Mtakatifu SIMON KITURURU - MAWAZONI

FALSAFA na WAZO ndani ya neno - DUH!

PIKINIKI MAKABURINI! Je ukimchungulia mtu mzima Utapofuka macho?

>> Wednesday, November 15, 2006

Naamini mila na desturi zetu wabongo bado zina nguvu sana ingawa watu wanadai hizi ni zama ya bongo fleva. Naamini kuwa katika shule zetu za jadi mbinu mbalimbali zilitumika kuwezesha mambo fulani katika jamii kwenda shwari na kulindwa kwa nguvu zote na jamii. Mimi ni mchanganyiko wa Kipare na Kijita na katika makabila yote haya mawili njia za kuelimisha zilitumia mbinu nyingi ikiwa pia na vitisho. Mfano kwa Wapare maswala ya kufundishwa kuwa mwanamume wa shoka yaliendana na vitisho na maumivu. Kama wewe ni mwanamume basi lazima uweze kuvumilia maumivu .Nadhani kwa walioenda jando watakumbuka! Kulikuwa mpaka kuna simba wamsituni akumezaye ukishindwa kufanikisha mambo fulani ya kidume. Hii maana yake ulikuwa unauawa ingawa ilidaiwa umeliwa na Simba. Sasa njia hizi za kutufundisha heshima , maisha na hekima nyingine nyingi zikajakuuawa na wakoloni na wengine walioleta tamaduni mpya. Basi unaweza kudhani kwa sababu Wakoloni waliua shule za jadi basi na baadhi ya mambo tuliyokuwa tunatishiana yamekwisha!Utadhani mpaka sasa tumeweza kuelewa au hata kujiuliza ni kwanini mambo mengine yalitishalo kabila moja, hayalitishi jingine hata hivi sasa baada ya makabila ya Tanzania kuchanganyika na kutawanyika katika mikoa mbalimbali . Jibu bado tukopalepale. Tunaamini wachawi wanapaa na ungo ingawa hata kushuhudia hatuja shuhudia. Tunaamini kibibi fulani kichawi kwasababu macho yake mekundu bila kushuhudia aliyelogwa. Tuna chanja na kuvaa hirizi kibao bila ya uhakika hata wa ni nini hasa tunakiogopa.

Sitaki kukataa kuwa hakuna uchawi kwa sababu hili ni jambo lililorekodiwa miaka mingi tu na vitabu vingi vimelizungumzia. Lakini mimi ninachoamini ni kwamba uchawi mkubwa ni hofu ya kibinadamu itokanayo naupungufu wa kibinadamu wakutokujua. Na upungufu huu kwa bahati mbaya hauna dawa. Upungufu huu umefanya wengine waabudu miti ili kuujazia, wengine Yesu, na Wengine Mtume Mohamedi. Tatizo jingine la upungufu huu uko kama njaa, kila siku unahitaji kupewa chakula ilikujazilizia pengo la upungufu wa kibinadamu ilikupata uhaueni. Mimi naamini pamoja na kuwepo wachawi, moto wa ahera na mambo yote hayo, lakini upungufu wa kibinadamu wenyewe hulenga binadamu kitofauti kutokana na binadamu mwenyewe alivyo na mazingira yake katika kumuelekeza binadamu huyu kuamini nini kinampa ujazo na uhaueni. Basi utakuta huku wanaogopa makaburi, kule wanaogopa mbuyu na hata wengine kukimbia vifuu vya nazi kutokana na mazingira yao. Basi unaweza ukakuta kutokana na mlengwa hirizi ikajazia na kuziba hofu hiyo, dini au hata kujinyonga. Naamini ubongo wa binadamu unanguvu kiasi kwamba hufanyia kazi hofu za binadamu na kuzipa uhai na uhalisi.Na naamini asilimia kubwa ya wajulikanao kama wachawi, waganga wa kienyeji au hata uchawi wenyewe haukuthibitika ingawa una uhalisi. Halafu si kweli zote ni zakufundisha maana nyingine ni zakutishana kwa madhumuni yakutishana tu.Na nyingi za mila na desturi hizi hatakama zilikuwa zinafundisha zamani hazina mchango mkubwa sasa hivi katika kuifundisha jamii ya leo.Na kama kuna sababu zakuzikubali hizi dini za kuletwa moja ni kwamba kwa sasa ndio zimeshikilia ukanda katika kuipa jamii muelekeo, ingawa hata kwa hili sina uhakika zitaweza jukumu hili mpaka lini kama jamii haifumbui macho nakuelewa mchango wake bila ya kukariri na kufuata kiulimbukeni.

Lakini hizi mila za kutishana kwa dhumuni la kufundisha kitu haziko afrika pekee. Na rafiki yangu Myahudi alikuwa anatishwa na wazazi wake asiweke Tattoo kwa sababu hata weza kuzikwa kiyahudi akiwa na tattoo, kitu ambacho baadaye akagundua hakina ukweli. Nakumbuka pia nilipotembelea Russia mitaa ya Viborg nishawahi kuwatisha wenyeji wangu kwa kuwa nilipiga mluzi ndani ya nyumba na wao waliamini kabisa kwa kupiga mluzi ndani ya nyumba unaleta bomba la balaa. Kitu ambacho mimi siamini, kwani mimi nilifundishwa usipige miluzi porini. Hivyo hizi mila na desturi ambazo zina mambo haya ya kutishana haziko Afrika tu. Duh !Unakumbuka kitabu kiuzacho kuliko vyote siku hizi cha Harry Potter kinastori gani za kichawi?

Sasa ngojea nikupe stori fupi kuhusu uoga wangu wa makaburi.
Nakumbuka tokea utotoni nilizoea kusikia habari za kutisha kuhusu maeneo ya makaburini. Nakumbuka kunakipindi nilikuwa nang'ang'ania kutokwenda kulala mapema ilikuendelea kusikiliza stori za wakubwa, basi ilikutaka kunifanya niondoke wanaanza kusimulia stori za kutishatisha. Sehemu kubwa za stori hizi zilikuwa zinalenga maswala ya majini mashetanishetani na maeneo ya stori yanakuwa makaburini. Basi nisitake kukuongopea mara nyingi ilivyokuwa inaingia giza nilikuwa natishika kukatizia njia yoyote inayokatizia makaburini.Kilichokuja kunishinda ni pale nilipokuwa natembelea Upareni kwani kule ni kawaida kabisa marehemu kuzikwa katika eneo la nyumba. Sasa kutokana na kukulia mikoani ambako kunatamaduni za kuogopa maeneo ya makaruri ilinichukua muda kidogo kuzoe mpaka kuona ni kawaida.Kama nakumbuka vizuri Wachaga nao hawana uoga sana na makaburi hivyo nadhani kwa waogopa makaburi wanaweza kupata taabu sana uchagani na Upareni pia. Lakini akipata tabu Uchagani atatokwa na jasho akikatiza katika anga kama za Ufini ambako kuna mpaka siku katika mitaa ya krismasi ambapo makaburini ndio pakwenda sio kikilio bali kimatembezi.

Mila na desturi zetu nyingi ni nzuri lakini hatuzisomi na kuzielewa sasa hivi tunapo ingia katika tamaduni za bongo fleva. Tatizo linalojitokeza ni kwamba mila nyingi nzuri zitapotea, halafu na zipo mila na desturi nyingi zisizo na manufaa sana kwetu tutaendelea kuzitunza. Bahati mbaya mila ambazo zitatunzika ni zile tuziogopazo! Je ukimchungulia mtu mzima utapofuka macho?Je , utakwenda pikiniki makaburini?

6 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:

luihamu 7:13 am  

Kwa mtazamo wangu unawaza kwenda pikiniki makaburini,kwani wafu bado wako hai ingawa hatuwaoni.

luihamu 3:53 pm  

Mzee Simon,(mtani)
katika hiyo picha uko wapi kweli ughaibuni maajabu.

Simon Kitururu 4:06 pm  

Niko geto tu !Mbona sioni maajabu ya picha hii?

luihamu 6:03 pm  

Mzee Simon sio maajabu,bali napiga darubini katika maisha mazuri unayoishi,wengi wanatamani maisha kama hiyo picha lakini wapi,sisi tunaishai kwa nguvu za macho,tukipata mlo mmjo tunamshukuru mwenyezi mungu.Natamani niibadilishe Afrika watu wote wawe sawa katika kila kitutusiwe na daraja la kwanza,la pili na la tatu.nina lilia Afrika.

Anonymous 9:18 am  

Suala la utamaduni wa kutishana na utamaduni wa hofu ya tusiyojua:

Fanya jaribio hili. Ukikutana na watu wengi ukiwaambia kuwa huna dini na humwanini mungu, swali la kwanza wanalokuuliza ni: Je ukifa itakuwaje?

Hofu. Athari za vitisho. Vitisho vya motoni, n.k.

Kuna mahali umezungumzia kuhusu kuabudu miti. Suala la "kuabudu miti" mara nyingi linahitaji uchambuzi zaidi maana unaposema hivi watu wengi kinachowajia akilini ni imani za Waafrika. Kuna huu mtazamo maarufu kuwa Waafrika tunaabudu miti. Lakini ukichimba kwa undani theolojia ya imani za Afrika unakuta kuwa dhana ya kuwa tunaabudu miti ililetwa na wamisionari na wageni wengine ambao hawakuelewa mtazamo wetu kuhusu mazingira na vyote vilivyotuzunguka.

Na wakati mwingine msemo huu wa kuabudu miti hutumiwa kama namna nyingine ya kusema dini au imani za Waafrika jambo ambalo nadhani ni kurahisisha sana upembuzi wa imani zetu.

Simon Kitururu 11:21 pm  

Nakubaliana kabisa na kwamba mtazamo uliojengeka juu ya dini za Kiafrika umejengeka sana katika misingi iliyokuwa katika jicho la wamishenari ambao kwa mara nyingi walijaribu kupata majibu kirahisi rahisi. Lakini pia ukifuatilia dini zao za zamani kabla ya Ukristo kuingia ulaya wao ndio walikuwa wanaimani nyingi nyingi tu za ajabu labda hizi zili saidia kuwafanya wahisi wanajua nini kinaendelea hata walipofika Afrika. Lakini pia kuna ukweli kwamba dini nyingine zote zilikuwa ni tishio kwa dini zao walizo taka kuziingiza , hivyo ilikuwa muhimu kwao kuzijengea hoja mbovu.

Idumu Jumuiya Ya Wanablogu Tanzania


Photo Sharing and Video Hosting at Photobucket

Partner

save mt. Kenya campaign
In partnership with africapoint.com

Taswira BANANGENGE

  © Blogger templates Romantico by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP