Mtakatifu SIMON KITURURU - MAWAZONI

FALSAFA na WAZO ndani ya neno - DUH!

HAKI ZA TOTO LA KUKU WA KIENYEJI ZIKO WAPI?

>> Friday, September 14, 2007

Tukumbuke:

  • Nchi kibao ni kama kibanda cha kuku wa kienyeji. Mmiliki wake hahitaji kumlisha kuku mapumba, ili amfaidi kuku na mimba yake.

Ngoja tumfuatilie kuku wa kienyeji....


Kuku wakienyeji hujitegemea.
DUH!
Asubuhi huenda kujitafutia na usiku anarudi kufungiwa.


Swali:
Unafikiria ni kwanini kuku aliyehuru anarudi kibandani jioni mwenyewe kwa hiari yake?

Lakini.....

Tunachojua ni kwamba:
  • Jioni, kuku wa kienyeji hurudi kibandani.
  • Asubuhi ukisahau kumfungulia ,jogoo atawika kukukumbusha kuwa kumekucha ukafungue mlango wa kibanda.

Sasaaa.....

Naamini kuwa, kuku hurudi kibandani jioni kwa sababu hutambua kibanda kama nyumba yake.

Tatizo ni kwamba;
  • mwenye kibanda naye anatambua kuwa anamiliki pale aishipo kuku.
  • mwenye kibanda humuita kuku , KUKU WANGU.
  • mwenye kibanda huita matokeo ya mimba ya kuku, MAYAI YANGU.
Mitazamo ya mwenye kibanda na kuku aishiye kibandani inatofautiana sana kiasi kwamba unaweza hata usihisi wana migogoro.

Lakini....

Mitazamo ni kitu cha ajabu sana!
Kwa mtazamo wangu toto la kuku wa kizungu linalelewa kama yatima, bila wazazi.
Mtazamo mwingine unaweza kubobea kwenye jinsi toto la kuku wa kizungu liletewavyo misosi chumbani na kunenepeshwa haraka.

Swali:
Hivi kwanini lile kuku jingine linaitwa la kizungu?

DUH!

Kuku wa kienyeji ni kiboko!
Kwa kuhaha humuwezi.
Kwa utamu ni balaa.
Matokeo ya mimba yake (mayai) ni matamu , ukiyakaanga hata kuchemsha.
Yakitamiwa na kutotolewa, watoto wake kwenye bustani yako ya mbogamboga utakutana nao.

Kuku wakienyeji kakomaa, misuli kwenye vigimbi miguuni utashuhudia kutokana na mahangaiko ya siku nzima chini ya jua kali.
Kuku wakienyeji huchuma halali kwa jasho lake.



Toto la bata , lazima lionee wivu toto la kuku wa kienyeji.
Toto la kuku, chakula latafutiwa na mama.
Mama pia ni mlonda au kwa jina maarufu, mlinzi.

Ukicheza karibu na wanae, waparuriwa.
Toto la kuku lina ustaarabu!

Ushastukia toto la kuku huchuchumaa likienda haja kubwa wakati toto la bata laweza harisha likitembea?

DUH!

Lakini.....

Tatizo ni kwamba :
  • ramani ya misafara ya kuku haiwekewi kumbukumbu.
  • kila siku , inaenda ilimradi chakula chafika tumboni .
  • kuku anadhani kibanda ni nyumba yake wakati mfugaji amuona kuku na kibanda chake kuwa ni mali zake.
Tatizo linalozidi kujitokeza ni kwamba, toto la kuku likikua linarithi mfumo lililoukuta kwa wazazi wake. Ni vigumu kustukia kuwa kilichomkuta baba yake(jogoo) baada ya mwenye kibanda kupata wageni, ndio kitakacho mkabili Kijeba aka Toto la Kuku, mfungo Ramadhani ukiisha.

DUH!

Swali:
Ushawahi kustukia waitwao wananchi mara nyingi ndio wasiomiliki nchi?

Sitaniiii!
Turudi kwenye hoja;

  • Kama mwananchi anajivunia nchi yake wakati akipatacho kwenye nchi ni sawa na uhuru wa kuku wa kienyeji, je, hiyo ni nchi yake?
  • Kama siyo nchi yake, ni nani anaimiliki ambaye wametofautiana mitazamo mpaka mwananchi anajidanganya kufikiria kuwa yeye ananchi?
  • Au tuamke tu na kufanya tufanyalo ilimradi chakula chafika tumboni na tuko huru kwenda kulia na kushoto, bila kujali tupaitapo nyumbani kuna mtu mwingine anapamiliki?
  • Unafikiri Tanzania inamilikiwa na Watanzania au Watanzania wanawakilisha mtazamo mmoja tu, kati ya mitazamo ya makundi mawili tofauti yatumiayo sentensi moja na kuiita Tanzania;nchi yangu?
Swali:
Nani anaathirika sana kati ya kuku au toto la kuku, kwa kosa la kutomstukia mwenye kibanda?

Sina uhakika lakini kama kuku anafaidika sana kwa kumstukia mwenye kibanda lakini bado kutokujua nia yake au hata jinsi ya kupambana naye.
Duh!
Naacha basi!


Tulia na Seal





3 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:

Anonymous 11:23 am  

Hili sitalisahau...
serina

Simon Kitururu 12:16 pm  

@Serina:Kwanini?

Anonymous 7:28 pm  

maswali mingi siku nyingine...serina.

Idumu Jumuiya Ya Wanablogu Tanzania


Photo Sharing and Video Hosting at Photobucket

Partner

save mt. Kenya campaign
In partnership with africapoint.com

Taswira BANANGENGE

  © Blogger templates Romantico by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP