Invitation for Bids - Meru Residential Apartments
>> Monday, October 17, 2011
SHIRIKA LA NYUMBA LA TAIFA
KUKARIBISHWA MAOMBI YA KUNUNUA NYUMBA 30 ZILIZOKO MJINI ARUSHA
Shirika la Nyumba la Taifa linawakaribisha watanzania wakazi na wasio wakazi kuleta maombi ya kununua nyumba zake zilizojengwa mjini Arusha. Nyumba hizo ambazo zinaitwa “Meru Residential Apartments” zinatarajiwa kukamilika ndani ya miezi mitatu (siku 90) kuanzia tarehe 1 Oktoba,2011.
MRADI WENYEWE:
Meru Residential Apartments zimejengwa kwenye mandhari murua inayokupatia maisha bora katika jamii yenye usalama. Zimepewa jina hilo kama ishara ya kuuenzi Mlima wa Meru ambao ni mlima wenye Volcano hai nchini Tanzania wenye urefu wa mita 4,566 (futi 14,980), ukiwa ni mlima wa kumi kwa urefu barani Afrika.
MAHALI ZILIPO:
Meru Residential Apartments ziko mjini Arusha kwenye eneo la katikati kabisa, kwenye mtaa wa Wachaga, Kiwanja Na. 565/I. Eneo hilo liko umbali usiozidi kilomita mbili toka ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), nyumba hizo zimepakana na hospitali ya Selian na Chuo cha Ufundi, na kwa upande wa mashariki inakupatia muonekano mzuri wa Mlima Meru.
MAELEZO YA NYUMBA HIZO.
Idadi ya Nyumba | 30 |
Ukubwa eneo la nyumba | 169.45 |
Idadi ya Majengo | 2 |
Idadi ya ghorofa kwa kila jingo | Ghorofa nne |
Idadi ya vyumba kwa kila nyumba | 3 (kimoja kinajitegemea) |
Sifa nyingine za nyumba hizo | Sebule kubwa, chumba cha kulia, jiko,stoo,bafu na choo [ Nyumba zinauzwa bila samani (furniture)] |
Kila nyumba ina maegesho maalum ya gari, pamoja na tanki la maji la lita 1000. |
BEI ZA NYUMBA HIZO:
Bei ya chini kabisa ya kila nyumba ni shilingi za Kitanzania 175,314,366.48 bila kujumlisha kodi ya ongezeko la thamani. Mwombaji atakayetoa bei ya juu zaidi na kutimiza masharti yote yaliyoelezwa hapo chini ana nafasi kubwa zaidi ya kuuziwa.
TARATIBU ZA KUOMBA:
Waombaji wanatakiwa kuzingatia utaratibu ufuatao:
- Wanaopenda kununua nyumba wachukue fomu za maombi kutoka Makao Makuu ya Shirika, kwenye ofisi za Shirika zilizopo Arusha, au kwenye ofisi yoyote iliyo karibu nao. Fomu zinapatikana pia kwenye tovuti wa Shirika (www.nhctz.com).
- Fomu za kuomba kununua zijazwe na kuwekwa saini na kurejeshwa kwenye ofisi za Shirika pamoja na barua ya kuonyesha kiasi ambacho mwombaji yuko tayari kulipa. Shirika litahitaji pia ushahidi wa malipo ya shilingi 10,000/=(Malipo yasiyorejeshwa) kama ada ya maombi na malipo ya asilimia kumi (10%) ya awali zilizolipwa kupitia benki kulingana na thamani ya nyumba uliyochagua.
- Waombaji wote waliofanikiwa wataandikiwa barua kujulishwa hivyo. Watapewa siku 90 toka tarehe ya barua hiyo kukamilisha malipo ya asilimia tisini (90%) iliyosalia kulipia nyumba husika. Utaratibu wa kulipa unaweza kuthibitishwa kwa kulipa pesa kwenye akaunti ya mradi au kuonyesha hati ya mkopo toka benki.
- Kama uthibitisho wa malipo hautawasilishwandani ya siku 90, mnunuzi atanyang’anywa na nyumba hiyo kuuziwa mtu mwingine toka kwenye orodha ya waombaji. Mnunuzi aliyeshindwa kulipa hiyo asilimia tisini (90%) ataruhusiwa kutumia asilimia kumi (10%) ya awali kulipia nyumba kwenye mradi mwingine. Aweza pia kurejeshewa fedha zake kwa kukatwa asilimia mbili (2%) ya kiasi hicho.
- Mwisho wa kuwasilisha maombi ni Jumatano tarehe 4 November, 2011 saa 4:00 asubuhi.
- Maombi yapelekwe ndani ya bahasha yenye rangi ya hudhurungi/kahawia iliyoandikwa juu;”Maombi ya Kununua Nyumba za Meru-Arusha”.
- Maombi yote yapelekwe kwa: Meneja wa Mkoa, Shirika la Nyumba la Taifa, S. L. P 883, ARUSHA
0 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:
Post a Comment