Nguvu ya Wasanii !AU?
>> Monday, January 15, 2007
Nakumbuka wakati ambao usanii haukuheshimiwa kabisa Tanzania.
Swali:
Hivi sanaa inaheshimika Tanzania?
Ilikuwa kawaida sana kusikia watu wazima wakiizungumzia sanaa vibaya.Hasa sanaa yenye asili ya tamaduni zetu za kiafrika.
Shule zetu ambazo zimehusika kutujenga kifikira , zimetujenga vilevile kuamini ukifuata mdundiko basi wewe hujaelimika.
Nakumbuka enzi zangu zakufuata mdundiko huku najifanya kama vile ni bahati mbaya tu kuwa ngoma na mimi tunaelekea njia moja!
Nakumbuka ilivyokuwa vigumu kujumuika barabarani katika kufurahia ngoma hii.
Nakumbuka kuwa hata dini zetu zimesaidia sana kutufundisha kuwa maswala ya ngoma na tamaduni zetu yanauhusiano sana na ushirikina, na hata shetani mwenyewe.lakini dini hizi hazikukawia kutuletea piano,violin nk. wakati zikiondoa ngoma zetu.
Chakujiuliza ni kwamba inakuwaje kwa wenzetu sanaa zao za asili na za zamani zina heshima zaidi kuliko hata hizi zisifikazo na tuzionazo na kuzisikia kila mahali?. Ukienda kwa waheshimiwa wa magharibi, utakuta kwao ujanja ni kujikusanyia kazi za sanaa za zamani na miziki ya zamani wengine waiitayo classical nakadhalika.
Sasa sisi Watanzania ambao tutazaliwa kesho tutazikuta hata dalili za sanaa zetu za zamani?
Sisemi kuwa sanaa zetu za sasa sio poa, sisemi kuwa za zamani ndio bora zaidi, nachojiuliza ni kwamba tunaziheshimu na kuzitunza sanaa zetu?
Mimi naheshimu sana wasanii na kazi zao. Nasikia siku hizi kuna dalili kuwa heshima kwa wasanii na sanaa inazidi kukua Tanzania. Na nasikia ni kwasababu imejulikana kuwa wasanii wanaweza kupata fedha kwa kutumia vipaji vyao na kuishi maisha mazuri tu. Nachojiuliza ni kama tumegundua kuwaheshimu wasanii wa Tanzania kwa sababu baadhi yao wamefanikiwa kutuzidi, lini tutajifunza kuwaheshimu kwa kazi wazifanyazo?
Lini tutawaheshimu kwa elimu watupayo...nk?
Wasanii wana nguvu sana! Na naamini kuwa sanaa imekuwa na itazidi kuwa shule kubwa kwa jamii yetu Watanzania.Hata katika kipindi kilichokuwa kawaida kabisa kudharau wapiga na wacheza ngoma za kienyeji. Ngoma hizi za kienyeji zilikuwa na ni shule ambazo zimehitimisha asilimia kubwa ya Watanzania vijijini na mjini.Na ukizingatia zaidi vijijini ambako asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi , unaweza hata kujua wanafikiria nini kwa kufuatilia nyimbo za ngoma za asili zinasemaje.
Hapa nimeongelea ngoma sana nikizungumzia sanaa. Kunawengine wanafikiria miziki tu wakifikiria sanaa! Nataka kukukumbusha kuwa naongelea sanaa kwa mapana na marefu yake hapa.
Swali:
Hivi kwanini hizi ngoma zinaitwa za kienyeji?
Msanii: Sema Yeee!
Watu: Yeeeee!
Msanii:Mikono ju! mikono juu!
Ukumbini:Watu wote mikono juu.
Kuna nguvu za wasanii ambazo mimi daima hunistaabisha sana!Naongelea wasanii wa aina zote.Lakini kuna Amri za baadhi ya wasanii naamini ndio zitiizwazo mara nyingi kwa furaha na bila mabavu kutumika kabisaaaaa!
Mcheki Bobby McFerrin alivyoushika ukumbi hapa chini hata bila kuongea
Huyu jamaa ni miongoni mwa wasanii ambao nimewashuhudia akikamata ukumbi akiwa pekee bila chombo chochote cha muziki na akawakamateni kwa zaidi ya saaa mmekaa kitako mkifurahi.Kama ushawahi kujaribu kukaa mbele ya watu unaweza ukajua ugumu wa kuushika ukumbi hata ukiwa na bendi nzima.
Mcheki hapa :
Wasanii mnanguvu sana za hata kuingiza watu mkenge bila wao kujijua.
Swali:
Au ndio maana wazazi wengi hupenda kuwaepusha mabinti zao kuwa na mahusiano na wasanii?
Hivi wasanii mnatumia nguvu zenu za usanii kusema nini au kutufundisha nini?
Nakubali mnatuburudisha.
Asanteni!
0 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:
Post a Comment