EMU THREE aka Muzee wa STORI katika kuhojiwa!
>> Monday, August 29, 2011
   
Karibuni katika mahojiano yetu ya kila week. Week hii nimepata bahati kufanya mahojiano na Emu Three ktoka blog ya Diary Yangu.  Kama wewe ni mpenzi wa riwaya natumaini mara ukiifahamu hii blog kila  siku utajikuta utarudi kusoma hadithi moto moto anazoziandika Emu Three.  
Karibu hapa na tunafurahi kuweza kufanya mahojiano na wewe. Unaweza kutueleza kidogo kuhusu wewe na blog yako?
Mimi  naitwa emu-three, na nimetumia emu-three kama ufupisho wa majina yangu  matatu yaani jina la kwangu la baba na la ukoo yote yakianzia na herufi  M. Na wakati naanzisha hii blog, nilikuwa nawaza niweje jina gani , na  mara likanjia jina hilo la miram3. Mira ikiwa ni jina langu halisi kwa  kifupi na m3, ikiwa M.M.M. 
•	Je blog  yako unatumia jina lako kamili au unablog kwa kutumia kivuli kingine na  watu wanasoma na kuenjoy blog yako lakini hawajui wewe ni nani?
Blog  yangu situmii jina langu kamili, natumia jina la kubuni tu `nick-name’,  na watu wananitambua kama emu-three, kama nilivyosema awali kuwa ni  kifupisho cha majina yangu matatu. Sina nia mbaya kutojiweka jina kamili  na picha yangu, ila nililenga kuwa ninachokiandika ndicho kinieleze  mimi. Nia ni kutoa kile nilichokuwa nacho, lakini ikiwa ni muhimu sana  nitaweka picha yangu na kujielezea zaidi, hapo wapenzi wa blog hii  watakapokuwa wengi na kupendekeza hivyo.!
•	Ni miaka mingapi sasa umekua ukiblog?
Nina  miaka mitatu sasa tangu blog hii ianzee kuwa hewani, mwanzoni na  nilituma nianze kublog, kwani nilituma maelezo ya mwanzo kabisa kama  utambulisho tarehe 14-7-2009.
•	Ni nini kilikufanya uanzishe blog?
Mimi  ni mpenzi sana wa kuandika hadithi, kuweka kumbukumbu za matukio(diary)  na napenda sana kusoma vitabu vya hadithi, hasa riwaya(novels) ,  tamithiliya nk. Nikawa naandika visa, au hadithi katika makatasi, na  mwisho wa siku hayo makaratasi yanapotea au kuharibika, nikawa naandika  kwenye computa za ofisini, nazo zinakumbana na virusi, au unaondoka  kwenye hiyo kampuni na ina maana kila kitu kinamepotea. Nikaja kugundua  kuwa kumbe kwenye blog unaweza ukaweka hizi kumbukumbu, za visa, hadithi  nk na sio kuweka tu, bali unaweza kupata watu wakazisoma, na  mkachangiana mawazo. Na kwa vile nia yangu ilikuwa sio kuandika tu, bali  pia kutoa maoni yangu, kushauri,nk kuhusu hili na lile, nikaona blog ni  sehemu nzuri kabisa. Kwa mfano mimi ninaamini kuwa kuwa kila tukio  lazima lina na sababu, basi kwanini nisiweke hayo matukio na kuanisha  nionavyo mimi ni sababu gani likatokea kwa kupekenyua chanzo chake, na  hatimaye iwe kama kisa ambacho sio burudisho tu, bali kiwe na mafundisho  ndani yake!
•	Je, wewe kazi yako ni kublog tu au hii ni kama kazi ya muda tu au hobby?
Kwakeli  kublog niliichukulia kama Hobby, na nina kazi nyingine inayonifanya  niishi mjini, na kama utachunguza blog yangu haina hata matangazo ya  kibiashara, sio kwamba sipendi, bali sijawapata watu wa kutangaza  biashara zao. Kama kuna atakayependa kuweka tangazo lake namkaribisha  sana. Kwa ujumla natumia muda wangu wa ziada, gharama zangu mwenyewe, na  nashukuru kuwa naweza kutumia vitendea kazi vya muajiri wangu kuweza  kufanikisha hili, ingawaje ni kwa shida, na vinginevyo nategemea sana  internet cafe.
•	Nini changamoto unazozipata kwa kuwa na blog?
Changamoto  ni nyingi, kwanza kama nilivyosema awali muda mwingine nategemea sana  vitendea kazi vya muajiri wangu, kama computa na internet ingawaje  najitahis sana kutokutumia muda wake wa kazi, ninachofanya nikuwahi  asubuhii sana na kuandika kile nilichokusudia kabla ya muda wa kazi, na  zaidi sana natumia internet cafe. Kwahiyo swala la muda, gharama na  vitendea kazi ni changamoto kubwa kwangu kwa sasa. 
•	Ni nani wasomaji wa blog yako?
Ni  wote hasa wale wanaoutumia lugha ya kiswahili, ingawaje wengine  wanaweza kutumia nyezo zilizopo kwenye blogs, kutafsiri kwa lugha zao.  Matarajio kama ningeliweza, nilitaka iwe kwa lugha mbili ya Kiswahili na  Kiingereza, ili wengine waweze kutafsiri kwa kirahisi kwenye lugha zao  kwa kupitia kwenye lugha ya Kiingereza.
•	Ni nini imekuwa mkakati wako kwa ajili ya kujenga kujulikana kwa mwenyewe na blog yako zaidi?
Hilo  pia limekuwa ni moja ya changamoto kwangu, kwani nimejulikana labda kwa  kupitia kwenye blog nyingine ambazo wamenisaidia kuniweka kama blog  rafiki,  na wengine wamekuwa wakiambizana, na kuweza kuwavuta marafiki  zao kuja kusoma visa kwenye blog hii, nawashukuru sana kwa hilo. Kama  ujuavyo, watu wengi sasa hivi hawapendi kusoma, wanapenda zaidi  kutizama, na kwahiyo mtu akiona umeandika taarifa ndefu, na haina hata  kivutio kama picha anaghairi. Kwahiyo mkakati wangu ni kuiboresha hii  blog, iwe ya kisasa zaidi, iwe sio tu kusoma, bali hata kutizama pia. 
•	Je  unatumia mitandao mingine kama Twitter au Facebook kuitangza blog yako?  Kama unazo unaweza kutuambia ili wasiofahamu waweze kufahamu na  kukufuata? 
Ndio natumia Facebook,  hata Twitter, kwenye Twitter unaweza kunitafuta kama `emu-three’ lakini kwenye face book unaweza kunipata kama `diary yangu’
 au http://miram3.blogspot.com/
•	Je ni nini mkakati wako na blog yako kwa ujumla?
Mkakati  wangu ni kuiboresha hii blog kuwa ya kisasa zaidi, na kuweza kuingiza  e-book, kweny hii blog, nikipata wataalamu wa kunisaidia nitashukuru  sana, na kwa vile leng ni kuwa mtunzi wa vitabu, basi blog hii itakuwa  sehemu ya kujitangaza pia. Na ikiwezekana nisiifanye blog tu kama hobby,  lakini iwe kazi yenye kuleta manufaa, sio kwangu tu hata kwa jamii kwa  ujumla. 
•	Ni jinsi gani (mtu) anaweza kuelezea style/theme ya yako unavyo blog?
Mtindo  wangu wa kublog unaweza kuelezewa kama blog ya visa vya kusisimua  kutokana na matukio halisia. Ni kumbukumbu za kimaisha, kwani visa  ninavyotunga ni vitu vilivyotokea na mimi naviboresha tu ili viweze  kumsisimua msomaji.
•	Je ni bloggers wapi ambao wewe unawaangalia na kufuata nyayo zao? Na kwanini?
Kwakweli  kublog kwangu siwezi kusema nafuata nyayo za mtu fulani, sikumbuki kuwa  nimeblg kwasababu ya mtu fulani, hapana, mimi nilipogundua tu kuwa kuna  kitu kama hiki na unaweza kuweka vitu vyako bure, nikajimwaga, sio kwa  ushawishi wa mtu, lakini wengi tu napenda blog zao, ikiwemo hii yako, na  mimii huwa napenda sana kusoma walichoandika wenzangu, na nina imani  kuwa kitu kipya ni kile hujakiona, kwahiyo kila blog ambayo sijaiona  kwangu inanisismua kuisoma,na kuona mwenzangu ana nini katika mawazo  yake! 
•	Je unafikiria kuwa unadaiwa na mtu akiacha comment/s kwenye blog yako?
Kuna  jambo moja tuliweke akilini, mfano mtu akiweka comment kwenye blog  yako, lazima atakuwa na shauku fulani, hasa iwe ya kuulizwa swali, ...au  hata kama inakukwaza yeye atakuwa na matarajio fulani kuwa wewe mwenye  blog unaweza kwa kutumia blog yako kumsaidia au kumsikia. Kwahiyo ni  bora ukasema lolote, au usiitie kapuni, kwani ukifanya hivyo bila  kuiweka hewani au bila kusema lolote, utakuona kama umemdharau, kwakweli  ni deni...utakuwa hujamtendea haki mpenzi wa blog yako. Na pia kwa wale  wanaosoma habari kwenye blog, ni busara  pia ukasema lolote, kwani ni  kama mtu kakupa kitu ukae kimiya,..ni busara kusema ahsante  ...kwahiyo.unaweza hata ukaandika neno dogo tu la kushukurui au  ukaandika `mmmh’ inatosha kabisa, ni maoni yangu tu.
•	Je kuna  thamani kujibu comment iliyoachwa kwenye blog yako wakati ukijua kuwa  huyo aliyeiandika labda hatarudi kusoma jibu lake tena?
Ukiulizwa  swali ni vyema kulijibu, kwasababu mara nyingi ukikaa kimya  unatafsiriwa kuwa umezarau au sio, kwahiyo kinachotakiwa ni kulijibu  lile swali, kwani muulizaji anaweza kuwa aliuliza hilo swali kwa maslahi  yake, lakini swali hilo linaweza likawa limesomwa na watu wengi na hata  kuwagusa watu wengine, kwahiyo kama yeye hakurudi kusoma majibu ya hilo  swali watafaidika wengine, walioguswa nalo.
•	Je wewe ni mtu ambaye uko rahisi kukata tamaa?
Hapana  mimi spendi kukata tamaa, kwasababu sisi tunaishi na kilichokukatisha  tamaa kinaweza ikawa sababu ya kukupambanua ubongo wako ili ufikiri  zaidi. Cha muhimu ni kutafuta kwanini, na baadaye utagundua hata kile  usichokitarajia kwani wanasema tukio hutokea ili iwe sababu, na hicho  kinachmfanya mtu ajisikia kukata tamaa, ni moja ya jambo, ambalo  halijatokea hivi hivi, ushauri ni kupambana hadipumzi ya mwisho!
•	Ni nini  baadhi ya malengo yako ya mwaka huu kwa ajili ya blogu yako au unaonaje  mwenyewe  kwa kipindi cha mwaka mmoja ua mitano toka sasa hivi blog ya  itakuaje?
Malengo  ni mengi, lakini unapoigusa blog, utagundua hii ni nyanja inayokuwa,  kila siku kunatokea mabadiliko, ni kama mwanablog unatakiwa kujifunza  kwenda na wakati. Tatizo ndio hilo utafanyaje... Kwahiyo lengo mojawapo  ni kuiboresha blog hii, ili niweze pia kutoka kwenye hobby tu, na  kuingia kwenye kublog kama kazi, na ili nitoke kwenye kumtegemea muajiri  nifikie kwenye kujitegemea mwenyewe kwani kuna kesho na leo. Na nina  matumaini makubwa kuwa kwa kupitia blog hii niweze kuwa mtunzi bora, na  hata blog hii kuwa miongoni mwa blog..
•	Je upi ujumbe wako kwa wale watu wanaotaka kuanza kublog?
Kwa  wale wanaoanza kublog, ushauri wangu ni kuwa kublog ni rahisi sana,  kwani ni bure, muhimu ni muda wako tu, na kupangilia nini unachotaka  kuwaambia wenzako, na unapoutoa ujumbe wako pia ufikiri mara mbili  ,usiweke ujumbe wenye madhara, kwani watakaosoma ni wengi, wa rika  tofauti, dini na mataifa mengine, kwahiyo ujaribu kublog ukiwa na uoni  kuwa haitaishia tu kwa wale uliowalenga, itafikia hata wale usiotarajia  kuwa wataisoma blog yako.
•	Je kwa maoni yako ni lipi lengo kubwa kwa mwanablogger?
Lengo  kubwa kwa mwanablog ni nini unachotaka kukitoa kwa jamii, nini  ulichokusudia na ukijua hilo wewe anza kuweka hoja zako, kwani hoja  huzaa hoja. Blog sasa ni kama vijiweni, ukiwa na jambo lako jema, litoe,  huwezi jua, ukiwa na matatizo yako yatoe, huwezi jua...unaweza ukapata  msaada mkubwa sana, kwahiyo lengo ni wewe mwenyewe tu!.
•	Kuna jambo lolote ambalo hatukuliuliza na ungependa kuwaeleza wasomaji wa blog yako?
Labda  maoni tu kwa wanablog mbalimbali. Mimi kama mzazi limekuwa likiniuma  sana, ni sawa kila mmoja ana malengo yake, kila mmoja ana utashi wake,  lakini lazima mtu ufikie na kujiuliza kwa kina faida na hasara kwa  anachokifanya., lazima ujiulize hivi hiki ninachokifanya kitajenga au  kitabomoa. 
Kizazi  kinachokuja kinategemea sana msingi wa kizazi kilichopo, na busara yako  ndiyo itakayojenga, kama tutasema hewala, kila mtu ana akili yake,  tutakosea, wapo watoto wadogo ambao hawaajui jema na baya, wanapupa ya  kuiga, sasa ni vyema lile tutakaloliweka hewani liangale hiki  kizazi,....natumaini ujumbe huu utaeleweka bila kutafsiri zaidi.
Nakushukuru  sana kwa kunitupa fursa hii na sina cha kukupa zaidi ya kukuombea heri  na fanaka katika utendaji wako, kwani wewe umekuwa mtu wa watu. Kujali  wengine, ni kazi kubwa sana, inahitaji moyo, wewe hili umeliweza hilo,  shukurani sana.
Asante sana Emu Three Kwa kufanya mahojiano haya na sisis na tunakutakia mafanikio mema katika blog yako. 
Waliomuhoji ni hawa huku TANZANIAN BLOG AWARDS,..
..... nakiri nahusudu sana tu kazi zake  huyu MKUU! 
 




2 KOMENTI a.k.a Maoni. :-(:
Mkuu nahavome sana! Nashukuru kwa kuniweka hewani hapa kwako ndugu yangu, kwetu kumoja. TUPO PAMOJA DAIMA
Tuko Pamoja MKUU!
Post a Comment