Mtakatifu SIMON KITURURU - MAWAZONI

FALSAFA na WAZO ndani ya neno - DUH!

Saikolojia ya kumpiga Mwizi

>> Saturday, January 06, 2007

Mtu.1:Mwiziiii!Mwiiizi!Mwiiizzziii!
Mtu.2:Piga huyoooo!...
Mtu.3:Hivi kaiba nini?
Watu:Hatujui lakini nasikia kamuibia mama mmoja , piga huyooo!Pumbafu kabisa huyo!!

Binadamu ni kiumbe kinachopenda kufuata mkumbo kikipewa mazingira yafaayo.Nachojiuliza ni kwa jinsi gani watu Tunasahau hili. Sababu kubwa kwa hili ni tabia ya binadamu yakupenda kurahisisha mambo. Karibu kila kitu binadamu anacho gundua au kupenda kutumia sana ni kifaa kirahisishacho mambo.Kuanzia kijiko, ngazi, baiskeli, jembe, nk. Lakini jambo kubwa binadamu analopenda kurahisisha ni kufikiria. Nirahisi kufuata mkumbo kuliko kufikiria na kuanzisha mambo au jambo mwenyewe.
Madhara yake ni kwamba mfumo huu uliopo duniani sasa hivi ambao umetutenga Afrika ni vigumu kuuondoa.Visingizio tunavyovingi.Kimojawapo ni kuwa kila mtu na maisha yake.Kwa hiyo kama mimi na familia yangu mambo si mabaya basi hakuna haja sana ya kuangaika.Kisingizio kingine ni kuwa ni afadhali zimwi ulijualo kuliko zimwi usilo lijua.
Lakini hivi zimwi hili tunalijua?

Ushawahi kuona watu wanampiga mwizi? Ushasikia jinsi maaskofu na wachungaji wakihutu na kitutsi walivyo shiriki katika chinjachinja?

Nachojaribu kusema ni kwamba, naamini katika kila mtu kunakisehemu kinachoweza kuvuka mpaka.Na katika kila binadamu kunakisehemu kinachojaribu kuhalalisha mambo bila fikira.Kwasababu ni ubinadamu. Lakini ni ubinadamu pia kujua nini kinaendelea na kujikwamua katika zimwi hili ambalo halijatunufaisha Waafrika.
Nimesoma jinsi watu wanavyomshangaa Ditopile kuua!Hivi akikwambia lengo lake lilikuwa si kuua utapinga?

4 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:

Anonymous 2:05 pm  

Ndugu Kitururu,

Mwizi anayepigwa ni yule wa kariba ya vibaka/mapanja/chori; kwa mfano pickpocket, wapora simu za mkononi, pochi, mikufu, saa, heleni, kofia nk, waanua nguo, wezi wa mizigo kwenye vituo vya usafiri, wezi wa bidhaa sokoni na madukani, na hali kadhalika.

Wezi wa kariba ya wezi: kwa mfano wanaosaini mikataba feki ya kiserikali, wanaoua mashirika na makampuni ya umma, wanaozidisha bei za bidhaa wanazotumwa kununua na serikali, wanaouza rasilimali ya taifa kwa bei mchekea, wanaojiuzia mali za umma kwa bei mchekea,wanaoiba malipo ya usafiri, malazi na vyakula kwenye ziara za ndani na nje ya nchi, na hali kadhalika. Hawa hawapigwi ng'o!

Ndugu Kitururu, wezi wa kabila niliyoitaja hapo juu, hawapigwi ng'o! Vyombo vya dola iwe polisi, akiwaona wezi hao utaona suruali yake inavyofyata matakoni kwa saluti kali. Iwe Jaji, utamsikia atakavyotumia misamiati na nukuu za kesi zilizotokea Uingereza karne tisa zilizopita ili tu amchomoe mtuhumiwa. Iwe Bungeni, utaona unafiki utakavyozuka na kuunda tume zisizo na maana yoyote au kwa staili ya siku hizi Mheshimiwa Spika atamlazimisha Mheshimiwa Mbunge kuikanusha kauli yake. Iwe Rais, utamsikia katangaza rishafo!

Hayati Franz Fanon, kwenye kitabu chake Wretched of the Earth, alisema "..wakandwamizwaji wakimshindwa mkandamizaji huwa wana tabia ya kuanza kukandamizana wao kwa wao.." Ikifikia hapo ndipo panapozuka Mgambo wa City kumpiga Mmachinga. Polisi kumpiga Mzururaji. Mzururaji kumpiga kibaka. Kibaka kumpiga mzururaji. Kolokoloni kumpiga kibaka. Kibaka kumpiga kolokoloni. Lakini katu huwezi kusikia Wamachinga wamemdindishia RC Kandoro. Au Makondakta wa Daladala na raia wengine wamempiga hadi kufa RC Ditopile baada ya kumuua kondakta mwenzao. Lakini utasikia kwenye taarifa za habari na kusoma vichwa vya habari magazetini "Wananchi wenye hasira waua majambazi sita" "..vibaka kumi mahututi kwa kipigo.." "..Wezi wanne wa mifugo soko la Vingunguti wakipata cha moto toka kwa Wananchi.."

Kamwe huwezi kusikia "..Wafanyakazi Bora Shoes Limited wampa kibano Meneja Mkuu kwa kufilisi kampuni.." "..Balozi aliyefanya dili feki alakiwa kwa kibano Uwanja wa Ndege Dar.." "..Wananchi wakusanyika Wizara ya Nishati kutaka kujua hatima ya IPTL, Richmond na Umeme wa Mgao.."

Hii ina maana kwamba Saikolojia ya Kumpiga Mwizi inafanana na wanaotekeleza saikolojia hiyo, ambao wengi wo huwa ni maamuma masikini.

Masalaam,

F M Tungaraza.

Simon Kitururu 3:20 pm  

Nakubali kabisa Mtimkumbwa.

Anonymous 1:39 pm  

Mti Mkubwa,
Umeelezea sawa kabisa kuhusu saikolojia ya wakandamizaji. Wakati vibaka wa elfu kumi tunawaua, wezi uliowaita "wezi wa kariba ya wezi" (ambao ni wezi wa mabilioni) si tu tunawacha, hatuwaui. Bali tunawachagua wawe viongozi wetu.

Akitokea mtu akaiba mabilioni kisha akakamatwa, utasikia watu mtaani wakisema, "fulani mjinga kweli. kaiba mabilioni akakimbilia Mbeya badala ya kwenda nje ya nchi?" Hawa huwa tunawashabikia na kuwaona wajinga pale wanapokamatwa. Badala ya kufurahia wezi wanapowekwa mikononi mwa sheria tunashangaa kwanini hawakutumia mbinu kali zaidi ili waepuke mkono wa sheria.

Hapo ndio Frantz Fanon anatupa jibu.

Anonymous 3:15 am  

Jela miaka 105 kwa wizi



na Magdalena Ally, Morogoro


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro imemhukumu Frederick Shimweta (29), mkazi wa Mtaa wa Sultani katika Manispaa ya Morogoro kifungo cha jumla ya miaka 105 gerezani baada ya kumkuta na hatia katika makosa 21 yanayohusiana na wizi wa sh milioni 1.5.


Adhabu hiyo litolewa bila ya mshitakiwa kuwapo mahakamani kwa kuwa alitoroka wakati alipoachiwa kwa dhamana, wakati kesi inasikilizwa.


Akisoma hukumu hiyo, hakimu wa mahakama hiyo, Jafari Mzonge, alisema kuwa mshitakiwa aliiba fedha hizo kutoka kwa mwajiri wake, Kampuni ya mafuta ya Simba Oil, ambako mshitakiwa aliajiriwa kama muuza mafuta.


Hakimu huyo alisema adhabu hiyo imetokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa mashitaka ambao haukuacha shaka yoyote katika kuthibitisha kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo.


Hata hivyo hakimu huyo aliutaka upande wa mashitaka kufanya jitihada za kumkamata mshitakiwa huyo ili aweze kutumikia kifungo hicho na kuwa haki ya kukata rufaa dhidi yake ipo endapo mshitakiwa huyo ataona mahakama haikutenda haki.


Awali, ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashitaka, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Edga Godwin, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo katika siku 21 tofauti za mwezi Machi na Aprili mwaka 2003 majira ya usiku wakati akiwa zamu kituoni hapo.


Alidai kuwa bila halali na akijua kuwa kufanya hivyo ni kosa kisheria, mshitakiwa aliiba fedha za mauzo ya lita 7,840 za mafuta ya dizeli na petroli.

Idumu Jumuiya Ya Wanablogu Tanzania


Photo Sharing and Video Hosting at Photobucket

Partner

save mt. Kenya campaign
In partnership with africapoint.com

Taswira BANANGENGE

  © Blogger templates Romantico by Ourblogtemplates.com 2008

Back to TOP