hauoni hata maana ya baadhi ya mambo unayosoma yanavyoweza kukusaidia maishani. Matokeo yake hata kuchagua nini cha kusoma unategemea na ninini unasikia kitakupeleka kwenye kazi inayolipa. Utasikia chukua PCB hapana chukua PCM unajua ndio yenyewe. Mwingine anakuja kukuambia unajua viongozi kama akina Nyerere walisoma Arts na ndio hata akina Prinsi Wiliamu kule Wingereza ndio wanachukua masomo kama hayo, basi ilimradi tu mtu unajikuta unahangaika kuchagua. Chakujiuliza ni kwamba kwanini mfumo wetu wa elimu hautujengi kujiamini kusoma kile mtu akipendacho kutoka moyoni bila ya kutishika kuwa du , nikisoma hiki nawezakujikuta niko hatarini? Ndio tumekopa mifumo ya kigeni ilikujenga mfumo wetu wa elimu, lakini utasikia Uingereza ambako bado hawajaridhika na mfumo wao wanajadili kuubadili. Utagundua Wajerumani , Wamarekani, Waskandinavia, Wajapani ...nk wote ambao tunaweza kusema mifumo yao ya elimu iliwanufaisha ilitengenezwa kukidhi mahitaji yao. Je mfumo wetu wa elimu Tanzania unakidhi mahitaji ya kiellimu ya Mtanzania?

Mfumo ambao unashindwa kumwezesha mwanafunzi wa kiTanzania kujitegeme akimaliza shule, unaoshindwa kumwezesha Mtazania kujua haki zake na kumfanya mwanafunzi kupasi mitihani kwa kukariri, kwa mtazamo wangu unakasoro. Mfumo wa elimu ambao unatuacha kila mwaka kushindwa kutatua matatizo yajulikanayo mwaka nendarudi unamatatizo.

Kama elimu inapanua mtu mawazo basi elimu hii ifikie kutuwezesha sisi Watanzania kupanuka mawazo na kuweza kutatua matatizo yetu. Huko ulaya kwenye baridi waliweza kugundua vipashajoto nyumba, kwenye sehemu ambazo wanahali ya hewa inayowezesha kilimo kwa muda mchache waliweza kujaribu kulima kwa muda huo mchache( Ingawa kunaukweli kuwa mazao mengi wanayatoa nchi za dunia ya tisa). Sisi Tanzania bado hatujaweza kukuza tamaduni zetu za kuhifadhi mazao ingawaje tunajua tokea mababu walikuwa wanafanya hivyo. Utasikia bado upande mmoja wa Tanzania kunanjaa halafu upande mwingine chakula kinaoza. Elimu yetu basi au mfumo wa elimu wetu ukazie maswala haya. Kila mwaka sasa unasikia tuna upungufu wa vyakula. Je kuna utafiti wowote unaondelea wakukuza hata njia za kijadi za kusindika mazao? Haiwezekani ikawa kila mwaka tunakumbwa na tatizo hilo hilo. Hivi zile nyama za kukausha, viazi, mihogo ya kukausha inakwenda wapi? Hivi mbona ni zamani wavuvi waligundua kutumia chumvi kuhifadhi samaki sasa hivi zile akili zilizowafikisha kwenye hatua hiyo haziwezi kupewa changa moto tutuvuta mpaka katika kutatua matatizo ya sasa?

Halafu utashangaa nchi kavu kama Misri inayo pata maji kutoka mto Nile unaotokea kwetu hausikii wakilalamika njaa. Sisi Waafrika tunaotokea sehemu yenye maziwa makubwa Afrika tunakufa njaa. Sasa elimu hii tunayopewa kweli inatupeleka wapi ikiwa hata matatizo ya kila siku haitujengi kuyatatua? Utashangaa nchi nyingi za magharibi zina kijisehemu katika vyuo vikubwa kinachoshughulikia kutusoma sisi waafrika. Hutakawia kukuta kuna researcher aliyekubuhu kwa maswala ya siasa au kilimo cha Tanzania aliye Muingereza ,Uingereza. Tukikumbwa na njaa anaitwa BBC kuelezea matatizo yetu! Wanafanya hivyo sio kijinga tu, ili kuhakikisha wanatujua. Sasa Kama elimu yetu haitufanyi hata kuwajua hao watu wa nchi za nje na mazingaombo yao, basi si itufanye tujijue wenyewe na ituwezeshe kujitatulia matatizo yetu ? Siongei hapa kutaka kusema kuwa Tanzania ijitenge, ila ningependa elimu yetu ituelimishe basi. Maana kwa sasa inatufanya tuwe katika hali vuguvugu, nikimaanisha haituwezeshi kujijua ilikutatua matatizo yetu wenyewe na pia naona haijatuwezesha kushindana na mataifa mengine. Hata kidini vuguvugu si sehemu nzuri kubobea kwa muda mrefu. Ni heri Uwe joto au baridi ililijulikane moja.

Ningependa mfumo wetu wa elimu tuuangalie tena. Ninaamini elimu haina mwisho,vilevile elimu inaotakutu kama haipigwi msasa. Hivyo hata walienda shule na kuelimika ni lazima kupiga msasa elimu hiyo kwa maana baada ya muda inaweza kugeuka kuwa zilipendwa. Usitupe vile vitabu baada ya kumaliza kozi:-)

Read more...

Dhamira ya Mtanzania Je Itafufuka?

Mimi siwezi kujiita mwanadini niliye kubuhu wala Mtanzania bora. Lakini katika kukua kwangu pale Tanzania nimeshuhudia jinsi gani Mtanzania alivyowezakubadilika tokea yule ambaye kuvunja sheria ilikuwa ni aibu mpaka yule ambaye imekuwa ni ujanja.

Kama mtu niliyekulia katika maadili ya kidini ni vigumu kuyakwepa maadili haya katika kuongelea swala hili, ingawa naamini mfano huu unaweza kutumika bila ya kunukuu dini yoyote . Katika maisha yangu nimefikia hitimisho kuwa kila siku unapoendelea kurudia kutenda tendo livunjalo maadili ya dini ndio jinsi moyo na ubongo unavyozidi kulitambua nakulipa uhadhi wa ukawaida au kulihalalisha. Kitendo cha ndoa nje ya ndoa kwa wanadini nijambo ambalo linatisha katika hatua za mwanzoni mpaka kinapozoeleka mpaka hata kile kijisauti cha pili(dhamira) kinachoingilia kutaka kukatisha maamuzi, kwa kumtaka mtu afikirie kwanza busara ya kuendelea na shughuli za uroda nje ya ndoa kinapokufa kabisa. Pale kile kijisauti kinapokufa basi mtu hasiti tena. Kila nafasi inapotokea maswala yote ruksa.

Dini inawezaikawa ni mfumo wowote ambao unamjengea mipaka mhusika katika kuonyesha ninini sahihi na nilipi potofu. Lakini dini ninayoiongelea hapa ni ile ambayo mwanadamu yeyote anakuwanayo ikilindwa na dhamira binafsi.

Tukiangalia kuanzia maswala ya rushwa mpaka uzembe kazini, utaonakuwa kuna wakati ilikuwa sio ujanja kufanya hivyo. Enzi za mababu zetu ilikuwa ukiwa mzembe kama ni mwanamume, hata mke inakuwa vigumu kupata. Kwa akina dada unaonekana unatabia mbaya hivyo sio mwanamke nona kwa ndoa. Sasa utashangaa imefikia wakati ambao ujanja ni kuwa laini au kulia ofisini. Ukiwa katika ofisi ambayo watu wanajua utaweza kirahisi kuiba fedha utasikia watu washaanza kusema naona uko jikoni, usipojenga wewe basi mjinga. Unakuta jamii nzima inategemea kuwa sasa utaonyesha mambo- maana uko jikoni. Na kuua dhamira au kile kijisauti haitakuchukua muda.

Sababu ziko nyingi ambazo zinabeba lawama yakuwa ni chanzo cha yote haya. Hali ngumu ya maisha, mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yameleta upungufu wa chakula, maswala ya ukiritimba katika mfumo mzima wa serikali na vikorokocho vyake nk. Jambo lakujiuliza ni kwamba je dhamira ya Mtanzania inawezakufufuliwa? Mara nyingi nirahisi kuwa tuna laumu tu bila ya kujaribu kupata majawabu ya matatizo yetu. Sheria pekee haiwezi kusawazisha mambo kama akilini mwa wananchi hakuna kijisauti kinacho wasuta kuwa wafanyalo si ujanja na si jambo lakujivunia. Mimi nafikiria kuwa Watanzania turudie kule tulikotokea , mafunzo ya maadili mema yapewe kipaumbele tokea shule ya vijidudu. Hata Propaganda za zamani zirudishwe.Mkabaila tulimuimba na hata yule Mnyampara. Propaganda za maadili mema zianzishwe tokea shule za vidudu tena. Nakumbuka niliimba kuhusu kaburu na ubaguzi wa rangi mbaya na nikamchukia kaburu tokea shule ya vidudu bila ya kujua ubaguzi wa rangi ni nini. Iliwezekana miaka hiyo itawezekana tena naamini.

Propaganda za kumwezesha Mtanzania kujiamini tena kuwa maisha yanawezekana kihalali ianzishwe tena. Mtanzania wa leo siye yule aliyekuwa anajiamini. Mtanzania wa leo anatakiwa ajiamini kuwa kuna mambo mengi tunaweza wenyewe. Kumbuka wenzetu kutokana na matatizo ndio wanapata ujasiri wakutatua matatizo. Angalia Brazili matatizo ya petroli wameyatatua kwa kuzalisha miwa anakutengeneza ethanol.

Nafikiri Tanzania ilikuwezesha kurudisha imani na Utanzania inabidi tujenge utamaduni wa kuwaenzi Watanzania mahiri na pia kujaribu kuwasaidia wale wanaoonyesha dalili za umahiri. Sioni sababu kwanini vyuo vyetu vikuu haviendeshi stadi za kuboresha mambo yajitokezayo nchini ambayo yakiboreshwa yanakuwa ni bora na ya Kitanazania. Sidhani kama kuna hata mkufunzi mmoja anaye wasoma mama ntilie kwa nia ya kuwawezesha kuboresha bidhaa zao zifikie katika hatua ya mbele. Sido haikuwasaidia akina mchaga kajitaihidi .Hivyo hata siku moja yule fundi viatu hakuweza kupiga hatua kuenda mbele.

Tunabidi tuwaenzi watu wanaoishi kihalali na wanaochangia maswala ya Taifa na kuletea sifa nzuri Taifa. Ningefurahi ikiwa tunaweza hata kuwaenzi watu hawa hata kwa ma sanamu na mapiramidi ikiwezekana. Na wale ambao wanavunja sheria hasa kwa kujinufaisha wao wenyewe wahadhirike mpaka wasiwe watu wa kuigwa. Serikali ni wananchi hivyo wananchi inabidi wajisikie kuwa wako pamoja na serikali yao na sio ukimuona polisi hata kama huna kosa unaanza kujihami. Kwa maswala ya polisi mimi na husudu mapolisi wa Skandinavia kwa jinsi wanavyohudumia watu wao. Tokea shule ya vidudu huwa wanatembelea kuelezea ni nini wanafanya. Ni wale watu ambao wagonjwa mpaka walevi waliozidiwa wanapata msaada wao.Ukizidiwa ulevi Unawezwa kupelekwa na nyumbani kama hawako na shughuli nyingi.Nakumbuka bongo mara nyingine hata rafiki yako akiwa polisi unaadha kujihami asije akakufanyia vibaya. Sasa katika kipindi ambacho Kikwete anasema kana kwamba analeta ari mpya basi tufufue na kadhamira ka zamani.

Read more...

Kuchekelea Wazungu !

Kwa muda mrefu sasa nimekutana na maswala yanayo nifanya nijiulize mambo mengi kuhusu ukarimu wa kibongo.Kuna wakati napigwa na butwaa hata pia kukerwa na ukarimu huu. Nazungumzia ukarimu uliojengeka sasa , ukarimu wenye masharti.Kunawakati ukarimu huu unanisababisha niamini kuwa, sisi wabongo tulitawaliwa na hawa wageni kutoka nchi za nje kutokana na ukarimu huu.Wabongo kwa kirahisi kabisa wanaweza kukuruka katika huduma ili wamuhudumie Mzungu. Nakubali kwamba ukarimu ni kitu kizuri, lakini naona huu ukarimu mara nyingine umekuwa unavuka mipaka, hasa ukiwa unapendelea baadhi ya watu katika matukio maishani. Kama sisi wabongo ni wakarimu kwa nini tusiwe wakarimu kwa kila mtu sawasawa, bila ya kujali anatokea wapi? Nakumbuka ukarimu wapewao watoto wamjini waingiapo kijijini unavyowaponza wanavijiji.Unakuta watokao mjini wanajaliwa zaidi mpaka katika maswala ya kujamiiana kitu ambacho kimesaidia kueneza ukimwi kutoka mijini kwenda vijijini bongo.Huu ndio ukarimu ninaouita wakuchekelea wazungu. Mara nyingi sana nimeshuhudia ukarimu huu ukiwezesha watu kujali watu wa mataifa mengine zaidi ya wabongo wenzao.Chakusikitisha ni kwamba tabia hii imejipenyeza mpaka katika serikali yetu. Angalia katika ubinafsishaji, wawekezaji wa nje hupewa ukarimu wa hali ya juu, hata pasipo sababu maalumu. Ukienda mahotelini ikatokea kuna wageni wa mataifa mengine wako hapo,mara nyingi, watapewa huduma kwanza kabla ya wabongo hata kama wabongo wamewahi na wanalipa vilevile.Huku magharibi ukiienda katika balozi za Tanzania, utakuta vilevile unaweza ukarukwa kwasababu kuna watu wa mataifa mengine walioko humo.Katika nchi kadhaa nilizo wahikutembelea za hawa Wazungu, kwa mfano, Finland, kuna kitu kimoja ninawasifu. Hata iweje huangalia matakwa na faida ya Wafini kwanza.Nchi ndogo kama Estonia, katika balozi zao , Muistonia kwanza ndio jina la mchezo. Lakini sisi wabongo jasho litakutoka.Rafiki yangu aliibiwa kila kitu Johanesburg ,Afrika Kusini, akaenda Ubalozini iliapate kibali cha muda ,ushauri au pasipoti ya muda, jasho lilimtoka.Ndio kwanza utafikiri kajipeleka motoni. Rafiki yangu mwingine ikamtokea Sweden ndio kwanza ubalozini walimshambulia kauza pasipoti.Cha ajabu wageni hawa tunao wajali Tanzania labda hawana kumbukumbu maana ukija kwao utashangaa mwenyewe jinsi wasivyokukukarimu . Mara nyingi ni mpaka wajue kunakitu watapata kutoka kwako ndio utakapo ona ukarimu wao.Lakini ,muda wote utajikuta unaonekana kuwa ni tatizo tu.Na mifumo yao yakuendesha nchi hujengwa kuzingatia zaidi wazawa nasio wageni.Wananchi wa nchi nyingi za Ulaya wanapenda kukukarimu kwa kukuuliza maswali haya: Umetokea wapi? Unafanya nini?Lini utaongoka?Ila wenzetu wanapenda nchi zao na wanajua jinsi ya kuzipanguvu nchi zao. Wananchi wa Finland kwa namna yoyote ile hujaribu kuisaidia nchi yao,kwa mfano, hata nyanya na vitunguu ,kama vimezalishwa Finland vinapigwa bendera ya Finland. Hata kama ni ghali kuliko vyakutoka nchi nyingine ambavyo ndio halihalisi, watu hununua vya kutoka Finland kwanza.Wanafanya hivi wakijua kuwa wanawasaidia wakulima wa Kifini.Katika miziki, nenda urudi utakuta watu hujali kwanza wanamuziki wao kabla ya kuanza kununua miziki ya wengine. Sisi wabongo ni wakarimu sana kwa mambo ya wenzetu mpaka utaona tunapenda kuvaa bendera za mataifa mengine, na vitu vyetu vya bongo hasa kukiwa na uhakika vimezalishwa bongo, ndio kwanza tunavikimbia. Angalia mpaka kanga wavaazo akina dada zetu zikafikia kuzalishwa India na kusaidia kuua viwanda vyetu vya nguo bongo.Ukarimu huu wakutoangalia madhara tunayayotendea Taifa letu ufe.Lakini naona hatujifunzi! Sasa hivi tunawakarimu wawekezaji madini yetu ,uzalendo wetu.... nk. Je hii sio sababu ileile tuliwakarimu wakoloni nchi yetu?Sisemi kuwa ukarimu ni mbaya, lakini ukarimu mwingine ni ujinga.

Read more...

Idumu Jumuiya Ya Wanablogu Tanzania


Photo Sharing and Video Hosting at Photobucket

Partner

save mt. Kenya campaign
In partnership with africapoint.com

Taswira BANANGENGE

  © Blogger templates Romantico by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP