Yote Maisha ,Yote Shule! Naheshimu shule ikufunzayo kwa kukupiga ngwala
>> Sunday, January 07, 2007
Nakataa kukubali kuwa mambo barani Afrika yatakuwa katika hali ya kusikitisha daima. Naamini tukiendelea kujielimisha na kuelimisha wenzetu nini kinaendelea duniani tutafikia hatua ambayo hakutakuwa na ujanja zaidi ya kujikomboa, kujiheshimu, na kupendana au kujifunza kuishi pamoja huku tukijua kuwa tunahitajiana hapa duniani.Kujielimisha hapa namaanisha kuzingatia mafunzo ya shule ya maisha, shule ya uzoefu, shule uipatayo kwa kupigwa ngwala na pia shule tuipatayo baada ya kuona mwenzetu kapigwa mueleka.
Baadhi ya mafunzo haya hupatikana kwa kuishi katika eneo fulani. Nimekutana na mijadala mingi mtandaoni kuhusu faida na hasara za wabongo kukaa ughaibuni. Kuna hasara nyingi na faida zake. Lakini kama kuna faida moja niijuayo ni ile ya kupata funzo kwa kupigwa ngwala na hali halisi.Nakumbuka bongo tulikuwa tunaimba nyimbo za kumsuta kaburu kwa ubaguzi na nilikuwa nafikiri najua ubaguzi ni nini. Kusema ukweli ubaguzi hauwezi kuuelewa kwa kusoma kitabu au kuaangalia sinema. Ni mpaka ukutane nao uso kwa uso uwe unakulenga wewe ndio hapo utajua ladha yake. Kuna maswali mengi yanaulizwa kuhusu tofauti za ughaibuni na bongo! Hakuna mtu mwenye jibu moja kwani hali halisi kwa kila mtu ni tofauti na shule ya maisha ni tofauti kwa kila mtu akutananaye nayo.Hapa siongelei watu watembeleao nchi nyingine kwa wiki kadhaa na ambao hawaishi na mifumo ya nchi hizo.Hapa siwaongelei mabalozi ambao kwa taratibu ofisini kwao ni nchini mwao. Hapa nawazungumzia watu ambao wanaingia mtaani wanakabiliana na wazawa walalahoi na waliofanikiwa.Wanakutana na kujifunza kutoka kwa watu wa kawaida mtaani kwa kupigana mieleka ya kiakili, kisaikolojia na hata ya kinguvu za mwili. Hapo ndipo unaweza ukasema umeenda shule ya maisha ughaibuni.Na shule hii mafunzo yake hayasahauliki. Na shule hii katika mengi ikufundishayo ni kumjua mtu unayekabiliana naye.
Dondoo:
JE, UNAKUMBUKA HADITHI ZA JESHINI?jE , KUNA WATU WAWILI WALIOWEZA KUKUSIMULIA KUWA WALILIKABILI JESHI KWA NJIA ZILIZOFANANA?
Kwanini ninaongelea shule hii?
Naamini Afrika imenyonywa sana na mataifa ya magharibi ,kiarabu na kwingineko. Na bado inanyonywa sasa hivi!Basi kama kunakitu kiitwacho adui au kitu chakujiadhari nacho itakuwa ni mataifa haya mageni ambayo yamebobea katika kutuingiza mkenge. ILI KUMSHINDA ADUI SHARTI UMJUE ni kiini cha kujikwamua katika janga.Na narudia hakuna shule nzuri ya kumjua mtu kama kuishi naye kwake ambako haitaji kujifanya mzuri ili akuridhishe.Basi kwa hilo walioko ughaibuni wanapata shule nzuri sana.
Naamini watu wengi hapa duniani hasa Afrika kwa muda mrefu tumenyonywa na mataifa ya nje kutokana na kutokujua ni nini wanafanya na ni nini kinaendelea. Naamini pamoja na watu kwenda shule, kuna mambo mengi watu hujifunza kwa kukabiliana na hali au hata kupigwa gwala na halihalisi.
Mara nyingi tunapoishi na kukabili siku hadi siku ni rahisi kusahau kuwa kila siku ni siku moja ya shule katika maisha. Mara nyingi tuongeleapo shule humaanisha mahali paitwapo shule na elimu ni ile ifundishwayo shule na mtu aitwaye mwalimu. Kwangu mimi naamini nimejifunza mengi mashuleni na mengi nimejifunza kutoka katika mazingira ya shule bila mtu aitwaye mwalimu kuhusika. NAAMINI KILA MTU NI MWALIMU NA KILA MTU NI MWANAFUNZI.
Ngoja nikuelezee baadhi ya elimu niliyopata mtaani ambayo mpaka leo inanipa mwelekeo wa maisha.Nakupa baadhi tu ya mambo ambayo nilijifunza kutokana na kuwepo mahali bila ya funzo hilo kuwepo kwenye silabasi.Kwani naamini kila siku tunafunzwa kitu fulani iwapo utafungua macho na kujifunza.
Ninaanzia nilipo kwenda shule ya vidudu ya Jeshi, Mbeya,wakati nakaa Simike .Pale nisichokisahau ni jinsi nilivyoumwa na mbwa wa Jeshi baada ya kuwachokoza kwa kuwapiga na rungu nililolitengeneza kwa kutumia lami.Nilijifunza kuwa pamoja na kujiamini, haitoshi nilijifunza kujenga heshima kwa wanyama.
Nikaendelea shule ya vidudu ya kanisa la Katoliki,Songea . Hapo pamoja na kujifunza kuwa mahiri katika AEIOU,nilipata darasa la mambo ya dini ambayo yananizingua mpaka leo hii.Pia ndio mara ya kwanza kujua wakubwa wananywele sehemu za siri, kwasababu mlinzi wa shule alituonyesha.
Dondoo:
HIVI KWANINI SHULE HIZI HUITWA ZA VIDUDU?KWA NINI SHULE HIZI SIO ZA MSINGI?
Nikaenda kuanza shule ya msingi Mfaranyaki.Hapo nakumbuka ni mara ya kwanza katika kupigana nilipigwa na mjamaa aitwaye Deogratus ,nimesahau jina lake la ukoo.Tulipigana raundi mbili zote nikapigwa.Nilivyopigwa raundi ya kwanza nilidai kwasababu ya viatu.Tulivyovua viatu nikapigwa tena nikavimba jicho nikasingizia aliniwekea pilipili jichoni.Funzo nililolipata kisawasawa ni jinsi gani mtu mwingine anavyoweza kunizidi nguvu kisawasawa. Hapa ,Mfaranyaki pia nilishikwa nikimbashia msichana darasani na mwalimu ambaye alikuwa ni rafiki wa wazazi wangu.Hakunisemea nyumbani lakini tokea siku hiyo sijawahi kubashia mwanamke tena hadharani , labda hata chobisi.Hapa Mfaranyaki ndio nilikutana na msichana wa kwanza ambaye nilimpenda kama msichana.Ingawa alikuwa anaishi mbali na nilipokuwanaishi nilikuwa najaribu kupita nje ya geti lao ilimradi nimuone tu ,halafu narudi nyumbani nikiwa mwenye furaha.Nilijifunza sana kuandika barua za mapenzi,nilifanya majaribio ya kuweka poda na hata kuchora maua.Kwa bahati mbaya barua yangu moja ya mapenzi ilishikwa na dada yangu na kusomwa na familia nzima !Nafikiri unajua jinsi gani nilitaniwa na jinsi gani niliingia aibu.Kwani hata umahiri wa kauli kwa wanadada sikua nao.Nafikiri unajua nilijifunza nini hapa.
Nikahamia shule ya Mchikichini ,Morogoro. Hapa ni sehemu ya kwanza nilipogundua kupendwa na wanawake na pia kugundua si kila umpendaye anaweza kukupenda pia.
Nafikiri utagundua kuwa hapa nilikuwa katika kipindi gani kwa maana mapenzi na wanawake walikuwa muhimu. Kipindi hiki nilipata uhakika kuwa wazazi sio ukweli kuwa hawaishiwi pesa.
Nikahamia Morogoro ,Sekondari. Hapa kwa mara ya kwanza niliona maiti ya mwanafunzi mwenzangu wa darasa moja ikining'inia kwenye kitanzi cha kanga, ambaye alijiua kutokana na matatizo ya kifamilia.Hili jambo mpaka leo silisahau.Huyu mwanadada alikuwa yuko sawa tu darasani. Anacheka na kila mtu darasani.Mchana tulivyoenda kula iliturudi shuleni baadaye akajiua.Nilijifunza si kila akuchekeaye anafuraha moyoni. Hapa Moroseki pia niliitiwa kundi ilikunipiga kutokana na kumtosa mwanadada kimapenzi.Cha ajabu kundi lilokuja kutaka kunipiga ni la marafiki zangu au watu niodhani ni marafiki zangu.Sikupigwa kutokana na wao wenyewe kuona aibu.Lakini nilijifunza jinsi gani mwanamke ananguvu yavishawishi.Aliweza kututenganisha marafiki kirahisi tu. Nilipoteza marafiki wengi kwa mara moja kwa mara ya kwanza siku hiyo.Nilijifunza kuchagua marafiki.Wakati niko Morogoro Sekondari pia ndio mara yangu ya kwanza kuanza kufanya kazi kama kiongozi wa misafara ya wageni kutoka nchi za nje, waendao vijijini kujifunza maisha ya Kiafrika.Nilipata kazi hii kwa sababu ya kujua ung'engé. Kwa mara ya kwanza nilijua utamu wa pesa uliyoitolea jasho.
Nikahamia Mazengo Sekondari, Dodoma. Hapa jambo kubwa nililojifunza ni jinsi ya kuishi na watu mbali na nyumbani.Nilijifunza pia umuhimu wa chakula.Hapa sisi wanafunzi tulikuwa tunachukia vyakula vya shule lakini wanakijiji kutoka vijiji vya karibu walikuwa wanakuja kuokota maugali hata ambayo wanafunzi wametupa au kudondosha kwenye michanga.Baadaye nilikuja kugundua kuwa wakisha okota vyakula hivi huenda nyumbani kuvianika halafu hutwangwa nakuwa unga tayari kwa msosi wa nyumbani.Nilijifunza pia ladha ya maji hata msosi huzoeleka ukikabwa na kiu au njaa kisawasawa.Unakumbuka ladha ya maji ya dodoma yana chumvichumvi?
Yote Maisha , Yote shule!
Sababu za kukukumbusha kuwa kuna mambo tuyakumbukayo na ambayo yanachonga jinsi tunavyopiga hatua hapa duniani ambayo hayana uhusiano wa moja kwa moja na madhumuni yaliyowekwa wazi kwanini tuko sehemu fulani na ni nini tunafanya.Naamini unajua hilo, lakini naamini ni muhimu kukumbushana umuhimu wa elimu hizi zitulengazo kila siku bila ya sisi kupanga. Kwa wanafunzi baadhi ya masomo muhimu kisawasawa tujifunzayo hayahusiani na yanayofundishwa darasani.Siwezi kusema kuwa yanayo fundishwa darasani hayakunisaidia au nilikuwa siyamudu!Nikisema hivyo nitakuwa naongopa. Nachojaribu kusema ni tuwe na busara ya kujifunza na kutenda kwa vitendo ili kuboresha maisha yetu katika muda huu mfupi tuishio.Tuyape kipaumbele mafundisho ya darasa hili la maisha hata katika kipindi hiki ambacho watu weusi tunajaribu kujikomboa kutoka katika makucha haya yatunyanyasayo hapa duniani.
Nafikiri unajua sasa kua hapa maishani mimi niko shuleni.Hapa nimekazia kujifunza kutokana na maumivu.LAKINI TUJIFUNZE PIA KUTOKANA NA ULAINI,STAREHE,nk wa baadhi ya mambo yatukumbayo.
Narunia:
ILI KUMSHINDA ADUI SHARTI UMJUE, LAKINI INABIDI UJIJUE!Kujijua na kumjua tutumie nyenzo zote tulizo nazo.
Kuna madarasa mengi ningependa kufaulu na mojawapo ni hili la mapenzi. Auningependa niamke tu siku moja halafu niwe na hakika asilimia mia moja kama Billy Ocean asemavyo hapa chini.Lakini najua hii ni ndoto tu kwangu.Mimi ni miongoni mwa wale ambao hata nicheze bahati nasibu sipati.Ni mpaka ni toe jasho.
4 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:
Saimoni,nakubaliana na wewe kabisa.Ipo siku bara letu huizi hadithi za "Starving children in Africa" zitakwisha na akina CNN na BBC watakosa habari kabisa za Afrika ni hapo ambapo tukatkuwa tumajikomboa kutoka katika makucha ya hawa ambao siku hizi tunawaita wawekezaji.
Lakini katika kujikomboa huko tunahitajika kuwajua maadui wetu na kujifahamu sisi ni akina nani na tumetoka wapi.Nafikiri hapo kama kuwafahamu hawa wakoloni wengi wetu tumeshawafahamu lakini kufahamu tulipotokea bado inakuwa ngumu kufahamika kwa kila mtu.
Simon,
Habari hii ni muafaka kabisa kwa kufungulia mwaka.Nimeisoma kwa makini huku nikijiuliza pia njia nilizopitia,mafunzo ya maisha niliyoyapata bila msaada wa wazazi au walimwengu bali mwenyewe.Majibu ni mengi,mengine bado yananihuzunisha na mengine yananivunja mbavu kwa kicheko kama sio tabasamu la mwendawazimu.Hapa Canada mambo haya yanaitwa life skills na ni somo ambalo linasisitizwa sana miongoni mwa vijana na wananchi kwa ujumla.
Kama ulivyosema,ni muhimu sana kujijua kwanza.Ni muhimu zaidi kwa sababu huwezi kujiongopea kuhusu wewe mwenyewe.
Kuhusu mapenzi; hii ni sanaa na sidhani kama kuna ambaye ashaiweza au kuielewa vilivyo.Ndio maana mpaka leo vitabu vya mapenzi na saikolojia yake bado vinauzwa kama njugu.Mapenzi,kwa mtazamo wangu,ni maisha.Mwisho wake ni futi sita ardhini.Kheri ya mwaka mpya.
... na hilo swala la kuishi mtaani na kuwajua wenyeji, kuujua ubaguzi na kujua jinsi ya kukaza nia.. na kama ilivyo nyumbani kuwajua binaadamu... tafakuri safi mzee mwenzangu.
Yote maisha. Vita mbele.
A luta continua
Post a Comment